BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limemuahidi ushirikiano Rais Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza majukumu ya kuliongoza Taifa.

Hayo yameelezwa jana Ijumaa Machi 26, 2021 na makamu mwenyekiti wa baraza hilo, Askofu Flavian Kassala wakati akitoa salamu za pole kwa Rais Samia kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tano hayati John Magufuli.

Alieleza hayo katika ibada ya mazishi ya kiongozi huyo jana wilayani Chato Mkoa wa Geita, akisisitiza kuwa kanisa litakuwa bega kwa bega na Rais Samia kuhakikisha anafikia malengo yake ya kuiletea maendeleo Tanzania.

Askofu Kassala alisema Tanzania imeondokewa na mtu mwaminifu, mzalendo, mchapakazi na mtetezi wa wanyonge akisisitiza kuwa TEC itaendelea kumuenzi kutokana na jitihada na mikakati yake ya kujenga uchumi.

Alisema kauli mbiu ya Magufuli ya Hapa Kazi Tu itabaki kuwa mwanga katika akili na mioyo ya wananchi kuelekea utekelezaji wa safari aliyotamani tufike.

“TEC inatambua uthabiti aliokuwa nao katika imani yake kwa Mungu. Amekuwa akimtegemea Mungu siku zote za maisha yake na ametukumbusha maisha hapa duniani ni mafupi. Ni imani yetu kuwa Mungu mwenye huruma atampokea mbinguni,” alisema