Papa Francis amelaani “njaa ya mali na madaraka” ya wanadamu katika Misa ya mkesha wa Krismasi huko Vatican, akionekana kurejelea vita vya Ukraine na migogoro mingine.”Tumeona vita ngapi!” alisema, akiongeza kuwa wahathiriwa wakubwa ni “wanyonge na maskini”.

Kiongozi huyo wa Katoliki alikuwa akiwahutubia waumini katika Kanisa la St Peter’s katika Jiji la Vatican.

Papa Francis, 86, aliingia kanisani kwa kiti cha magurudumu, na kuketi kwenye eneo la madhabahu kwa sehemu kubwa ya Misa Jumamosi jioni.

“Wakati wanyama wanakula katika mabanda yao, (binadamu) wanaume na wanawake katika dunia yetu, kwa njaa yao ya mali na madaraka, hula hata majirani zao, mama zao na dada zao,” alisema.

Hakuitaja moja kwa moja vita vya Urusi-Ukraine wakati wa huduma yake hiyo.

Wakati wa hatua za mwanzo za uvamizi wa Urusinchini Ukraini uliozinduliwa tarehe 24 Februari, Papa alikosolewa sana nchini Ukraine kwa kutoa maoni ambayo wananchi wengi wa Ukraine waliyaona kuwa ya tahadhari, bila kuilaumu Urusi moja kwa moja.