Teknolojia ya mawasiliano ilianza kubadillika haraka tangu karne ya 15 ilipogunduliwa mitambo ya kuchapa. Katika karne ya 19, redio iligunduliwa na baadaye televisheni na satellite katika miaka ya 1956. Mabadiliko yalikuwepo lakini jambo jipya ni kuwa mabadiliko ya sasa ni tofauti sana na huko nyuma. Kwa upande wa kanisa, kuna hatari kanisa kuachwa nje au kurudi nyuma sana kama uangalifu wenye umakini hautachukuliwa mapema. Gutenbert alipogundua mitambo ya kuchapa, biblia ilikuwa kitabu cha kwanza kuchapwa. Kanisa lilitumia teknolojia ya kuchapa pamoja na redio katika kueneza neno la Mungu. Huu ni upande wa matumizi mazuri sana ya utandawazi.

 

Katika karne hii ya habari na teknolojia, mabadiliko yanatokea kwa kasi kubwa lakini nionavyo mimi, ushiriki wa kanisa ni mdogo au basi kasi yake haitosherezi. Vijana hawatumii tena muda kanisani kama zamani. Sasa vijana wanatumia muda wao mwingi kwenye intaneti ambako wanawasiliana na watu wengi kutoka dunia nzima. Vijana tunao hapa lakini hawapo hapa. Swali ni hili: Je, tufanyeje?

 

 Mimi nimeamua kuwatafuta vijana waliko na ndicho kisa cha makala hii tunayoendelea nayo leo ikiwa ni toleo la sita. Basi leo tuangaze kwenye madhara ambayo vijana wamepata kwa kukumbatia zaidi mambo ya mtandaoni.

 

Athari za mitandao kwa afya ya akili na mwili wa mwanadamu: 

Kila kitu kikitumika kuzidi kawaida huleta madhara. Madhara ya kuzidisha matumizi ya simu hasa katika afya ya akili ni kama ifuatavyo:

 

 

  • Husababisha msongo wa mawazo (Stress/Distress disorder):

 

Vyanzo vya msongo kupitia simu ni Pamoja na mtu kuwa na wasiwasi kuhusu jinsia yake hasa baada ya kuangalia picha mbovu kwenye simu- sexual identity crisis. Kutukanwa katika mitandao (Cyberbullying), kupotea kwa mawasiliano ghafla na mtu mliyezoeana, kukosa muda wa kupumzika kutokana na matumizi mengi ya simu (insomnia), kuona matukio ya kinyama katika mitandao ambayo hushtusha na kuacha jeraha la kudumu akilini (Post-Traumatic Stress disorder).

 

  • Husababisha ugonjwa wa kupungukiwa na umakini (Attention Deficit Hyperactive Disorder-ADHD) na tatizo la kujirudiarudia kwa taswira za matukio ya kwenye simu (Obsessive-Compulsive Disorder).

Mtu aliyetawaliwa na matumizi ya simu hawezi kutulia na kufanya kitu kwa utulivu na umakini. Huwa na mahangaiko ya kutaka kujua nini kinaendelea katika simu yake hata kama hayupo nayo (Offline Distress Online Response-ODDOR). Wakati mwingine, mtumiaji wa simu huwa na kumbukizi za mara kwa mara za kile alichokisikia ama kukiona katika simu kiasi kwamba hawezi kutulia bila kuwaza. Baada ya kukosa utulivu na umakini, mtu anaweza kupata tatizo la usahaulifu na kumfanya ashindwe kukumbuka mambo ambayo kimsingi aliye makini hapaswi kusahau, mfano kukokotoa mahesabu madogo, kumbukumbu za tarehe ya kuzaliwa, harusi, ubatizo na kadhalika.

 

 

  • Husababisha tatizo la kunyong’onyea (Unyongofu) na wasiwasi (Depression and Anxiety):

 

Unyongofu ni tatizo la mtu kukosa amani na utulivu wa nafsi bila sababu za msingi. Wasiwasi ni tatizo la kushindwa kujiamini, hivyo kuwa na mawenge ama hofu katika masuala ya kawaida katika Maisha. Dalili za wagonjwa wa unyongofu na wasiwasi zitokanazo na matumizi ya simu ni pamoja na: Kushindwa kuishi bila simu fulani, kukumbatia marafiki wa mitandaoni (Para-social interaction) kuliko wale walio naye karibu, kuongea mambo ya wengine pasipo na uwezo wa kujitetea, mkato wa tamaa, kuwa na mawazo mengi lakini yasiyo na sababu maalumu, kushuka kwa kiwango cha sukari mwilini, kuumwa ovyo ovyo, kukosa usingizi mzuri na kupendelea kukaa pweke.

 

 

  • Husababisha tatizo la kupoteza uelewa sawia wa mazingira na vitu katika uhalisia wake (Reality Apprehension Disorder).

 

Kuna baadhi ya watu huamini uhalisia wa wanachokiona katika simu zao. Ubongo wao hurekodi na kuhifadhi yote wanayoyatazama na kuyasikia. Inapofika hatua ya kutenda yale wanayoyaona kwenye simu ‘nje ya simu’ basi ubongo hukataa maana ulishazoea kile kinachoonekana kwenye simu kama ndio halisi. Mfano wa hali hii ni pale mtu anapochagua picha za watu kwa kuwa amevutiwa nao lakini ikitokea akaonana nao ana kwa ana katika uhalisia, hushindwa kulinganisha!

 

Madhara mengine ni Pamoja na woga wa kuongea mbele za watu (Social phobia), Paniki (Panic Disorder) Matatizo ya kula (Eating Disorders-Anorexia nervosa). Kwa nyongeza, mimi binafsi nakubaliana na Pd.Titus Amigu anavyoona jambo hili kwa umakini kwenye kitabu chenye anuani, Madhara ya utandawazi katika familia. Padre anasema hivi:

 

Kuna vijana wa kike na kiume ambao wameiga baadhi ya mambo kwenye mitandao ya kijamii ambayo siyo sahihi. Kuna akina dada wanaotumia madawa na nyenzo nyinginezo za kuzuia mimba, na ikitokea wamepata mimba huitoa. Baadaye wanapata magonjwa ya kansa na wengine wanakosa watoto kabisa. Mwishowe, kutokana na kunyong’onyea na kukosa amani, hasa wanapokumbuka jinsi walivyofurahia maisha kipumbavu; hupata ugonjwa ambao kwa kitaalamu unaitwa Post-Traumatic Stress Disorder (PTSD) na Obsessive-Compulsive Disorder (OCD) ambao huwafanya wakimbilie kwenye ‘Maombi’ wakidhani wana mapepo.

Pd. Dkt. Stephen NYAKUMOSA Kadilo

Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi ya Afya na Tiba Shirikishi cha Mt. Francisko (SFUCHAS)-Ifakara.