Omba neema ya Mungukwa njia ya sala; kwa sababu msamaha ni tendo la kiroho na wala si rahisi kibinadamu.
Kataa kuongozwa na hasira: “Kama mkikasirika, msikubali hasira yenu iwafanye mtende dhambi, na wala msikae na hasira kutwa nzima. Msimpe ibilisi nafasi.” (Efe. 4:26-27)
Tafuta mtu mwenye busara anayeweza kuwa mshauri wako; hasa katika nyakati ngumu zenye ugumu wa kuachilia maumivu. Unaweza ukawaona viongozi wa Dini.
Jenga utamaduni wa kujishusha, uwe mnyenyekevu.“Enyi ndugu, maandiko ya Mungu yatugutia yakisema “ Kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa” (Kanuni ya Mt. Benedikto 7:1)
Usiweke makwazo moyoni mwako, yakija yapokee kama kitu cha kawaida wala usihangaike (don’t panic).
Tambua kuwa kutosamehe kuna madhara; kama vile msongo wa mawazo, vidonda vya tumbo, kupanuka moyo, n.k.
Tamadunisha maisha ya upendo; kwani palipo na upendo Mungu yupo. “Mwenyeupendo haweki kumbukumbu ya mabaya, hafurahii uovu, bali, hufurahia ukweli. Mwenye upendo huvumilia yote, huamini yote, na hustahimili yote. Upendo hauna kikomo kamwe.” (1 Kor. 13:5-8)
Tambua ya kuwa usiposamehe nawe hutasamehewa, na wala sala zako hazitajibiwa. “Utusamehe makosa yetu kama nasi tunavyowasamehe waliotukosea. … Maana mkiwasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe nuinyi pia. Lakini msipowasamehe watu makosa yao, naye Baba hatawasamehe ninyi makosa yenu”
(Matayo 6:12, 14-15).
Utambulisho waUPENDO ni MSAMAHA.
Tumia msaada wa Neno la Mungu (Biblia); Mtume Paulo anasema; “Ujumbe wa Kristo ukae ndani yenu pamoja na utajiri wake wote. Fundishaneni na kushauriana kwa hekima yote. Imbeni zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Mungu mioyoni mwenu kwa shukrani. Na kila mfanyacho kwa neno au tendo, fanyeni vyote kwa jina la Bwana Yesu na kumshukuru Mungu Baba kwa njia yake.” (Wakolosai 3:16-17)
Uwe mvumilivu; kukosekana kwa uvumilivu huzua ugomvi, uadui, chuki, kusengenyana. Hii ni hatari katika maisha ya kiroho.