Ni katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Yosefu, tarehe 19 Machi 2013, Baba Mtakatifu Francisko aliposimikwa rasmi kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 266 kwa kuchagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi. Vipaumbele vyake tangu wakati huo ni: Maskini, Amani, Mazingira na sasa ni Udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika diplomasia ya huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake wote sanjari na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa tarehe 19 Machi 2023 anaadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Yosefu, mtu wa haki, Mume wake Bikira Maria na Baba Mlishi wa Mtoto Yesu, aliyezaliwa kwa kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Mtakatifu Yosefu akamwita jina lake Yesu, maana Yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao na kutambuliwa kisheria kuwa ni Mwana wa Ukoo wa Daudi, Mwana wa Ibrahimu, Baba wa imani. Mtakatifu Yosefu aliteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni mlinzi mwaminifu wa Nyumba ya Mungu, kama ilivyokuwa kwa Ibrahimu sanjari na kukubali kupokea mpango wa Mungu katika maisha yake, kama alivyoambiwa na Malaika wakati akiwa usingizini. Akamchukua Bikira Maria kama mchumba wake. Katika hali ya hatari, alimchukua Mtoto na Mama yake Bikira Maria, wakakimbilia Misri na kukaa huko hata alipofariki Herode, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa Nabii akisema, “Kutoka Misri nalimwita mwanangu”. Rej. Mt 1: 1-25; 2: 1-23. Ni katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2013, Baba Mtakatifu Francisko aliposimikwa rasmi kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 266 kwa kuchagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi. Vipaumbele vyake tangu wakati huo ni: Maskini, Amani, Mazingira na sasa ni Udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika diplomasia ya huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake wote sanjari na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni amana na utajiri wa Kanisa; wao ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu.

Kumbukizi ya Miaka 10 tangu Papa Francisko aanze utume wake.

Hawa ni maskini wa hali na mali; wanaotumbukizwa katika biashara ya binadamu na viungo vyake; wanaodhalilishwa na kunyanyaswa utu, heshima na haki zao msingi kama watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hawa pia ni wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa. Ni katika maadhimisho ya kumbukizi ya miaka kumi tangu Baba Mtakatifu Francisko achaguliwe na kuanza kuliongoza rasmi Kanisa Katoliki, Rais Sergio Mattarella wa Italia kwa niaba yake mwenyewe na watu wa Mungu nchini Italia, amemwandikia Baba Mtakatifu Francisko ujumbe wa matashi mema, sanjari na kumshukuru kwa kutumia vyema Mamlaka matakatifu ya ufundishaji katika Kanisa “Magisterium” kwa ajili ya huduma kwa Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake, ili kukuza na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rais Sergio Mattarella anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu na kuendelea kukazia haki na wajibu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na kuendelea kukuza ari na mwamko wa ushirikiano na mafungamano ya Kimataifa. Rais Sergio ana mpongeza Baba Mtakatifu kwa Waraka wake wa Kitume “Fratelli tutti”: Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” uliozinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020, kwa kugusia kuhusu: Magonjwa jamii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Msamaria mwema anawekwa mbele ya walimwengu kama ni mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini.

Ujenzi wa udugu wa kibinadamu

Baba Mtakatifu anakazia maisha ya kiroho, mshikamano wa kidugu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, utawala bora, ushirikiano na mshikamano katika kukabiliana na changamoto mamboleo kwamba ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee.  Baba Mtakatifu anajikita kwenye siasa safi kwa ajili ya huduma kwa jamii, maendeleo, ustawi na mafao ya wengi; utu, haki msingi za binadamu na umuhimu wa kufanya mageuzi makubwa kwenye Umoja wa Mataifa ili kweli uweze kuwa ni kielelezo cha “familia ya Mataifa.” Watu wa Mungu hawana budi kujikita zaidi katika mchakato wa majadiliano na urafiki ili kujenga sanaa ya watu kukutana. Baba Mtakatifu anapembua kuhusu makutano yaliyopyaishwa ili kujenga misingi ya haki na amani; msamaha kwa kuondokana na “dhana ya vita ya haki na halali” ambayo kwa sasa imepitwa na wakati kama ilivyo pia kwa adhabu ya kifo kwani inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu, utakatifu na zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote utamaduni wa kifo! Dini na udugu wa kibinadamu ni chanda na pete; hapa mkazo ni umuhimu wa dini kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu na kwamba, Kanisa litaendelea kujizatiti katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa kuzingatia kanuni msingi za Kiinjili.

Maskini wana upendeleo wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa

Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya vinasaba vya maisha ya mwanadamu. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” umegawanyika katika sura kuu sita: Mambo yanayoendelea kujiri katika mazingira; Injili ya Kazi ya Uumbaji na Amani Duniani; Vyanzo vya mgogoro wa Ikolojia na jinsi vinavyohusiana na watu; Ikolojia ya mazingira, uchumi na jamii. Njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni kuhusu umuhimu wa elimu ya ikolojia inayojikita katika wongofu wa ndani, furaha na amani, Sakramenti za Kanisa pamoja na sala. Waraka huu una mwelekeo wa umoja na mshikamano ambao unadhihirishwa na mchango uliotolewa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko anaonekana kufuata nyayo za Mtakatifu Francisko wa Assisi, kwa kuimba utenzi wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na dunia na kwa kukazia umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki, kwani uharibifu wa mazingira unalinganishwa na umaskini; anaihimiza jamii pamoja na kuendelea kutunza furaha, amani na utulivu wa ndani; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete na kamwe hayawezi kutenganishwa.

Utunzanji bora wa mazingira nyumba ya wote
Utunzanji bora wa mazingira nyumba ya wote

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka huu, anapembua kwa kina na mapana jinsi ambavyo uharibifu wa mazingira unavyohitaji kujikita katika wongofu wa kiikolojia; kwa kuwa na mageuzi makubwa katika maisha, ili kweli mwanadamu aweze kuwajibika katika utunzaji wa nyumba ya wote. Hii ni dhamana ya kijamii inayopania pia kung’oa umaskini, kwa kuwajali maskini pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya dunia inatumika sawa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rais Sergio Mattarella wa Italia anakaza kusema kwamba, Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, yataendelea kuwa ni nguzo msingi na rejea kwa Serikali, Jumuiya ya Kimataifa, Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa, kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Anamshukuru Baba Mtakatifu kwa utume wake kwa watu wa Mungu nchini Italia pamoja na kuendelea kuwajengea matumaini; kwa kuwaimarisha katika maisha na utume wao kwa njia hija na shughuli mbalimbali za kichungaji katika sehemu mbalimbali za Italia. Rais Sergio anamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko na hatimaye, anamtakia heri, baraka na mafanio mema katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.