Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI amefariki dunia Jumamosi tarehe 31 Desemba 2022 akiwa na umri wa miaka 95 ya kuzaliwa, kwenye Monasteri ya Mater Ecclesiae iliyoko kwenye Bustani za Vatican, tangu alipong’atuka kutoka madarakani kunako mwaka 2013. Wakati wote huo, ameendelea kulitegemeza Kanisa kwa sala na tafakari zake, akionesha unyenyekevu mkubwa!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI amefariki dunia Jumamosi saa 3: 34 Asubuhi tarehe 31 Desemba 2022 akiwa na umri wa miaka 95, katika makazi yake kwenye Hosteli ya Mater Ecclesiae iliyoko kwenye Bustani za Vatican tangu mwaka 2013 alipong’atuka kutoka madarakani kutokana na sababu za umri kuwa mkubwa. Alifanya maamuzi haya magumu, ili kutoa nafasi kwa kiongozi mwingine, aweze kulitumikia Kanisa la Kristo Yesu, kwa ari na moyo mkuu. Kwa uchungu na majonzi makuu, lakini tukiwa na tumaini la maisha ya uzima wa milele, tunawaalika kuungana na Mama Kanisa kwa ajili ya kumwombea maisha ya uzima wa milele Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Baada ya muda si mrefu, tutaweza kuwajuza mengi zaidi kuhusiana na msiba huu mkubwa kwa sasa.