Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky yuko Roma ambapo anakutana na viongozi wa kisiasa na amekutana na Papa Francis.

“Ziara muhimu kwa ushindi unaokaribia wa Ukraine!” Zelensky aliandika kwenye mtandao wake wa twitter alipotua katika mji mkuu wa Italia.

Atakutana pia na Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni, Rais Sergio Mattarella na kuelekea hadi Vatican baadaye Jumamosi.

Kumekuwa na usalama mkubwa, na zaidi ya polisi 1,000 wamepelekwa kwenye eneo lisilo na ndege huko Roma.

Papa Francis amewahi kusema kwamba Vatikani iko tayari kufanya kazi kama mpatanishi katika mzozo kati ya Urusi na Ukraine.

Mapema mwezi huu, alisema kwamba Vatikani ilikuwa ikifanya kazi katika mpango wa amani wa kumaliza vita, akisema kwamba mpango huo “haujaonekana hadharani. Utakapowekwa hadharani, nitauzungumzia.”