MWANASANAA NI MLEZI WA VIJANA.

Kamusi ya Kiswahili Sanifu inatoa maana ya sanaa. Inasema hivi: sanaa ni ufundi wa kuwasilisha mawazo yaliyomo katika fikira za binadamu ili yadhihirishe sura mbalimbali kama vile kwa maandishi, michoro, uchongaji na kadhalika. Kwa upande mwingine Muziki umeelezwa kuwa ni mpangilio wa sauti za ala na uimbaji unaoleta athari fulani kwa kiumbe; nyimbo.

Kumbe, kwa kupita katikati ya mistari na kwa fikra sahilifu, mwanamuziki ni mwanasanaa ambaye ni kioo cha jamii mwenye kuleta athari yenye mvuto wenye kuigwa kirahisi sana kwenye jamii hivyo anatakiwa kuwa mlezi makini sana la sivyo anaweza kuipeleka jamii nzima shimoni kwa upande wa maadili. Ndiyo, nakubaliana na fikra hii kwani nimeona mambo mengi sana yanayofanywa na wanasanaa yakivuma kwa haraka sana katika jamii hata yale ambayo ni fedheha kwa maadili yetu kama binadamu.

Wanamuziki wengi wana mitindo mbalimbali ya kunyoa nywele ama kuvaa nguo zao na ninazidi kuona watu wengi wanafuatisha na kuiga mitindo hiyo kwa kasi kubwa, kucheza, kuimba au kutembea kadiri wanamuziki wanavyochipuka kila kukicha. Napongeza sana jambo jema na zuri linaloletwa na wataalamu hawa kisha likaenea kwa haraka na kufurahisha watu bila kuharibu maadili kwa namna yoyote ile hapa nikipongeza muziki wa zamani uliosaili jamii bila kuleta vionjo na hisia tofauti kimaadili. Napongeza sana melodia nzuri na za kuvutia ambapo nyimbo zsizo na maadili kijamii zinapobadilishwa ili kumsifu kiongozi fulani wa nchi huwa mzuri na zenye kuvutia kila sikio la msikilizaji. Kwa upande mwingine ninalaani vikali mambo yasiyo na maana yanayoanzishwa na kuenea haraka hata kama yanadhalilisha maadili na tunu zetu njema za Kitanzania na Kiafrika.

Mara nawaona wanamuziki wa kiume wakivaa vizuri na kucheza vizuri. Loo, inavutia na kkupendezesha sana! Nafurahi na kushangilia nikiona watu wakiwa wanacheza kwa ustaarabu huku wakiimba kisha kuwapa zawadi wachezaji hawa. Ama kweli, mcheza kwao hutuzwa! Wanaume wakiwa wamevaa nguo zao bila kuacha sehemu yoyote ya mwili wao ukipigwa na upepo ni jambo adilifu sana. Nabaki nikijiuliza, kwanini akinadada wao hupenda kuvaa nusu uchi ili wacheze? Nani aliamuru kwamba ukiwa nusu uchi ndipo utacheza na kufurahisha watu kama si kuita tamaa na mwisho wake ni balaa tupu? Kwanini mwanamke anatumika kama chombo cha kufurahisha watazamaji na yeye akakubali hali hii? Mbona akifanyiwa matendo mengine kinyume cha utu husema amenyanyaswa kijinsia wakati katika muziki anajipa nafasi ya mbele ya kadamnasi kuwa uchi bila kujali? Kwanini hakuna mtu anayekemea halii hii? Serikali uliyemwangalizi mkuu uko wapi? Hii ni ajabu sana kwangu!

Baadhi ya nguo ambazo hazina maadili huvaliwa kwenye muziki. Ndipo aina ile ya nguo tuliyoijadili wiki iliyopita tunaikuta ikitumika sana kwa wanamuziki hasa wa ulaya na kuigwa na ‘wabongo’ walio mashuhuri kudaka mambo mengi kwa kuigiza. Kama Mmarekani ataleta jeans iliyotatuka na kuubana mwili wako ikawa fasheni ya kunua nchini mwako na ukajisia sawa, hii si dalili ya utumwa wa kifikra? Akiona tumeukubali udhaifu huu hawezi kutuletea kitu kingine na kuingiza tamaduni nyingine zisizofaa kwa kivuli cha uhuru wa kuamua mtu anavyotaka kufanya na afanye? Ndiyo maana watu hawa wangetaka ndoa za jinsia moja na utoaji mimba ziwe kati ya haki za binadamu tungepokea bila shida. Baadhi ya watu hapa nchini wanabanwa tu na sheria za nchi la sivyo wangekuwa wameshajitangazia uhuru wa kufanya mambo haya hadharani. Hata hivyo, mambo haya yamo nchini kisirisiri maadamu ni jambo la kuiga; jambo la kuiga daima ni tamu. Loo, huu ni umaskini mbaya kuliko ule wa kukosa fedha mfukoni!

Kungekuwa kumeruhusiwa kuingia makanisani huku vijana wamevaa wanavyotaka huenda wangekuja wakiwa wamevaa kadiri wanavyoonekana mtaani kwani huenda wengine hawana nguo ya staha hata moja. Vijana wangeruhusiwa kuingia wakiwa na namna mbaya ya unyoaji wa nywele, ibada zingeendeshwa kama wote tuko klabuni. Vijana nawasihi mfikiri upya na  kijasiri kurudi kwenye mstari wa maadili kwani ninyi si ‘samaki ambao mmeshashindikana kukunjika.’

Namna muziki unavyotungwa nyakati hizi mbona ni tofauti na miaka ya nyuma? Muziki unatungwa ukieleza mapenzi kwa lugha isiyo na kina katika kufumba. ‘Fumbo mfumbie mjinga, mwelevu huling’amua.’ Nionavyo mimi na ndivyo ilivyo, haihitaji welevu kufumbua fumbo la wimbo wa mwanamuziki wa Tanzania kwa namna ya pekee. Maneno ya matusi ya kweli kiasi kwamba kusikiliza muziki wa sasa huku uko pamoja na wazazi wako bila kuona aibu ni dalili ya umbumbumbu wa maadili katika mwendo wima kuielekea mifumo ya maisha ya wanyama ambao wana akili bila kuwa na utashi wa kuamua jema au baya.

Katika maisha ya kiroho, kama jambo baya katika jamii litafanyika bila kukemewa basi ni dalili ya ukomavu wa roho ya kipagani na kishetani. Kwanini serikali haizuii muziki na uchezaji usiofaa? Mama anatikisa makalio kwenye ‘muziki wa singeli’ huku akishangiliwa aendelee ‘kumwaga lazi’ na hata kuinua nguo kumbe hata nguo ya ndani hana anategemea kuvuna nini kutoka kwa binti yake anayemwona akifanya hivyo? Je, matendo yasiyofaa ni sehemu ya kukua kwa jamii kuelekea maendeleo ama upotevuni? Kitengo kinachoangalia ustawi wa wanasanaa hawa (BASATA) hauoni maadili yanavyoharibika nchini mwetu au mpaka tuzomewe na nchi jirani ndipo tushtuke kubadili mwenendo wetu? Ni ajabu na inasikitisha sana!

Nakiri na kuamini kuwa muziki ukitumika vizuri utarekebisha mambo mengi na kuwaleta vijana katika mstari wa maadili mema. Muziki utapendwa kusikilizwa na wengi pasipo kikwazo, muziki utaangaliwa na kuchezwa kwenye familia bila kuogopana. Na pia ujumbe wake utakuwa fundisho kwa jamii nzima. Lakini kwanini sasa mambo yanazidi kuwa hivi isivyofaa kila kukicha?

Mwanasanaa na kwa namna ya pekee mwanamuziki ni mlezi anayependwa sana lakini ameonekana yeye mwenyewe kuwa mlegevu katika kuwasaidia vijana wenzake kuondokana na ulimbukeni wa kuiga mitindo yake isiyofaa. Nampongeza sana mwanamuziki anapofanya vizuri na kuwa kioo cha jamii na kujenga umoja kwa burudani  na kucheza kwa umaridadi na wepesi wa mwili. Hima hima wazazi, walimu shuleni na vyuoni, viongozi wa dini na serikali kwa pamoja elekezeni macho kwenye tasnia hii nzuri ili ibadili vijana wengi kuelekea mitindo ya uungwana na maadili na pia kujenga tabia njema. Najua maoni yangu ni kama alivyoimba mwanamuziki Remmy Ongala, ‘kilio cha samaki machozi huenda na maji’ lakini naamimni kuwa ‘ndo ndo ndo si chururu! Ninyi wasomaji mkiniunga mkono kupinga upotoshaji huu wa maadili, nitaendelea kuamini kuwa ‘haba na haba hujaza kibaba.’ Tukiwa pamoja kupinga mambo mabaya kwenye tasnia ya Muziki, nitazidi kuamini kuwa ‘Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu.’  Karibuni tujenge chetu pamoja!

Pd. Dkt. Stephen NYAKUMOSA Kadilo

Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi ya Afya na Tiba Shirikishi cha Mtakatifu Francisko (SFUCHAS) – Ifakara.