WAZAZI NA WALEZI

Kijana anahitaji kupata taarifa muhimu za kimalezi lakini ijulikane kuwa malezi anayoyapata kutoka kwa wazazi na walezi ni tofauti na yale anayopata kutoka kwa makundi yake ya makuzi (marafiki).

 

Mzazi anaweza kumzuia kijana kutumia muda wake mwingi kuangalia Televisheni ama intaneti lakini yote hayo anaweza kuyafanya akiwa na wenzake. Kumbe majibu ya maswali mengi ambayo walezi wanachelewa kujibu ama wanaogopa kuwaambia vijana waziwazi mara moja wanayapata wakiwa na wenzao. Mzazi anafungwa na mila na uhusiano wa karibu na kijana wake lakini hapa kuna namna nyingine ya kufanya. Wajomba na shangazi tangu zamani walikuwa ni watu wa muhimu sana kufikisha ujumbe muhimu kwa vijana.

 

Makabila mengi sana hapa Tanzania bado yanatumia namna hii kufikisha ujumbe na mafanikio ni makubwa hasa kwenye ustawi wa maisha ya ndoa na malezi katika makuzi. Ni heri kubwa sana kuwatumia hawa ili kuwaweka vijana katika malezi yenye kuzingatia maadili mema bila kukwepa wajibu wao. Sehemu ambazo kumekuwa na aibu kuzungumza mambo mbalimbali yahusuyo makuzi na malezi zimekuwa na idadi kubwa ya wasichana kuolewa ama kupata ujauzito katika umri mdogo kiasi kwamba ‘mama anazaa mtoto wakati yeye bado ni mtoto.’

 

Katika hali hii kumekuwa na mwongezeko wa magonjwa mbalimbali yanayoendana na tatizo hilo la kuzaa mapema kama vile kuongezeka idadi ya wagonjwa wa kansa ya shingo ya kizazi, kuongezeka kwa matatizo wakati wa kujifungua: mimba kutoka mapema (miscarriage), mimba kutolewa (abortion), kushindwa kujifungua kwa sababu nyonga hazijatanuka ipasavyo (inadequacy of pelvis), kuzaa watoto wenye kifafa (Cerebral palsy) na kadhalika. Isitoshe, mimba za mama ambao bado ni watoto zimepewa jina ambalo linaleta ukakasi kwa malezi ya yule atakayezaliwa-Unwanted pregnancy.

 

Hii mimba isiyotakikana inaonekana kuwa hata atakayezaliwa hahitajiki: hiki ndicho kisa cha mimba nyingi kutolewa na mama kugeuka kuwa adui wa wale wasio na hatia. Vitu vinapothaminiwa zaidi kuliko maisha kumesababisha tuwe na mashirika yanayosaidia kuteketeza maisha ya watu kwa kusudi la kupanga uzazi ili dunia isijae watu. Mungu utusamehe na kutunusuru!

WALIMU 

Walimu wana nafasi kubwa sana ya kutoa majibu kwa maswali mengi ya vijana kwa nyakati nyingi wakiwa na vijana shuleni na vyuoni. Kinachosikitisha tu ni kwamba ukiukwaji wa maadili unaoletwa na sera kandamizi za uhai wa binadamu zinafundishwa na walimu mashuleni na vyuoni kungali mchana kweupe.

 

Matumizi ya vidhibiti mimba linapokuwa somo darasani unabaki unajiuliza, kwanini njia mbaya inahalalisha tendo ovu? Katika maadili, haitakiwi kitu chema kifikiwe kwa njia mbaya. Kupanga uzazi ni kitu kizuri ikitumika ile njia nzuri iliyopo yaani njia ya Kalenda (Bill’s method).

 

Ifahamike bayana kwamba, kila kitu kinachozuia mpango wa Mungu kufanyika au kutimilika daima hicho si kitu chema na si halali kukifanya au kukitekeleza. Kamwe lengo huwa halihalalishi njia. Ikitokea popote pale lengo likahalalisha njia, basi huo ni uovu na tena ni dhambi kubwa.

Inashangaza sana unapokutana na mwalimu kisha akaanza kuporomoka maneno mazito: ‘vijana wa siku hizi kimalezi wameshindikana kabisa. Hawasikii na hawafuati ushauri.’ Mpendwa mwalimu, haya maadili yaliyokufiksha hapo hukuyapata toka kwa walimu hapo zamani ulipokuwa wa umri kama vijana hawa unaowakatia tamaa? Tafadhali wajibika!

 

VIONGOZI WA DINI

Viongozi wa dini wanapaswa kunuka harufu ya wale wanaowaongoza. Kamwe wasiwaache vijana bila kuwatafutia namna njema ya kuwakutanisha na kuwapa mafundisho yafaayo katika makuzi ya rika zao mbalimbali. Kuwafundisha matumizi mazuri na manufaa ya michezo kwa kuwafanyia matamasha yenye semina na mawaidha mbalimbali ya maisha kama uchumba, uzazi, ndoa, maisha ya wakfu na mashauri mengine ya kidini na kimaadili. 

 

Aidha, kuwe na maelekezo sahihi ya matumizi ya nguvu za kimaumbile ambazo vijana wanazo kwa kuzielekeza kwenye utume mwema zaidi badala ya kuwaza mambo mabaya na kukumbatia nafasi za dhambi. Mafundisho ya kiroho yatoe mbinu mbadala za kukwepa nafasi zinazoongoza miili ya vijana kwenye hisia bila kuitawala miili yao.

 

VIONGOZI WA SERIKALI

Viongozi wa serikali wasimamie mitindo ya maadili na si kufumbia macho uovu. Ipo mitindo mibaya ya uvaaji lakini hakuna anayesema neno. Kama anayeendesha biashara ya ngono hukamatwa sanjari na mtu wa madawa ya kulevya, kwaje asikamatwe na kukalipiwa yule anayetembea nusu uchi? Sauti hii ya katazo imebaki makanisani tu: ‘Ndugu waamini, tunaomba mzingatie kuzima simu na kuvaa nguo za staha!’ 

 

Mintarafu mwenendo mwema wa uvaaji, ni jambo la msingi sana katika jamii kufundisha na kusimamia ukweli kwamba kadiri mtu anavyoonekana amevaa, huashiria tabia na mwenendo mwema kitabia. Jambo hili linakubalika hata kitabibu: 

 

‘ngozi ya mwanadamu kuonesha ugonjwa wake alionao ndani ya mwili wake hata kabla hajajieleza kwa daktari. Makucha yakirefuka kwa kujipinda kama yalivyo ya mwewe ama vidole kuvimba na kuwa kama fimbo ya kupigia ngoma mara moja tunagundua kuwa mtu huyu ana shida ya kudumu ya kifua.  Kama nyayo zitakuwa na madoa meusi hapa tunapata hakika ya shida fulani kwenye ini na kadhalika.’ 

 

Hali kadhalika, mavazi nayo huashiria tabia na mwenendo mwema ingawa siku hizi kwa kugundua hivi mwizi naye ameanza kuvaa kwa utanashati na ulimbwende japo kwa ndani ni mbwamwitu mkali.Hata hivyo inabaki ni ukweli mtupu kuwa faida za kuvaa vizuri kitabia ni nyingi zaidi kuliko kuvaa vibaya.

 

Mtu anayeenda kwa mahojiano akitafuta kazi huanza kwa kujizatiti kimavazi na maarifa au ujuzi huja baadaye. Hii ni kwanini? Mavazi huzungumza lugha ya kitabia na hivyo kumwonesha mtahiniwa kuwa anafaa au hafai hata kabla ya kuanza kuzungumza chochote.

 

Kuvaa mavazi yanayolingana na sehemu ulipo ni msaada mkubwa sana katika hatua za kukuwezesha kufahamika haraka. Mfano kubebwa kwenye pikipiki au taxi na kijana ambaye amevaa suluari ya jeans iliyonunuliwa mpya toka dukani ikiwa imetoboka na kuwekewa viraka humfanya yule aliyebebwa afananishwe na hulka ya tabia mbaya ya yule aliyembeba. Hali hii yaweza kusababisha udhaifu fulani katika mapokezi na hata utendaji kazi kutoka upande wa wale wanaompokea. Ukinionesha rafiki zako, nitakuambia tabia yako ilivyo!

 

Jamii yetu japokuwa bado inapambana kuwaondoa maadaui wa maisha, yaani, maradhi, ujinga na umaskini, bado vita hii inazidi kupamba moto. Bado tunao watu ambao wanavaa viraka kwa sababu hawana uwezo mkubwa wa kununua nguo. Inapotokea mtu akanunua nguo mpya yenye viraka ni tukano kwa asiye na uwezo wa kujinunulia nguo mpya. Dharau hii ni mbaya kwani ni tukano la ukarimu wa majaliwa ya Mwenyezi Mungu. 

 

Ni kukosa shukrani kwa wema uliojaliwa na Mungu. Uwezo wa kupata hicho ulichonacho. Kwa mwanadamu kutokuwa na shukrani kwa Mungu ipasavyo kumemfanya Padre Dr. Ndelacho David Msaki ALCP/OSS kuhitimisha kitabu chake chenye anuani ‘Kushukuru ni kuomba tena’ kwa maneno haya: ‘Kichwa kisichofikiri vizuri ni mzigo kwa kiwiliwili chake.’

 

Je, wanasanaa wana mchango wowote kwenye malezi na makuzi ya vijana? Jibu lake ni ndiyo. Tutafafanua jibu hili wiki ijayo!

Pd. Dkt. Stephen NYAKUMOSA Kadilo, MD

Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi ya Afya na Tiba Shirikishi cha Mtakatifu Francisko (SFUCHAS)-Ifakara.