BABA Mtakatifu Francisko, ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro nchini Tanzania, Telesphor Mkude la kung’atuka madarakani. 

 

Papa Francisko ameridhia ombi hilo la Askofu Mkude, jana Jumatano tarehe 30 Desemba 2020, baada ya kuwaongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu kama Padre kwa miaka 48 hadi kufikia mwaka 2020 na miaka 32 kama Askofu Jimbo.

Tangu tarehe 12 Februari 2019, majukumu yote ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu jimbo hilo la Morogoro yamekuwa yakisimamiwa na Monsinyo Lazarus Vitalis Msimbe aliyeteulia na Papa Francisko ili kutoa nafasi kwa Askofu Mkude kushughulikia zaidi afya yake.

Askofu Mkude alizaliwa tarehe 30 Novemba 1945 eneo la Pinde, wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.

Baada ya safari yake ya kimasomo, tarehe 16 Julai 1972, Mkude alipewa daraja takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Morogoro.

Tarehe 18 Januari 1988, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteua kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga na kuwekwa wakfu tarehe 26 Aprili 1988 na Hayati Kardinali Laurean Rugambwa, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Ilipogota tarehe 5 Aprili 1993, tena Mtakatifu Yohane Paulo II akamteua kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro hadi Jumatano ya tarehe 30 Desemba 2020, Baba Mtakatifu Francisko aliporidhia ombi la kung’atuka kwake kutoka madarakani.