KIJANA ALIPO SASA-TOLEO LA KUMI

KUJENGA TABIA NJEMA KWA KUTUMIA UTASHI

Kijana akishikilia maadili sawa sawa anakuwa na afya njema kimwili na kiroho, atakuwa mwenye dhamiri isiyo na madeni.Kijana ataishi maisha yenye maamuzi sahihi na kwa kweli hii ndiyo huitwa busara. Ili kuishi na jamii vizuri na hivyo kujenga mahusiano mazuri kijana anapaswa kuwa mtu wa utashi maridhawa katika kuenenda kwake. Kwa ujumla kuwa na utashi imara ni uamuzi maalumu wa kuamua kuacha kile kiovu na kukumbatia kile kilicho chema kwa ufanisi wa nafsi ya mtu na jumuiya nzima inayokukabiri ama uliyonayo.

Kuna mambo kadha wa kadha ambayo yanahitaji kufanywa kwa kuzingatia utashi na bila hiyo hali basi mambo mengineyo ya msingi hayawezi kwenda mbele katika ufanisi wa kawaida wa maisha na hata maana nzima ya kuishi kwetu sisi binadamu. Mambo ya kuimarisha utashi wetu ni kama: Tabia njema katika kuishi maisha yetu, Utakatifu katika maisha yetu na Msamaha kwa Mungu na kwa wenzetu.

  1. TABIA NJEMA:

Tabia njema ni pato la utashi kamili. Bwana wetu Yesu Kristo kwenye hotuba ya mlimani alisema: ‘Basi iweni wakamilifu kama baba yenu wa mbinguni alivyo mkamiligu’ (Mt 5:48). Kumuiga Mungu jinsi alivyo na ukamilifu au utakatifu wake ni jambo la maamuzi na ni la kitabia linalojifumbata kwenye mhimili wa tabia njema. Tendo la kitabia linapaswa kuwa la kujirudiarudia mpaka iwe tabia halisi kwa maana tabia haipimwi kwa tendo au tukio moja tu.

Tunawezaje kubadili tabia mbaya kuwa njema? Ni lazima kuwe na wazo jipya lenye ukamilifu la sivyo turudie wazo la zamani ambalo limesahauliwa. Hapa panahitaji msukumo wa ndani wenye mvuto na hamasa ya kubadili tabia yetu.

Haitoshi tu kuwaambia watu waache jambo fulani bila kuwapa kitu cha kufanya badala yake. Tena, kuacha jambo fulani ghafula bila kitu cha kufanya badala yake kwaweza kuzalisha ombwe na utupu usio na msingi wowote. Nyumba isipojazwa na wema, uovu huingia mara moja na kuanza kutawala. Hivyo ni lazima kuwa na mabadilishano ya kitu kimoja kwa kingine na mabadilishano haya yawe kati ya kile ambacho tunanuia kukiacha kwa kile ambacho tunataka kuwa nacho maishani.

Zakayo katika Injili ya Luka alikuwa mwanasiasa ambaye hakuwa mwaminifu kwenye kazi yake ya utoza ushuru; lakini alipopata wazo jipya kupitia ugeni wa Bwana Yesu nyumbani mwake, alifanya maungamo makuu yenye kubadili tabia. Maria Magdalena alipoacha tabia yake mbaya ya uhuni, aliweka wema badala yake kwa kuona kuwa usafi wa Kimungu (Divine purity) inafaa Zaidi kuliko mambo machafu aliyokuwa anayafanya.

Saikolojia inatuambia kwamba huwa tunatenda kutokana na kile tunachoamini. Hivyo, kama mawazo na Imani ni mabaya, matendo yetu lazima yawe mabaya tu. Mwanzoni ni vvema sana kubainisha mawazo mema ya msingi ili tutende kadiri ya mawazo hayo. Saulo alipokuwa anatenda kwa kutumia mawazo ya chuki, alilitesa vibaya sana kanisa la Mungu kwa kuwadhulumu vikali wakristo wa mwanzo. Lakini alipobadili mawazo na kuongoka aliitwa Mtume Paulo. Ndiye mtume aliyetenda mambo mengi kuliko wengine katika utume na mateso mengi katika maisha.

Haitoshi tu kugundua wazo jipya, kitu kingine cha muhimu ni kuwa na nguvu ya nje itakayotusaidia. Hii ndiyo NEEMA ya Mungu ndani yetu.

Tukiwa watumwa wa tabia mbaya, si rahisi kwetu kuukata mnyororo wa uovu. Tukikamatwa na makucha ya tabia mbaya tukasafiri kwenye barabara za uovu, inahitajika nguvu ya kimungu kutugeuza na kutufanya tuende upande tofauti. Hapa ndipo kanuni ya kifizikia ya Kijana machachari Isaack Newton ndipo inaposhika hatamu alipotunga kanuni za mwendo (Laws of inertia) akasema:

Kitu kilicho kwenye mwendo, kitaendelea kwenye uelekeo wa mwendo huo isipokuwa kama kuna nguvu kinzanifu.

Kwa kweli neema ya Mungu ndani mwetu ndiyo nguvu kinzanifu ya matendo na tabia mbaya. Nguo (suluari, gauni au shati) ambalo limeshaharibu mfinyo haiwezi kujinyosha yenyewe. Pasi ni nguvu ya nje inayotumika kurejesha mfinyo huo na kuifanya nguo iwe imenyoka tena.

Punde akili inapopata wazo jipya na kugundua kuwa ina umaskini wa roho, huhitaji nguvu ya nje (neema) na hivyo lazima kuwe na ushirika wa pekee sana na utashi.

Kiswahili sanifu kinatupatika maneno mawili yenye kushabihiana lakini yenye uwezo tofauti wa kiutendaji. Shauku (wish) inaweza kugundua wazo fulani lakini haiwezi kutilia maanani ufuatiliaji wa jambo au wazo hilo. Utashi (will power) hushirikiana na neema ya Mungu ili kuamua jambo zuri na jema. Lengo la utashi ni kuondoa shauku ya uovu ndani mwetu.

Je, tendo la kuondoa tabia mbaya ni la haraka au pole pole?

Bwana wetu Yesu Kristo anatufundisha na kuonesha kuwa tabia mbaya ni ya kuondoa haraka wala si ya kubembeleza. Alifundisha akasema:

Jicho lako la kulia likikukosesha, ling’oe na ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika Jehanum (Mt 5:29).

Kama kuna jambo ambalo linakusababisha ushindwe kutimiza wajibu wako dawa yake kuu ni kuachana nalo mara moja. Askofu Mkuu Fulton Sheen anasema hivi:

‘Iruhusu akili yako kuonja furaha ya mambo mema na itaomba tendo hilo lirudiwe tena.’

Unapokuwa na wazo zuri halafu ukashindwa kulifanyia kazi tabia huumia.Ni vema sasa kutambua kuwa ni vema sana kujiweka kwenye  mazingira ambayo kuna uwezekano wa kuwa na mazingira yanayoruhusu maendeleo ya ukuaji wa tabia njema inayojikita katika maamuzi sahihi na matumizi mazuri ya utashi kwa kuwa tabia ni hamali ya utashi na si akili. Hivyo machaguo yetu, maamuzi yetu na hamasa zetu hutufanya tuwe tulivyo. Kama maamuzi yetu ni mabaya na tabia zetu pia itakuwa mbaya licha ya kufahamu mambo mengi kwa kutumia akili zetu. Mwandishi wa kitabu cha Mithali yuko sahihi kabisa anapoonya juu ya matendo ya kiakili na kuonesha kuwa tabia njema ni njia ya Kimungu. Anasema hivi:

Mtumaini Bwana kwa Moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe; katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako (Mith 3:5-6).

Tabia ndiyo inapaswa kubadilishwa. Michelangelo alisema: ‘Bwana, uniondoe ndani yangu mwenyewe na unifanye nikupendezeshe wewe.’ Naye Askofu Mkuu Fulton J. Sheen anasema hivi:

Kama tabia yetu haitabadilika ndani mwetu, lakini ikawa ya nje tu, tutakuwa kama mtu anayesafisha kioo cha nyumba kwenye asubuhi yenye baridi. Anavyoendelea kupangusa, ukungu huondoka kwenye kioo kimoja lakini hujikusanya kwenye dirisha jingine. Kuwasha moto ndani ya nyumba kungesafisha vioo vyote

Upendo mpya, upendo wa Kimungu lazima uwashwe toka moyoni ndipo ubaya utapotea. Mtakatifu Augustino alikuwa na haya ya kusema:

Mpende Mungu halafu ufanye unavyotaka. Kwa sababu kama utampenda Mungu, hutafanya kitu chochote kuuhaaribu upendo.

Pd. Stephen NYAKUMOSA Kadilo, MD

Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi ya Afya na Tiba Shirikishi cha Mtakatifu Francisco (SFUCHAS) – Ifakara.

0 Comments

leave a comment