Baba Mtakatifu Francisko anaungana na Maaskofu pamoja na Mapadre wote wanaoadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya wito na zawadi ya Daraja Takatifu katika kipindi cha Mwaka 2023. Na taarifa kutoka Tanzania zinaonesha kwamba, Mheshimiwa Padre Octavian Linuma wa Jimbo Katoliki la Mahenge, tarehe 27 Julai 2023 anaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya zawadi na wito wa Upadre, Parokiani Kwiro, Jimbo Katoliki la Mahenge. Gambera kati ya mwaka 1980-1987.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kristo Yesu katika maisha na utume wake alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu na kusimika Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano. Akawachagua Mitume wake kumi na wawili ili kusaidia mchakato wa uinjilishaji, huku wakisaidiwa na wafuasi wengine 72 waliotumwa kwenda kumwandalia Kristo Yesu, mazingira ya uinjilishaji. Alhamisi Kuu, siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Kristo Yesu aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Daraja Takatifu, kielelezo cha huduma makini inayomwilishwa katika Injili ya upendo na huduma. Yesu aliwapatia Mitume wake jukumu la kuwa ni: Manabii ili wahubiri Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa; Makuhani ili waweze kuwatakatifuza Watu wa Mungu kwa sala, sadaka na ushuhuda wa maisha yao; na Wafalme kwa kuwaongoza watu wa Mungu. Kimsingi, Padre ni ufunguo wa malango ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Ikumbukwe kwamba, wito na maisha ya Upadre ni neema na zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kumwilishwa katika fadhila ya huruma na mapendo kwa Mungu na jirani. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 29 Machi 2023 ameungana na Maaskofu pamoja na Mapadre wote wanaoadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya wito na zawadi ya Daraja Takatifu katika kipindi cha Mwaka 2023. Na taarifa kutoka Tanzania zinaonesha kwamba, Mheshimiwa Padre Octavian Linuma wa Jimbo Katoliki la Mahenge, tarehe 27 Julai 2023 anaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya zawadi na wito wa Upadre, Parokiani Kwiro, Jimbo Katoliki la Mahenge. Padre Linuma aliwahi kuwa Gambera wa Seminari Ndogo ya Mtakatifu Petro Jimbo Katoliki la Morogoro kuanzia mwaka 1980 hadi mwaka 1987. Jubilei ni muda muafaka wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani. Itakumbukwa kwamba, katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 tangu Mtakatifu Yohane Maria Vianney alipofariki dunia, Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI akatangaza Maadhimisho ya Mwaka wa Mapadre Duniani uliozinduliwa tarehe 19 Juni 2009 na kuhitimishwa rasmi 19 Juni 2010. Huu ukawa ni muda wa kufanya tafakari ya kina kuhusu: Ukuu, Utakatifu, Wito na Maisha ya Kipadre ndani ya Kanisa sanjari na kukazia malezi na majiundo ya Kipadre.

Mapadre walikumbushwa kuwa, utambulisho na uhuru wa wafuasi wa Kristo Yesu ni mambo makuu mawili yanayowawezesha hata Mapadre katika maisha na utume wao, kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani. Kama binadamu wanatambua udhaifu na uwepo wa dhambi katika maisha yao, changamoto ya kutubu na kuongoka, ili kuanza hija ya utakatifu inayokita mizizi yake katika mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu. Mapadre wanapaswa kuwa ni wachungaji wema, kwa mfano wa utakatifu wa maisha yao, wawasaidie waamini walei kuiona njia ya hija ya utakatifu wa maisha, kwa kukazia umoja, maisha ya kisakramenti, kazi na utume wa mashirika na vyama mbali mbali vya kitume parokiani, bila kusahau, nidhamu na wajibu wa kila mwamini. Uaminifu wa Mapadre na walei uwawezeshe kuuona utakatifu, kwa njia ya maisha ya kisakramenti, liturujia na sala, kila upande ukijitahidi kutekeleza wajibu wake. Katika Maadhimisho ya Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney, Baba Mtakatifu Francisko akawaandikia Mapadre wote duniani, barua ya upendo na mshikamano wa kibaba, akiguswa na furaha ya huduma inayotolewa na Mapadre sehemu mbali mbali za dunia, kila kukicha! Hawa ni mapadre ambao wengine wamechoka na kudhohofu kwa afya mbaya na changamoto za maisha; kuna baadhi yao wametumbukia katika mateso na mahangaiko makubwa ya ndani kutokana na huduma yao kwa familia ya Mungu. Licha ya mambo yote hayo, Baba Mtakatifu anasema, Mapadre wanaendelea kuandika kurasa za maisha na utume wa Kipadre sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu katika barua hii anapenda kuwashukuru na kuwatia moyo Mapadre, wote wakitambua kwamba, wao kwa hakika ni marafiki wa Kristo Yesu katika maisha na utume wao. Baba Mtakatifu anasema, kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale, ameyaona mateso na mahangaiko ya watu wake, anasema haachi kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Mapadre, akiwakumbuka katika sala zake; anataka kuwafariji wote katika nyoyo zao, ili hatimaye, waweze kuimba ukuu na utukufu wa Mungu katika maisha yao.

KUHUSU MATESO: Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, katika miaka ya hivi karibuni mapadre wamekuwa wasikivu kwa kilio na mateso ya ndugu zao na wakati mwingine katika hali ya ukimya. Hawa ni watu waliokumbwa na nyanyaso za kijinsia zilizosababishwa na matumizi mabaya ya madaraka. Wahanga, familia pamoja na watu wote wa Mungu katika ujumla wao, wameteseka sana. Kanisa limedhamiria kujikita katika utamaduni wa shughuli za kichungaji kwa kukazia mfumo wa kukinga ili kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena katika maisha na utume wa Kanisa, changamoto kwa watu wote wa Mungu kuwajibika barabara. Baba Mtakatifu anakazia wongofu wa ndani, ukweli na uwazi sanjari na mshikamano kwa waathirika wa nyanyaso za kijinsia. Kwa njia hii, Kanisa litaweza kujenga utamaduni wa kuwa sikivu kwa shida na mahangaiko ya walimwengu. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, mateso haya yamewagusa hata Mapadre wenyewe, kiasi cha kuona kwamba, si mali kitu mbele ya watu wanaowahudumia kwa sadaka na majitoleo makubwa. Kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa imegusa na kutikisa maisha na utume wa Mapadre. Kwa hakika, mapadre wengi, wamesikitishwa na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa na wanaendelea kupandikiza mbegu ya matumaini mapya. Kuna madhara makubwa ambayo yametendwa na Mapadre katika nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Lakini, bado kuna maelfu ya mapadre wanaoendelea kutekeleza dhamana na wito wao kwa ukarimu na uaminifu mkubwa. Ni watu ambao wamekuwa ni vyombo na mashuhuda wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baadhi yao wanafanya utume katika mazingira magumu na hatarishi sana. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime kwa ushuhuda wao katika nyakazi hizi za mateso na magumu yanayoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Mapadre. Mapadre waendelee kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo sehemu mbali mbali za dunia. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, kipindi hiki cha utakaso katika maisha na utume wa Kanisa, kitawawezesha Mapadre kuwa wanyenyekevu na watu wenye furaha, kwa kutarajia kuyakumbatia ya mbeleni kwa matumaini makubwa. Kipindi hiki cha mateso, kisiwakatishe tamaa, bali iwe ni fursa ya kushikamana na kuambatana na Kristo Yesu, kwani bila yeye ni Mapadre si mali kitu. Kristo anapenda kuwaokoa kutoka katika unafiki na tabia ya kutaka kujikweza, ili kuonekana mbele ya watu, lakini Yesu anataka kuwarudishia ule uzuri na utakatifu wa maisha na utume wa Kipadre. Toba na wongofu wa ndani unaosimikwa katika unyenyekevu na machozi ya uchungu, yapate kibali cha ukuu wa Mungu unaofumbatwa katika msamaha, mwanzo wa hija ya utakatifu wa maisha.
Papa Francisko: Mapadre Msijikatie tamaa ya maisha!