Takriban watu 200,000 walitoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Papa Benedict XVI wakati wa kulazwa kwa mwili wake kwa siku tatu zilizopita, Vatican inasema.

Mwili wake sasa umefungiwa kwenye jeneza kabla ya mazishi yake siku ya Alhamisi.

Papa Francis ataongoza mazishi hayo – ikiwa ni mara ya kwanza kwa Papa aliyepo kuongoza mazishi ya mtangulizi wake katika zaidi ya miaka 220, Vatican inasema .

Papa huyo wa zamani alifariki usiku wa kuamkia mwaka mpya akiwa na umri wa miaka 95 , karibu muongo mmoja baada kujiuzulu kwa sababu ya afya mbaya.

Makumi ya maelfu ya watu wanatarajiwa kuhudhuria mazishi hayo katika Medani ya St Peter’s, mbele ya Basilica ya St Peter, saa 9:30 kwa saa za huko (8:30 GMT).

Tukio hilo halitakuwa na mambo mengi kulingana na kile Benedict alichotaka Vatican inasema.

Kwa sababu Benedict hakuwa tena mkuu wa nchi alipofariki, ni wajumbe rasmi tu kutoka Italia na Ujerumani asili ya Benedict ndio watakaohudhuria.

Viongozi wengine watakuwepo lakini sio katika nafasi zao rasmi – ikiwa ni pamoja na Mfalme Philippe wa Ubelgiji na Malkia Letizia wa Uhispania, pamoja na viongozi wa Poland na Hungary, shirika la habari la Kikatoliki linaripoti.

Papa Mstaafu atazikwa katika makaburi chini ya Basilica baada ya mazishi yake, kulingana na matakwa yake ya mwisho.

Kabla ya kuwekwa kwenye kaburi, mwili wake utafungwa kwenye jeneza la zinki, ambalo litawekwa kwenye jingine la mbao. Vitu vinavyoashiria wakati wake katika upapa pia vitawekwa kando ya mwili wake.