ASALI MUBASHARA-Ijumaa 22/11/2019
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika asubuhi ya leo tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza. Hapa tunakutana na habari ya matumaini kabisa, habari ya ushindi kwa wayahudi. Adui waliyekuwa akipigana nao leo, yaani Antiochus Epiphanes na Wagiriki wenzake sasa ameshindwa, adui aliyewatesa, aliyeingiza sanamu na kuwaamuru Wayahudi waiabudu, aliyelikufuru hekalu la Wayahudi namna hiyo, aliyewaua viongozi wote wa Kiyahudi kwa kuwalazimisha wale nyama za nguruwe kama tulivyokuwa tunasikia kwa wiki sasa, sasa huyu anashindwa.
Wale wayahudi waliopambana kuupinga huu udhalimu nao wakiwa chini ya kiongozi wao aitwaye Yuda sasa leo wanatangaza ushindi na cha kwanza wanaenda Yerusalemu, wanaondoa ile sanamu iliyowekwa kule ndani ili waiabudu, sanamu iliyokuwa inalikufuru hekalu sasa wanaitoa huko na kulitakatifuza tena hekalu.
Ndugu zangu, hawa Wayahudi waliweza kushinda kwa sababu walikuwa wanapigana kwa ajili ya Bwana, hawakuwa tayari kuona hekalu la Bwana linageuzwa kuwa kama nyumba ya kipagani. Na kwa kweli Mungu alikuwa pamoja nao na kuzikirimia juhudi zao na mwishowe kupata ushindi. Katika somo la injili, tutasikia habari kama hii lakini hapa Wayahudi wanashindwa kuwa watu wa ushuhuda, wanalikufuru hakalu lao na kulifanya kuwa kama pango la wanyanganyi. Tunajua kwamba uzembe huu wa Wayahudi uliwafanya waje washindwe tena na warumi mwaka 70AD ambapo mji wa Yerusalem pamoja na hekalu lao uliangamizwa wote.
Ndugu zangu, hapa tunalo kubwa la kujifunza: ukimpigania Mungu, ukijiotolea kwa ajili yake, naye lazima atakulipa tu. Hatakuacha uaibike. Utajiona kwamba unateseka sana, mateso yatakuwa mengi mwanzoni-utaanza na kukata tamaa kidogo lakini ukishaanza anza tu-unashangaa kuona kwamba unashinda, ushindi unakuja. Unajiuliza yale mateso yote yalikuwa ni nguvu za soda tu na ndivyo ilivyotokea kwa Wamakabayo wa Agano la Kale.
Hivyo, ndugu usisiste kujiotolea kwa ajili ya Bwana. Bwana hatakuacha, atakukimbilia tu. Ukishamuweka mbele mateso yote yanakwisha. Tusisite kujitolea, kufanya kazi za kujitolea kuwasaidia wenzetu, kutumia muda kukaa na wenzetu na hata kuwatembelea wagonjwa. Kazi kama hizi huonekana kama upotezaji wa muda lakini nakwambia malipo yake ni makubwa. Jaribu nawe utaona.
Kingine ndugu zangu, tusikubali kuchafua miili yetu kwa dhambi kwani ni mahekalu ya Mungu. Tufanye jitihada kama Wayahudi katika somo la kwanza, tusafishe hekalu hili kwa sakramenti ya kitubio ili Mungu aweze kukaa ndani. Usikubali kuliharibu hekalu kwa chuki, kutokusamehe, umbea, usengenyaji, matusi, uzinzi, uasherati, kwa kufanya hivi unafanya mwili wako kuwa pango la dhambi! Utakasa na Kristo leo na usimike nguvu mpya ya kutumia mwili kwa ajili ya kuimba kusaidia maskini, mdomo kuombea watu nk. Utaonesha ukuu wa Mungu kwa kukuumba. Tumsifu Yesu Kristo.
©Pd. Prosper Kessy OFMCap.
*NB: SHAJARA YA ASALI MUBASHARA SASA ZIPO ZA KUTOSHA: Ukihitaji shajara ya “ASALI MUBASHARA” ya mwaka 2020 yenye masomo ya kila siku na tafakari zake za Asali Mubashara mwaka mzima wasiliana nami kwa number hizi 0755444471 au 0714002466. Shajara imeshiba na masomo mpaka na zaburi zimechambuliwa kuongeza ufahamu wa maandiko na kukuza hekima yetu kwa Mungu.* *Ukiipata utaipenda mwenyewe, itakusaidia mnoo*