Kundi la Wamisionari Wakatoliki Mtandaoni lilianzishwa mwaka 2010 wakati huo likiitwa Vijana Wakatoliki Tanzania, baada ya viongozi wa Vijana wa Parokia ya Familia Takatifu Njiro Jimbo kuu la Arusha kupata wazo la kuunganisha vijana wote Wakatoliki wa Tanzania kupitia Mtandao wa Facebook. Kundi hilo hapo awali lilipewa jina la VIWAWA FAMILIA TAKATIFU –NJIRO. Kundi lilipata umaarufu na kujulikana zaidi baada ya kongamano la Vijana Kitaifa lililofanyika Jimbo Kuu la Arusha 5-9 September 2011 na hivyo ikalazimika kubadili jina na kuliita VIJANA WAKATOLIKI TANZANIA ili kukidhi mahitaji ya wanachama walioanza kujiunga baada ya kongamano maana walitoka kila kona ya Tanzania.
Kijana yeyote Mkatoliki anapokelewa kujiunga na kundi. Tuna kila aina ya vijana na wasio vijana kwenye kundi wakiwemo Viongozi na wanachama wa Viwawa kutoka majimbo mengi ya Tanzania, Vijana ambao hawafungamani na chama chochote (Vijana Walei), Mashemasi, Mapadre na walei wengine. Hadi sasa Kikundi kina wanachama wapatao kwenye Mtandao wa Facebook Zaidi ya 9000 na wanachama 80 ambao ndio walio hai na wanaoshiriki shughuli za mara kwa mara za utume kwenye mitandao. Kwa sasa tunapatikana katika mitandao ya whatsap, instagram, telegram na kwa sasa tupo kwenye hatua ya mwisho ya kuanzisha website yetu.
Kati ya mambo ya msingi yanayofanywa ndani ya kundi ni Elimu juu ya Imani Katoliki. Kundi limekuwa msaada mkubwa kwa vijana wanaohitaji kuelimishwa juu ya jambo lolote ama changamoto yoyote kwenye imani Katoliki. Mashemasi na Mapadre walioko kwenye kundi wamekuwa msaada mkubwa kwa kujibu maswali mengi kwa ufasaha. Tunaamini tumetoa mchango mkubwa katika kuwasaidia Vijana kuielewa imani yao.
Aidha tunajivunia kuwa kati ya wadau waliokuwa mstari wa mbele kuhakikisha filamu iitwayo SISTER MARY, ambayo kwa macho yetu ilikuwa ikidhalilisha Ukatoliki iliyotarajiwa kusambazwa mwaka 2014 haitoki. Harakati zetu ziliwezesha filamu hiyo kuzuiwa kusambazwa.
Pia tulijaribu kuhamasisha kukomeshwa kwa mauaji na dhuluma mbalimbali dhidi ya makasisi na viongozi wengine wa kanisa, mambo yaliyoshika kasi hapo mwaka 2015.
Pia tumejiwekea utaratibu wa kufanya matendo ya huruma mara mbili kila mwaka; wakati wa Pasaka na wakati wa Noeli. Tunafanya matendo ya huruma kwa kuratibu michango inayotolewa na Wamisionari kote Tanzania kutoa michango yao ambayo hukusanywa kupitia mitandao ya simu na kisha kununua mahitaji husika. Toka tumeanza utaratibu huu mwaka 2012, tumeshafanya Matendo ya Huruma kwenye vituo vifuatavyo;
- Kituo cha Watoto Yatima cha Mburahati Charity Centre, Jimbo Kuu Katoliki, Dar es Salaam (Januari 2012)
- Hospitali ya Saratani ya Ocean Road, Dar es Salaam (Mei 2012)
- Kituo cha Kulelea watoto Yatima cha Camp Joshua, Arusha (Januari 2013)
- Kituo cha Kulelea Watoto walemavu na wenye Mtindio wa Ubongo cha Amani, Jimbo Katoliki la Morogoro (Aprili 2013)
- Kituo cha watoto walemavu wa akili cha Miyuji Cheshire Home, Jimbo Katoliki la Dodoma (Januari 2014)
- Kituo cha watoto yatima cha Nyumba ya Furaha (Cassa dell Gioia), Jimbo Katoliki la Tanga (June 2014)
- Watoto Wagonjwa wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam (December 2014)
- Kituo cha Kulea Wazee cha Welezo, Jimbo Katoliki Zanzibar (Aprili 2015)
- Kituo cha Kulea Watoto Yatima cha Karibu Nyumbani, Kibaha, Jimbo Katoliki la Dar es Salaam (Januari 2016)
- Kituo cha Kulea Watoto wenye Mtindio wa Ubongo cha Bethlehem Centre, Jimbo Katoliki la Ifakara (Aprili 2016)
- Kuchangia Ujenzi wa Kanisa la Kigango cha Katembo, Ikwiriri, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam (Februari 2017)
- Kuchangia Uchimbaji na Ujenzi wa Kisima cha Maji Safi kwenye Mahabusu ya Watoto Upanga Dar es Salaam (June 2017)
- Kutembelea na kufanya matendo ya huruma kwenye gereza la Mbozi Mbeya (June 2019)
NB: Mpaka sasa tumeweza kukusanya jumla ya mahitaji na michango ya zaidi ya sh 20m na kuiwakilisha sehemu husika.