Papa Francis atafanyiwa upasuaji wa tumbo lake Jumatano alasiri katika hospitali ya Gemelli ya Roma.

Anatarajiwa kukaa hospitalini kwa “siku kadhaa” ili kupata nafuu kutokana na upasuaji wa mishipa iliyovimba au ngiri, Vatican imesema.

Tatizo hilo “linasababisha maumivu makali sana ya mara kwa mara,” msemaji wa Vatican Matteo Bruni aliongeza.

Mzee huyo mwenye umri wa miaka 86 amekabiliwa na msururu wa matatizo ya afya katika miaka ya hivi karibuni, na anatumia fimbo na kiti cha magurudumu kutokana na maradhi ya goti yanayomkumba.

“Mapema alasiri atafanyiwa upasuaji … akiwa amedungwa sindano ya ganzi,” alisema Bw Bruni.

Aliongeza. “Atasalia katika kituo cha afya kwa siku kadhaa ili kuruhusu matibabu ya kawaida ya baada ya upasuaji na kupona kamili.”

Siku ya Jumanne, Papa alikuwa katika hospitali hiyo hiyo ya Roma kwa uchunguzi uliopangwa, miezi kadhaa baada ya kulazwa hospitalini kwa ugonjwa wa kupumua.

Alikaa siku tatu hospitalini mnamo mwezi Machi kutibu ugonjwa wa mapafu, katika mwezi huo huo na akaadhimisha kumbukumbu ya miaka 10 ya upapa wake.

Mnamo mwaka wa 2021, Papa Francis alikaa hospitalini kwa siku 10 baada ya kuondolewa sehemu ya matumbo yake, kwa nia ya kushughulikia tatizo alilokuwa nalo lililokuwa likimsababishia uchungu mwingi.

Mwezi uliopita, alijiondoa kutoka kwa umma siku ya Ijumaa kwa sababu ya homa.

Wakati mtangulizi wake Benedict XVI akiwa alijiuzulu mnamo 2013, Papa amepuuza uwezekano wa yeye kuondoka madarakani pia.

“Hauendeshi Kanisa kwa goti bali kwa kichwa,” anasemekana kumwambia msaidizi wake mwaka jana.

Papa anaendelea kudumisha ratiba yenye shughuli nyingi, na anatarajiwa kuzuru Ureno na Mongolia kuanzia Agosti.