Wajitahidi kujichotea nguvu katika sala, kwa ajili ya huduma kwa maskini na watu ambao wamejeruhiwa na wanabeba mwilini mwao madonda makubwa.. Wanachama wa upendo wamekuwa ni kielelezo cha Msamaria Mwema. Papa anasema, huruma ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele, inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Kitume la Mtakatifu Petro: “Circolo S. Pietro” kwa zaidi ya miaka 150, limekuwa likijisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wahitaji zaidi wa mji wa Roma, kwa njia ya sala, sadaka na matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ndiyo kauli mbiu inayonogesha Injili ya huduma ya upendo inayotekelezwa kila kukicha, kwa ari, upendo na moyo mkuu. Utume huu ulianzishwa rasmi na Mwenyeheri Papa Pio IX kunako mwaka 1869 na kunako mwaka 2019, wameadhimisha Kumbukizi ya Miaka 150 tangu kuanzishwa kwake. Utume huu wa Injili ya Msamaria mwema, ukawekwa mikononi mwa vijana wa kizazi kipya, ili kuhakikisha kwamba, maskini na wahitaji zaidi wa mji wa Roma walau wanapata mahitaji yao msingi ya: chakula, malazi na huduma bora ya afya. Lengo ni kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za maskini, kwa kuwaonesha huruma na upendo kama ilivyokuwa katika Injili ya Msamaria Mwema. Utume huu kwa ufupi kabisa unaratibiwa kwa: “Sala, Matendo, na Sadaka.”
Huduma kwa familia zinazokabiliana na ugumu wa maisha
Huduma kwa familia zinazokabiliana na ugumu wa maisha

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 20 Februari 2023 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Shirika la Kitume la Mtakatifu Petro: “Circolo S. Pietro” na kuwataka kuzamisha utume wao katika: Imani inayomwilishwa katika huduma ya upendo, kama kielelezo cha imani tendaji. Wajitahidi kujichotea nguvu katika sala, kwa ajili ya huduma kwa maskini na watu ambao wamejeruhiwa na wanabeba mwilini mwao madonda makubwa na wanachama hawa katika huduma ya upendo wamekuwa ni kielelezo cha Msamaria Mwema. Baba Mtakatifu anasema, huruma ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele, inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha, chemchemi ya furaha na matumaini mapya, yanayovunjilia mbali ubaguzi, ubinafsi na uchoyo ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni. Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya mang’amuzi ya huruma inayowakirimia furaha, hata kama maisha yao bado yanasheheni matatizo na changamoto mbalimbali, ili kuondokana na utamaduni wa huzuni, utupu na upweke unaopelekea msongo wa mawazo kwa watu wengi!
Injili ya upendo: Sala, Sadaka na Matendo ya huruma
Injili ya upendo: Sala, Sadaka na Matendo ya huruma

Kanisa linaweka mbele ya macho ya waamini Mfano wa Msamaria mwema, maarufu kama Injili ya Msamaria mwema, ili kuwaganga kwa mafuta ya faraja wale waliovunjika na kupondeka moyo; kwa kuwanyweshwa divai ya matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kristo Yesu ni kielelezo ufunuo wa Uso wa huruma na upendo wa Baba wa milele, aliyemimina maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, akawakirimia waja wake huruma na msamaha! Hii ni changamoto kwa waamini kupenda kama Kristo Yesu alivyowapenda. Wanachama hawa watekeleze dhamana na wajibu wao kwa ukimya, hali ya unyenyekevu na moyo wa sala, kwani daima Kristo Yesu yuko kati pamoja nao katika huduma ya upendo na hii ndiyo siri ya maisha ya Kikristo. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko kwa mara nyingine tena, ametoa shukrani zake za dhati kwa huduma ya upendo wanayoitekeleza kwa ajili ya maskini na wahitaji zaidi wa mji wa Roma. Bikira Maria Afya ya Warumi, “Salus Populi Romani” awakinge na kuwalinda katika hatari zote za roho na za mwili.