Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko ameupongeza Mfuko huu kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha Miaka 75 iliyopita na kwamba, ni filamu inatoa fursa kwa watazamaji kuangalia na kutafakari uzuri wa kazi ya uumbaji, inayofanywa na wasanii wenyewe, kielelezo cha sauti ya Mungu, ikimtaka msanii kufunguka! Efatha! Rej Mk7: 34. Utu na Heshima!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mfuko wa Filamu Italia, “Fondazione Ente dello Spettacolo” ulianzishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki wa Italia, CEI kunako mwaka wa 1947. Lengo ni kukuza na kusambaza utamaduni wa filamu nchini Italia. Hadithi katika maneno zikiambatana na picha zinabeba uzito zaidi katika mawasiliano, mafungamano na mahusiano ya jamii katika ulimwengu mamboleo. Mfuko wa Filamu Italia unachangia kwa kiasi kikubwa dhana ya upembuzi yakinifu, ili kutoa nafasi kwa watazamaji kuweza kukosoa; kutoa mafunzo, upangaji, uratibu na mpangilio wa hafla, warsha, hakiki na sherehe. Mfuko huu unasimamia sekta ya Filamu nchini Italia na hivyo kutoa fursa kwa wale wanaotaka kushiriki kikamilifu katika ulimwengu wa filamu fursa za masomo ya kitamaduni, ukuaji wa mtu binafsi, maendeleo pamoja na biashara.
Papa ameupongeza Mfuko wa Filamu Italia kwa mchango wake
Papa ameupongeza Mfuko wa Filamu Italia kwa mchango wake

Mfuko wa Filamu Italia, “Fondazione Ente dello Spettacolo” kwa mwaka 2023 unaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 75 tangu kuanzishwa kwake, ili kutoa nafasi kwa Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” kuchangia katika ustawi na maendeleo ya vyombo vya mawasiliano ya jamii kama ilivyokuwa kwa Papa Pio XI aliyehimiza kuanzishwa kwa Mfuko huu, ili kuhakikisha kwamba, filamu zinazotengezwa na kuoneshwa hadharani zinazingatia kanuni maadili na utu wema na hivyo kutoa nafasi kwa watu wote wa Mungu kuweza kuangalia pasi na vizuizi kwa familia, makleri na watawa kuziangalia. Kumekuwepo na maendeleo makubwa katika kipindi cha miaka 75, kilichoziwezesha Parokia kuanzisha kumbi za kuangalia filamu kama jumuiya pamoja na ujenzi wa vituo vya michezo kwa watoto na vijana maarufu kama “Oratori.”
Mfuko umesaidia ujenzi wa vituo vya michezo parokiani