Rais wa Tanzania John Magufuli afariki

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli amefariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa akipatiwa matibabu.

 

Taarifa za kifo cha Rais Magufuli, zilitangazwa jana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ametangaza kifo akisema Magufuli alifariki dunia saa 12 jioni kwa maradhi ya moyo baada ya kulazwa katika hospitali hiyo tangu Machi 6.

 

Amesema awali, Rais Magufuli alifikishwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Machi 6 akisumbuliwa na tatizo la moyo la mfumo wa umeme ambalo alikuwa nalo kwa zaidi ya miaka 10.

 

“Machi 14 mwaka huu, alijisikia vibaya akakimbizwa hospitali ya Mzena ambako aliendelea na matibabu chini ya uangalizi wa madaktari na wauguzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete hadi umauti ulipomkuta,” amesema Mama Samia.

 

Amesema Tanzania itakuwa katika kipindi cha maombolezo ya siku 14 na bendera zitapepea nusu mlingoti. Alisema wananchi watajulishwa juu ya taratibu za mazishi za kiongozi huyo mkuu wa nchi.

0 Comments

leave a comment