TABIA NI JAMBO LA MOYO SI LA MAZINGIRA YA NJE… Mpendwa msomaji, leo ninapenda tuzame kidogo ndani ya fikra ya kimaadili kuangaza kwa dhati ili kuelewa kuwa ‘tabia ni jambo la moyo wala si la mazingira ya nje’ yanayomzunguka mlelewa. Mintarafu malezi na ukuaji wa kitabia kwa kijana awaye yote, ni vigumu sana siku hizi kumkuta mtu akipingana na wazo linalofundisha kuwa ‘daima tabia huwa inaundwa na kuathiriwa na mazingira ya nje kama vile nyumbani anakotoka, shule aliyosoma, umaskini ama utajiri wake au mazingira aliyolelewa. Mwishoni mwa mada hii utakuwa umenielewa fika na kupata kile ambacho nimedhamiria leo ukipate.

 

Tunao msemo katika Kiswahili usemao: “Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.” Lakini ukweli wa mambo hauko namna hiyo. Mazingira ya mlelewa huathiri tu hali yake, lakini hayawezi kamwe kufanyiza tabia yake.

Tangu siku ya kwanza tulipoanza kuleta mada juu ya malezi ya vijana, tumeweza kuona dhahiri kuwa vijana wengi wamekengeuka kitabia. Muda wote tumekuwa tukiangaza juu ya ukweli kwamba mazingira ya vijana walipo sasa yamewaathiri kufikia hali hiyo lakini si kweli kwamba mazingira hayo yamefanyiza tabia zao. Ni nini chanzo cha tabia sasa? Chanzo cha tabia alikinyoshea mkono Bwana wetu Yesu Kristo aliposema:

 

Nisikieni nyote na kufahamu. Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu…Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya: uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi (Mk 7:14-23).

Kwa kusema hivi ‘Yesu alivitakasa vyakula vyote.’ Lakini ujue kuwa hii ilikuwa sababu mojawapo kuu iliyomsindikiza kwenye hatima ya kifo chake msalabani kwa mateso yasiyo kifani. Kwanini ilikuwa hivyo?

 

Historia inatuambia kuwa, Mfalme Antioko IV Epiphanes, mfalme wa Kigiriki ambaye majeshi yake yaliivamia na kuiteka Israeli yapata mwaka 170 K.K, alikuwa mfalme katili sana. Antioko IV alidhamilia kuondoa kabisa imani ya Kiyahudi hivyo akaandaa madhulumu ya kutisha kidini. Mfano wa madhulumu hayo yameelezwa kinagaubaga kwenye Kitabu cha Pili cha Wamakabayo. Wale vijana saba walioteswa na kuuawa mbele ya mama yao mjane kwa sababu wamekataa kula chakula najisi, nyama ya nguruwe, yaani, Kitimoto (2 Mak 7).

 

Mafarisayo walikasirika sana pale Yesu alivyofutilia mbali sheria za usafi wa chakula namna ile ambapo mababu zao walikufa wakizitetea. Lakini Yesu kimsingi fundisho lake lilikuwa hili:

Kinachomfanya mtu awe najisi si kile kiendacho tumboni, bali kile kitokacho kwenye moyo wake.

 

Ni jambo la kujiuliza kama sisi tunaiona dini yetu ni kama jukumu la nje tu na si la moyo. Ndiyo maana mara nyingi tunaishi kwa kuangaliana mambo ya nje tu kumbe ndani mwetu, yaani, roho zetu zinawaza mambo ya ajabu na ya kipagani kabisa.

 

Saikolojia ya sasa inapigia debe sana umuhimu wa akili iliyofichika (subconscious), lakini Yesu anasisitiza juu ya umuhimu wa akili ya utambuzi wa mambo (conscious factor). Hapa ndipo akili na utashi ni makao ya kudumu.

 

Ndiyo kusema, ufahamu na maamuzi yetu yanapaswa kuongozwa na akili na utashi wetu kama binadamu na wala si vinginevyo. Muunganiko wa mambo haya mawili wakati mwingine huitwa Moyo, na humo ndimo tabia hutoka kama ilivyo kwenye mti wa mwembe ndipo tunapata maembe.

 

Mageuzi ya mwenendo na mazingira ya nje kama tulivyokwisha kujadili huko nyuma ni muhimu sana maana huku ndiko sheria za nchi zimezaliwa na kushamiri. Kwa maneno mengine, mageuzi ya mwenendo na mazingira ya nje hushughulika zaidi na matokeo tu ya tabia na wala si chanzo cha tabia. Mageuzi ya kijamii ni ya juu juu tu; ni kama kukata magugu juu juu huku mizizi yake bado imejisimika ndani ardhini.

 

Ni katika kiwango kidogo sana mazingira humuunda kijana, hufanya hivi kwa kiwango kwamba kijana huruhusu mazingira yamuunde kuwa jinsi alivyo. Si kitu cha nje huathiri ndani ya kijana ikilinganishwa na kitu cha ndani kinavyoathiri nje yake. Kama chanzo cha mto kitakuwa safi, vijito vyote vinavyomimina maji ndani mwake lazima viwe safi.

 

Uovu una mizizi yake ndani kabisa ya moyo. Hivyo basi, “Kadiri mtu anavyofikiri moyoni mwake, ndivyo alivyo kwa nje. Na hii kwa kweli ndiyo tabia yake.” Kwa maneno mengine, tabia ya kijana imeundwa na mawazo yake. Ewe kijana, jaribu kutoa mawazo yako hadharani tukuelewe jinsi tabia yako ilivyo!

 

Kama mawazo, shauku au matashi ya moyoni yatabeba hazina ya maamuzi na fikra potofu au mbaya, haichukui muda mrefu kujenga mihimili ya tabia mbaya kwa nje; kinyume chake ni kweli kwamba, fikira, mawazo na matashi ya moyoni yakiwa mema, tabia huwa njema, takatifu na safi sana.

 

Kwenye kitabu chake, Way to inner peace, Askofu Mkuu Fulton Sheen akiyatetea yote yaliyoelezwa hapo juu ameandika hivi:

Uovu si mwivi anayevunja na kuharibu kwenye nyumba yetu; Uovu ni mpangaji ambaye nyumba imepangishwa kwake. Kama tutaiweka mioyo yetu katika hali ya usafi wa Kimungu, tutaweza kuyabadili mazingira yetu.

 

Kwa maneno hayo tunahitimisha kwa kishindo kikubwa kuwa: TABIA NI JAMBO LA MOYO NA SI LA MAZINGIRA YA NJE.

Pd. Dkt. Stephen NYAKUMOSA Kadilo

Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi ya Afya na Tiba Shirikishi cha Mtakatifu Francis (SFUCHAS)-Ifakara.