Katika fursa ya Siku ya Kimataifa ya watu wenye ulemavu,Papa ametoa ujumbe wake kwa kubainisha kwamba:“Injili nzima imetolewa kwa kila mtu bila kujali sifa na bila ubaguzi kwa pamoja nayo kuna hitaji ka furaha ya kuitangaza na mafundisho ya udhaifu ni karama ya kulitajirisha Kanisa ili kubomoa sintofahamu na ubaguzi.
Na Angella Rwezaula; – Vatican.
Katika ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko uliochapishwa tarehe 3 Desemba 2022 katika Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu, umejikita na mada ya Mafundisho ya udhaifu na kwamba ni karama. Katika ujumbe huo, Papa ameandika kwamba “Nyinyi akina dada na kaka wenye ulemavu mnaweza kulitajirisha Kanisa: uwepo wenu unaweza kusaidia kubadilisha hali halisi tunamoishi, na kulifanya kuwa la kibinadamu zaidi na la kukaribisha zaidi. Bila udhaifu, bila mipaka, bila vikwazo vya kushinda, usingekuwa ubinadamu wa kweli. Na hii ndiyo sababu ninafurahi kwamba mchakato wa safari ya sinodi unadhihirisha kuwa ni tukio la kupendeza ambalo hatimaye ni kusikia sauti yenu pia na kwamba mwangwi wa ushiriki huu umefikia hati ya maandalizi kwa ajili ya hatua ya kibara ya Sinodi.”
Kila mtu anapewa Injili
Kila mtu anapewa Injili kwa ukamilifu wake na, pamoja nayo, kuna kazi ya furaha ya kuitangaza. Sisi sote tumeitwa kutoa kwa wengine ushuhuda wa upendo wa wokovu wa Bwana, ambaye zaidi ya kutokamilika kwetu hutupatia ukaribu wake, Neno lake, nguvu zake, na kutoa maana kwa maisha yetu( rej. Evangelii gaudium). Kuwasilisha Injili si kazi iliyowekwa kwa ajili ya watu fulani tu, bali inakuwa hitaji la lazima kwa mtu yeyote ambaye amepata uzoefu na urafiki na Yesu. Kumtumiani Bwana, uzoefu wa huruma yake, faraja ya ushirika wake si mapendeleo pekee kwa wachache, wala haki ya wale ambao wamepata mafunzo makini na ya muda mrefu. Kinyume chake, huruma yake inaruhusu kujulikana na kukutana kwa namna ya pekee sana na wale wasiojiamini na wanaona haja ya kujiachia kwa Bwana na kushiriki pamoja na ndugu zake.
Mafundisho kuhusu udhaifu
Katika waraka huo, Baba Mtakatifu Francisko amekazia hasa dhana ya Mafundisho ya udhaifu kwamba kama yangesikilizwa, ingefanya jamii zetu kuwa za kibinadamu na za kidugu, na hivyo kupelekea kila mmoja wetu kuelewa kwamba furaha ni mkate usioweza kuliwa peke yake. Lakini baadaye anaongeza kuandika kwamba Je, ni kiasi gani mwamko wa kuhitajiana ungetusaidia kuwa na mahusiano zaidi kwa kuepuka uadui na wale wanaotuzunguka! Na ni kiasi gani uchunguzi unabainisha kwamba hata watu hawawezi kujiokoa wenyewe ungeweza kutusukuma kutafuta suluhisho la migogoro isiyo na maana tunayoishi. Wazo la Papa kwa maana hiyo linalenga matukio ya sasa ambapo anaandika kuwa: “leo hii tunataka kukumbuka mateso ya wanawake wote na wanaume wote wenye ulemavu wanaoishi katika hali ya vita, au ya wale wanaojikuta walemavu kutokana na mapigano.” Maneno ya Papa yanaambatana na swali: Ni watu wangapi huko Ukraine na katika vita nyingine wanabaki gerezani mahali ambapo kuna mapigano na hawana hata uwezekano wa kutoroka? Ni muhimu kuwapa kipaumbele maalum na kuwezesha kwa kila njia upatikanaji wao wa misaada ya kibinadamu”.
Yesu pekee ndiye kiini chetu kama ilivyo ukarimu kwa walemavu
Katika ujumbe huo, Baba Mtakatifu Francisko pia anakumbuka kwamba kwa pamoja tunaweza kubomoa kuta za sintofahamu na ubaguzi. Zaidi ya yote, Sinodi, pamoja na mwaliko wake wa kutembea pamoja na kusikiliza kila mmoja wetu, inatusaidia kuelewa jinsi katika Kanisa, hata kuhusu suala ulemavu kuwa hakuna suala la sisi na wao, bali sisi ni wamoja, pamoja na Yesu. Kiini cha Kristo, mahali ambapo kila mtu huleta karama na mapungufu yake. Ufahamu huo, unaozingatia ukweli kwamba sisi sote ni sehemu ya ubinadamu sawa walio katika mazingira magumu unaochukuliwa na kutakaswa na Kristo, huondoa tofauti yoyote ya kiholela na kufungua mlango wa ushiriki wa kila mtu aliyebatizwa katika maisha ya Kanisa. Hatimaye, Baba Mtakatifu Fransisko ametoa matashi yake kwamba mahali ambapo Sinodi ilijumuisha watu wote, ilifanya iwezekane kuondoa ubaguzi uliokita mizizi. Kwa hakika, ni kukutana na udugu ambao wanabomoa kuta za sintofahamu na kushinda ubaguzi; kwa sababu hiyo ni matumaini kwamba kila jumuiya ya Kikristo inakuwa wazi kwa uwepo wa dada na kaka wenye ulemavu, daima ili kuhakikisha kuwa wanakaribishwa na kujumuishwa kikamilifu.