Kwa adhimisho la dominika hii ya Matawi tunaingia katika Juma Kuu ambamo ndani yake tunaadhimisha mafumbo makuu ya ukombozi wetu. Mfungo wetu wa Kwaresima, bidii ya kuishi katika maisha ya fadhila na matendo mema kwa njia ya sala, toba na wongofu vilikuwa pia na lengo la kutandaa kushiriki kikamilifu maadhimisho haya makuu yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo!

Na Padre William Bahitwa, – Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Jumapili hii tunaadhimisha Dominika ya Matawi, Dominika ambayo inaunganisha pamoja maadhimisho makuu mawili. Adhimisho la kwanza likiwa ni lile la Yesu kuingia kwa shangwe mjini Yerusalemu na la pili likiwa ni adhimisho la Mateso yake. Ufafanuzi wa Masomo ya Misa kwa ufupi: Liturujia ya dominika ya Matawi inatoa nafasi kusoma masomo manne. Lipo somo la Injili linalosomwa kabla ya Misa katika ibada ya kubariki Matawi, halafu yapo yale masomo matatu ya kawaida katika Misa ya dominika. Masomo yote haya manne yanaakisi matukio yale makuu mawili ambayo Kanisa linayaadhimisha katika dominika hii, yaani adhimisho la Yesu kuingia Yerusalemu na lile la Yesu huyo huyo kuingia katika Mateso yake. Injili inayosomwa wakati wa Ibada ya kubariki Matawi, kwa mwaka huu B wa Kanisa, inatoka kwa Mwinjili Marko (11:1-11). Inaelezea namna tukio lenyewe la Yesu kuingia Yerusalemu lilivyokuwa.

Awali ya yote, ni vizuri tukajikumbusha kuwa Yesu aliingia Yerusalemu katika kipindi ambacho sherehe ya Pasaka ya Wayahudi ilikuwa inakaribia. Hii ilikuwa ni sherehe ambayo Wayahudi waliiadhimsha kila mwaka kukumbuka namna walivyokombolewa kutoka utumwani Misri. Ilikuwa ni sherehe ambayo kila myahudi alilazimika kwenda Yerusalemu kuhiji. Yeye lakini, hija aliyokuwa anaifanya ni tofauti. Alikuwa anakwenda Yerusalemu kukamilisha kile ambacho kilimleta duniani. Alikuwa anakwenda kuutoa uhai wake kwa ajili ya kuwakomboa watu wake na kwa ajili ya kuukomboa ulimwengu mzima. Katika somo hili tunaona namna Yesu alivyojiandaa kuingia Yerusalemu. Aliwaelekeza wanafunzi wake namna watakavyompata mwanapunda atakayetumia na wao wanampata vivyo hivyo alivyowaelekeza. 

Tunaona pia namna watu walivyompokea. Walishangilia mno. Walitandika mavazi juu ya mwanapunda huyo na njiani, wakashika matawi mikononi wakiimba “hosana, hosana, ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana, umebarikiwa ufalme wa baba yetu Daudi, hosana juu mbinguni”. Namna tukio hili lilivotokea, lilibeba pia alama nyingi na nzito. Kwa upande mmoja alama hizi zilimuonesha Yesu kuwa ni mfalme au mtawala aliyekuwa anatazamiwa na kwa upande mwingine zilimwonesha kama ni masiya au mkombozi. Kwa upande mmoja zilimpandisha Yesu na kumkuza juu kabisa na kwa upande mwingine zilionesha unyenyekevu au udogo aaliokuwa nao. Kitendo cha Yesu kupanda mnyama wa safari ambaye alikuwa hajatumiwa na mtu yeyote kilikuwa ni cha kifalme lakini hapo hapo kumchagua mwanapunda badala ya farasi kama mnyama wa safari kilionesha unyenyekevu mkubwa.

Tukiangalia pia sifa alizopewa na watu: walimwita Mwana wa Daudi, walitandika mavazi yao chini na walipaza sauti hosana hosana, maana yake tuokoe, tuokoe: hizi zote ziliashiria kuwa walimtambua kama mfalme aliyekuwa anakuja kuwakomboa kutoka ukoloni wa kisiasa waliokuwamo chini ya dola ya kirumi. Lakini yeye hajibu kwa kutoa hotuba ya ukombozi kama walivyofanya watawala wa aina hiyo. Yeye anakwenda moja kwa moja hekaluni. Kumbe tangu mwanzo kabisa Yesu anawaonesha watu yeye ni mfalme lakini si kama wafalme wa dunia hii, yeye ni masiya, ni mkombozi lakini haendi kuwakomboa kwa njia nyingine yeyote ile ya isipokuwa kwa njia ya unyenyekevu na ya utii kwa mapenzi ya Mungu. Hiyo ndiyo nguvu pekee inayoweza kukomboa. Masomo tunayokuja kukutana nayo sasa kwenye Misa yanazidi kutoa mkazo wa njia hiyo anayoitumia Yesu kuleta ukombozi; njia ya unyenyekevu na utii kwa mapenzi ya Mungu.

Somo la kwanza, ambalo linatoka katika Kitabu cha Nabii Isaya (50:4-7), linaonesha kuwa ilikwishatabiriwa tangu enzi ya Nabii Isaya kuwa masiya atalikomboa taifa kwa njia ya mateso. Nabii Isaya alitoa utabiri huu kupitia tenzi zinazojulikana kama tenzi za mtumishi wa Bwana. Hapa ni utenzi wa tatu unaomwonesha mtumishi asiye mkaidi, mtumishi anayeyakabili mateso, mtumishi asiyerudisha ubaya wanaomfanyia kwa ubaya. Ni mtumishi anayejua kuwa Mungu hajamwacha kuwa kuwa anayatimiza mapenzi yake. Somo la pili kutoka Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi (2, 6-11) linaeleza wazi wazi kuwa utume mzima wa Yesu haukuwa mwingine isipokuwa ule wa unyenyekevu na utii. Hakuna sehemu nyingine katika Biblia inayoelezea sifa hii ya Yesu kama linavyofanya somo hili la leo. Tunaona kuwa Yesu hapo mwanzo alikuwa namna ya Mungu, alikuwa ni Mungu. Akauachilia mbali ule utukufu wake wa kimungu, akajishusha akatwaa mwili wa binadamu, yaani akazaliwa mwanadamu.

Hakubakia hapo tu bali alienda chini zaidi, zaidi ya hata pale ambapo mwanadamu alishindwa kufika: kutii mpaka kufa kifo cha msalaba. Sasa kilichotokea ni kwamba kwa unyenyekevu na utii huo usio na mfano, Mungu amemkuza mno. Akampa jina linalopita kila jina. Jina linalopita kila jina ni Jina la Mungu. Maana yake ni kwamba huyo ambaye alionekana si masiya kadiri ya mategemeo ya watu, huyo ambaye walimuua kwa kusema amejifanya Mungu, sasa Mungu Baba mwenyewe amemtambulisha kuwa Mungu kwa kumpa hilo Jina. Na kwa sababu ni Mungu, sasa kila goti linapigwa, yaani sasa ataabudiwa; na kila ulimi utakiri, yaani atakuwa ni chanzo cha imani kwa watu wote; kwa utukufu wa Mungu Baba, yaani kwa namna ile ile ambayo Mungu Baba anaabudiwa, kama alivyo chanzo cha imani na kama anavyopewa utukufu. Na Kristo ameyafikia hayo kwa kupitia njia ya unyenyekevu na utii.

Somo la Injili ya dominika ya Matawi huwa kwa kawaida ni historia ya Mateso ya Yesu. Kwa mwaka huu B wa Kanisa tunaisoma historia hiyo kama ilivyoandikwa na Mwinjili Marko (14:1-15:47). Ni historia inayoanza pale amapo wakuu wa makuhani na waandishi wanatafuta namna ya kumkamata Yesu na kumuua. Na inaishia pale ambapo azma yao hii inakamilika, Yesu anakufa Msalabani na anazikwa. Ndani kuna matukio mengi sana yanayoelezwa. Ni ngumu kuyafupisha kwa sababu kila moja lina maana yake. Na hii ndiyo moja ya sababu kwamba historia hii inasomwa yote nzima tangu mwanzo hadi mwisho. Tuachoweza kukiona kwa haraka haraka ni kuwa Yesu anakufa Msalabani kama mtu asiye na kosa. Kushtakiwa kwake kulikuwa ni kwa sababu ya ugumu wa mioyo ya watu kumpokea kama Masiha aliyetabiriwa na kama mjumbe wa Mungu anayekuja kuleta ukombozi. Nia hii ilifanikiwa kwa sababu ya chuki, hila na usaliti waliomfanyia hata wale waliokuwa karibu naye.

Tunaona pia kuwa Yesu anayakabili mateso yake hayo kwa hiyari yake. Kwa sababu alijua ni sadaka anayoitoa akiwa na utashi kamili. Kama mwanadamu alihitaji nguvu ya kimungu ili kuyatimiza mapenzi yake, ndiyo maana alienda katika bustani ya Getsemani kusali. Na mwisho tunachokiona ni mazingira yenyewe yalivyokuwa. Kifo cha Yesu kinatokea wakati ambayo wayahudi wanaadhimisha pasaka yao ambayo Yesu pia anaishiriki. Lakini katika pasaka hiyo hiyo ya wayahudi, Yesu anaadhimisha Pasaka yake, mpya kabisa, Pasaka ambayo tangu wakati huo ndiyo wote waliokombolewa naye wataiadhimisha hadi atakaporudi. Na Pasaka ya Yesu sio tena ile ya kuwakomboa wayahudi kutoka utumwani Misri bali inakuwa ni kuukomboa ulimwengu mzima kutoka katika utumwa wa dhambi anayehusika katika Pasaka hii. Tena sio mwanakondoo – mnyama anayechinjwa ambaye damu yake inapakwa kwenye miimo ya milango, ni Kristo – mwanakondoo wa Agano Jipya anayejitoa mwenyewe sadaka na damu yake inapakwa katika mioyo yao wote wanaompokea. Ili kama damu ya mwanakondoo ilivyowakomboa wayahudi kutoka lile pigo lililoipiga Misri basi sasa damu ya Kristo iukomboe ulimwengu mzima.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, kwa adhimisho la dominika hii ya Matawi tunaingia katika Juma Kuu ambamo ndani yake tunaadhimisha mafumbo makuu ya ukombozi wetu. Mfungo wetu wa Kwaresima, bidii ya kuishi katika maisha ya fadhila na matendo mema kwa njia ya sala, toba na wongofu vilikuwa pia na lengo la kutandaa kushiriki kikamilifu maadhimisho haya makuu. Tuzidi kuomba neema na tuzidi kujibidiisha ili kweli tuyashiriki kikamilifu. Ni muhimu kuzingatia kuwa maadhimisho haya ya mafumbo matakatifu, hatuyafanyi kama kumbukumbu tu. Ni zaidi ya kumbukumbu. Na ni zaidi kwa sababu kwa njia yake, kazi ya ukombozi inaendelea kutendeka ndani yetu. Kwa njia yake mafaa ya ukombozi na neema zake zinafanyika upya ndani yetu. Kumbe kuyashiriki tukiwa na maandalizi mema kiroho ni hatua muhimu ya kuyapokea matunda ya kiroho ambayo maadhimisho haya yanaleta kwetu na kwa ulimwengu mzima.

Katika dominika hii Kristo anatuonesha kuwa ametuokoa kwa njia ya unyenyekevu na utii kwa mapenzi ya Mungu. Ni njia dhaifu na isiyopewa nafasi katika macho ya ulimwengu tunaoishi. Na Yesu bado hajaacha hata leo kutujia kwa neema zake akiwa ameuficha umungu wake ndani ya maumbo dhaifu ya mkate na divai katika Ekaristi Takatifu. Ni kutuonesha bado thamani ya unyenyevu wake na ya utii wake ambavyo vinabeba upendo mkubwa. Upendo uliompelekea Yeye kuutoa uhai wake kwa ajili ya ulimwengu. Njia inayoonekana ndogo ila iliyobeba upendo mkubwa na iliyo na nguvu kubwa ya kuokoa. Mungu na awashe ndani yetu upendo kwake na kwa wenzetu ili kwa njia ya upendo wetu, ukombozi aliotuletea Kristo uzidi kudhihirika katika maisha ya watu wote.