Maskini wengi wamefurahishwa sana kwa ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko kwa chakula cha mchana, alama ya mshikamano wa udugu na upendo. Kwa maskini wengi, hii ilikuwa ni siku tofauti kabisa na siku nyingine za Mwaka katika maisha yao; siku ambayo wamepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na watu mbalimbali, ushuhuda wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Sita ya Maskini Duniani tarehe 13 Novemba 2022 yamenogeshwa na kauli mbiu: “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.” 2Kor 8:9. Siku ya Maskini Duniani ni fursa ya kushikamana kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana, kama alama ya: urafiki, umoja na udugu wa kibinadamu unaovunjilia mbali kuta za utengano na tabia ya maamuzi mbele. Maadhimisho haya yanakamilishwa kwa namna ya pekee, Mama Kanisa anapoadhimisha Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu. Huu ni ufalme wa kweli na wa uzima; ufalme wa utakatifu na wa neema; ufalme wa haki, mapendo na amani. Ufalme wa Kristo Yesu unafumbatwa kwa namna ya pekee katika Fumbo la Msalaba, ushuhuda wa utimilifu wa upendo wa Mungu na chemchem ya maisha mapya wakati wa Pasaka. Siku ya Maskini Duniani iwe ni nafasi ya kuwaonjesha huruma na upendo maskini na wahitaji; ni siku ya kuwakaribisha na kuwakirimia wageni; Siku inayowasaidia waamini kumwilisha imani yao katika matendo; watu wawe tayari kupokea msaada na kujitahidi kuishi kwa kuzingatia mambo msingi ya maisha, tayari kujiachilia kwa huruma ya Mungu.