WAJIBU WA WALEZI

Mnamo mwezi wa Agosti mwaka 2020 nikiwa na Padre Achilleus Ndege tukitokea Ifakara,
tuliingia mji wa Iringa. Baada ya misa ya mazishi ya baba wa Padre Raymond Mahimbi
hatukuwa na haraka ya kurudi tulikozoea kuishi.

 

Kijana mmoja alitukuta tukiwa eneo fulani kwa ajili ya kupata chakula cha mchana. Kwa vile ilikuwa ni mchana kati, njaa ilituruhusu kula na pia kunywa kidogo kwa sababu ya wingi wa muda tuliokuwa nao. Hapa
mazungumzo hayakukatazwa eti kwa sababu ya baridi kali ya mkoa huo. Makoti yetu
yalisaidia kuleta joto walau hakuna aliyetetemeka kwa baridi.

Kijana alikuwa wa makamo alikuwa anauza vitu mbalimbali alivyokuwa amebeba kwa
mikono yake yote miwili. Alikuwa mrefu na mwili ulioshiba misuli kuonesha ana nyama
nyingi. Alikuwa mrefu karibu anaelekea kuitwa mtu wa miraba minne. Kwa mwonekano
wake, hakuwa na umri mkubwa sana na ndivyo alivyodhihirisha mwenyewe baadaye
aliposema si miaka mingi imepita alikuwa mtumishi wa misa kwenye parokia ya jirani na
pale tulipokuwa tumekaa.

 

Kijana alikuwa na mtindo wake wa kunyoa nywele kichwani. Alikuwa amenyoa nywele zote
pembezoni mwa kichwa na kuacha nywele zikiwa zimekunjamana bila kuchanwa. Nadhani
huu ndio mtindo unaitwa kiduku, mtindo unaopendwa na kutumiwa na wanamichezo na
wanasanaa wengi hasa wanamuziki hapa nchini na duniani. Miguuni alivaa viatu kikubwa

kuzidi kile cha Vasco da Gama alipokuwa anatembelea pwani za Afrika ya kusini.

 

Alivaa
soksi ndefu zilizokaribia magotini akazikunja kidogo kuelekea chini. Kwa kweli alionekana
kama anataka kwenda kwenye mechi yenye ushabiki mkubwa. Kaptula na tisheti nyeusi ya
bendera ya Taifa vilikuwa vimembana utadhani amepakwa rangi tu akaambiwa aendelee na
safari!

Mwendo wa kijana alipokuwa anatembea ulikuwa wa mikogo na alipozungumza alikuwa na
maneno yenye ushawishi na ujanja mwingi. Hii ilikuwa nzuri sana kwangu kwani najua
alikuwa kwenye biashara na inafahamika wazi kuwa biashara ni matangazo na ushawishi
mwingi kibiashara ni dalili njema ya kupata wateja wengi.

Kijana alitukazia macho wakati ananadi bidhaa zake nasi tulimskiliza kwa umakini mkubwa
vile vile lakini pia kwa matumaini kuwa tutavua samaki mkubwa vile! Tulishikwa butwaa
aliposema, ‘Hivi ninyi si mapadre?’ Tulipotaka kufahamu kwanini ameuliza hivyo, yeye
alijibu akasema, ‘mnavyozungumza na jinsi mnavyoonekana nimejua tu ninyi ni
mapadre.’ Akaendelea kusema:
Mimi nimetumikia sana kwenye misa hapa parokiani na paroko aliyepo sasa
ndiye aliyenibatiza. Basi nikamuuliza kijana nikitaka kujua kama huwa
anaenda kanisani kusali. Jibu nililoambulia ni hili: Kwa kweli padre siendi
kusali kwa sababu hamna kitu kipya ambacho kimeongezeka ama
kuboreshwa. Tangu nibatizwe na kuendelea kuja kanisani, misa

haijabadilisha fomula ya kusali. Namna ya kusali ni ile ile inayoanza na ishara
ya msalaba (kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu) na kuishia
kwa maneno, ‘Nendeni na Amani.’
Tulishangazwa sana na hoja za jibu la kijana. Hii ni dalili ya Kudharau kanisa kwa kukosa
shukrani kwa Mungu, matumizi mabaya ya uhuru na pia ni kutojitambua kwa hali ya juu
sana. Uhuru wa kweli unaonekana kwa vijana ni kufanya vile unavyotaka. Kadiri ya Askofu
Mkuu Fulton J. Sheen, aina hii ya uhuru anaiita ni uhuru wa uongo. Yeye anaweka bayana
kwa kuainisha kwamba, maelezo ya uhuru wa uongo unauweka uhuru kuwa ni haki ya
kufanya vile unavyotaka.

 

Hii huupunguza na kuufanya uhuru uwe wa kiumbo zaidi kuliko
kuwa wa kimaadili na nguvu. Askofu anaendelea kusema, ‘ni kweli tunaweza kufanya
jambo baya dhidi ya wenzetu kwa uhuru huu tulionao. Lakini je, ndivyo
tunavyopaswa kufanya?’ Unachopaswa kufanya ni kitu gani? ‘Ni kile ambacho
kinamaanisha lengo, dhumuni, maadili na sheria ya mwenyezi Mungu. Katika mambo
ya kiroho niko huru kama ninaheshimu na kutii sheria za mwenyezi Mungu.’
Jibu la kijana huenda ni jibu la vijana wengi ambao hawaji kanisani huku wakiwa mtaani
wakifanya shughuli zao. Tatizo ni kubwa zaidi kwa vijana wa kiume kuliko kwa wanawake
licha kwamba sensa zote nchini zinaonesha kuwa idadi kubwa ya wanawake ni jambo la
kawaida kabisa kutokea kwenye nchi za Kiafrika. Biashara ndogondogo za kutembeza kwa
miguu, boda boda, bajaji, huba, baiskeli, bolt, haisi na taxi; na kwa nyongeza zaidi, mazoezi
ya viungo viwanjani zimekuwa ndizo shughuli muhimu zaidi kuliko kuanza siku ya Bwana

kwa sala. Mitandao ndiyo sasa inazidi kuathiri kundi kubwa la vijana. Je, kwa sasa jukumu
la kuwarudisha vijana kwenye mstari wa kimaadili ni la nani hasa? Sambamba na uhuru,
kijana lazima ajitambue kuwa ana hadhi ya namna gani hapa duniani. Mwandishi Eugene
Kamau anasema, ‘Kujitambua ni uwezo wa mtu kuwa na maarifa ya juu ya tabia na
hisia zake. Ni maarifa aliyonayo mtu juu ya hisia za za mwili wake, namna ya
kupambana na hisia hizo, vitu anavyopendelea, tabia na fikara zilizopo ndani yake.’
Kwa maneno mengine, kujitambua ni uwezo wa kuweza kutawala maisha kwa njia iliyo
sahihi.
Ni wajibu wa wazazi au walezi, walimu shuleni, viongozi wa kiroho au dini, viongozi wa
serikali, wanasanaa na jamii kwa namna ya pekee kila mmoja kwa nafasi yake afanye juu
chini kuwezesha utoaji wa malezi stahiki yenye kumpa kijana Uwezo, fursa na motisha
katika malezi na ukuaji.

Je, Walezi wafanye nini kunusuru hali hii? Soma toleo lijalo!
Pd. Dkt. Stephen NYAKUMOSA Kadilo

Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi ya Afya na Tiba shirikishi cha Mtakatifu Francisko

(SFUCHAS) – Ifakara.