‘’Ukijishusha thamani na ulimwengu utakushusha thamani”.
– Ophra Winney
Kujikubali ulivyo ni kujiponya. Bila wewe mwenyewe kujikubali, hakuna atayekukubali ama kukubali unachokifanya. Mwenyezi Mungu anakupenda sana. Alikuumba kwa sura na mfano wake. Hakukuumba kwa bahati mbaya. Usijikatae. Usijidharau. Usijione kama mtu wa bahati mbaya. Hakuna mtu anayeweza kuwa kama wewe hapa duniani. Wewe ni wa tofouti. Una kitu ambacho watu wengine hawana. Wewe ni wewe. Miongoni mwa watu ambao dunia inasubiri kuona mafanikio yao ni ‘Wewe’. Dunia inasubiri kuongozwa na mawazo yako. Kuna watu wanasubiri kuajiriwa na kampuni yako. Ukikata tamaa utakuwa umeua ndoto za watu wengi sana. Amini kila unalotaka kupata utalipata hata kama ni kwa kuchelewa. Wewe ni mshindi sio mshindwa.
Mwanamitindo Ophra Winney anasema, ‘’Ukijishusha thamani na ulimwengu utakushusha thamani”. Tafadhari nakuomba usijishushe thamani. Jithamini. Wewe ni wa thamani sana katika dunia hii. Wewe ni wewe, hakuna anayeweza kuliziba pengo lako. Mwaka 2012 gazeti la Kiongozi linalomilikiwa na Kanisa Katoliki nchini Tanzania lilichapisha makala yangu iliyokuwa inasema: ‘’Krismas bila Kristu sio Krismas”. Msomaji mmoja alinitumia ujumbe mfupi kupitia simu yangu ya kiganjani. Ujumbe wake ulisomeka:
Ndugu yangu William Bhoke, hii ni Krismas yangu ya 50, kwa maana hiyo nina miaka 50. Ninachosikitika ni kwamba sina hata mtoto wa kusingiziwa, sina uwanja wala nyumba. Niliajiriwa miaka 12 iliyopita ninaelekea kustaafu kazi lakini maisha yangu hayana nyuma wala mbele. Nimekata tamaa kabisa. Nimejikataa na kukataliwa. Siamini kama nitafanikiwa tena. Ninaomba unipe muongozo mpya wa maisha.
Mwandishi wa vitabu, Mark Kay Ash anasema, “Mungu hakuwa na muda wa kuumba mtu ambaye hana maana, bali mtu wa maana tu’’. Wewe ni mtu wa maana sana. Una sababu za kuzaliwa. Kataa kujikataa. Kujikataa ni kuhisi kuwa wewe si mtu muhimu. Ukweli ni kwamba, wewe ni mtu mhimu sana katika sayari hii ya dunia. Mwenyezi Mungu hakukuumba kwa bahati mbaya. Kwa Mungu hakuna bahati mbaya. Kwa Mungu hakuna bahati na-sibu. Kwa Mungu kila kitu ni uhakika. Mfalme Daudi alimtukuza Mungu kwa maneno haya:
“Ninakusifu (Mungu) kwa kuwa nimeumbwa kwa namna ya ajabu ya kutisha’’ (Zab139:14).
Usimwaibishe Mungu kwa kuishi maisha ya kujikataa. Kujikataa ni kumwaibisha Mungu aliyekuumba kwa sura na mfano wake [Rejea Mwanzo 1:26-27]. Kujikataa ni kumwambia Mungu: ‘Hukuniumba vizuri’. Kujikataa ni kuzikataa baraka za Mungu katika maisha yako. Kuanzia leo kataa kujikataa. Kataa kuwa maskini. Kataa kuwa ombaomba. Kataa kuwa mlevi. Kataa kuwa mzinzi. Kataa kuwa mchepuko. Kataa kuwa muongo. Kataa kuwa mnafiki. Kataa kuwa na kiburi. Kataa kuwa na majivuno. Kataa kuwa na hasira. Kataa kuwa mfano mbaya katika jamii. Usijikatae. Wewe ni mtoto wa Mungu.
Kujikataa ni kukubali kushindwa kufanikiwa. Unapojidharau unakuwa adui wa mafanikio yako. Iko hivi: Kutokuwa na mipango mikubwa katika maisha yako ni kujikataa. Kutokujistahi ni kujikataa. Kutojipenda ni kujikataa. Kutokujiamini ni kujikataa. Kutokujitakia mema ni kujikataa. Kuishi na chuki moyoni mwako ni kujikataa. Kutokusamehe ni kujikataa. Kuwawazia watu wengine mabaya ni kujikataa. Leo andika upya historia maisha yako. Kuanzia leo jiwekee agano la kufanikiwa. Jikubali kuanzia leo na siku zote zijazo. Jipende kuanzia leo na siku zote zijazo. Jiamini kuanzia leo na siku zote zijazo. Jisamehe kuanzia leo na siku zote zijazo. Jiheshimu kuanzia leo na siku zote zijazo.
Mwanasaikolojia wa Uswisi, Carl Jung anasema, ‘’Kujua giza lako mwenyewe ni mbinu bora ya kukabiliana na giza la watu wengine’’. Kila mtu ni kiongozi wa maisha yake na maisha ya wengine. Usipojiongoza wewe mwenyewe, huwezi kuwaongoza wengine. Kesho inakuja. Usipojiandaa vizuri leo, kesho yako itakuwa na lawama. Fanya kazi kwa bidii ili kesho yako iwe njema. Lawama ni mtaji wa walioshindwa kufanikiwa. Acha kulalamika. Jiondoe kwenye kundi la watu wanaolalamika kwa kila jambo. Waandishi wa kitabu cha The Power of No, James Altucher na Claudia Altucher wanasema, ‘’Kulalamika ni kukimbiza fursa. Unapoacha kulalamika unaanza kuona kila hali ya fursa. Unafungua mlango wa kupata mawazo mapya’’. Hakuna aliyefanikiwa kwa kulalamika. Usilalamike.
Mwandishi T. L. Osbon anasema, “Ukiacha kujifunza unaanza kufa’’. Tafuta wazo jipya kila siku. Kumbuka: Usipotumia nguvu nyingi kuwaza mawazo yatakayoibadili dunia, ni lazima utaajiriwa na watu waliotumia nguvu nyingi kuwaza mawazo yaliyoibadili dunia. Mwandishi wa vitabu vya Kiroho, Tony Evans anasema, “Watu wengi wanatumia muda wao mwingi kuishi maisha ya watu wengine’’. Acha kupoteza muda wako wa thamani kwa kuiga kuishi maiha ya mtu fulani. Ishi maisha yako.
Tembea kwenye kusudi la Mungu. Mungu ana mpango na wewe. Anataka jambo kubwa litokee kupitia wewe. Anataka atukuzwe kupitia wewe. Wewe ni mpakwa mafuta wa Bwana. Una upako wa ajabu. Uwepo wako duniani sio ajali ya kibaiolojia, bila kujali mazingira yaliyozunguka kuzaliwa kwako. Uko hai kwa sababu ya Umwilishwaji wa Ki-Mungu uliopitia kwa wazazi wako. Kutungwa kwako mimba na kuzaliwa kwako ni uthibitisho kwamba, Mungu ana mpango na wewe. Usijutie kuwa miongoni mwa wanafamilia wa kibinadamu wanaoishi katika sayari hii ya dunia. Jambo moja na la mhimu ambalo kila mtu anapaswa kulifahamu ni kwamba; Mungu hawezi kuruhusu chochote kije katika maisha yako ambacho hutaweza kukabiliana nacho. Kumbuka: Pale unaposema, hapa nimefika mwisho, Mungu anasema, ‘Huu ni mwanzo mpya’. Mtume Paulo ameandika hivi:
‘’Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya mwanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili’’ [1Wakorintho 10:13]
Kumwamini Mwenyezi Mungu wakati wa raha ni rahisi mno kuliko kumwamini wakati wa shida, na utahitaji imani kuendelea kumwamini wakati wa dhiki. Vipindi vigumu katika maisha yetu hutokea kwa kila mmoja wetu. Kuamini ya kwamba Mungu ana makusudi ya lazima kukuondolea vikwazo katika maisha yako ni vigumu sana wakati mwingine, lakini imani ndicho kitu cha muhimu zaidi unachotakiwa kuwa nacho katika kipindi hiki ambacho dunia imekata tamaa. Amani ya Mungu, ambayo huzidi hekima na maarifa yote ya kibinadamu, ni kuliamini neno la Mungu kwamba ni la kweli. Bila imani hutaweza kumfurahisha Mungu. Imani ni ufunguo wa nguvu, uwezo na neema ambavyo Mungu ametupangia. Kwa ufupi, Mungu ni mkubwa kuliko wewe na matatizo yako. Jikubali.
KOSA KUBWA NI KURUDIA KOSA
‘’Kama hufanyi makosa, hufanyi chochote katika maisha’’.
– John Wooden
Kosa ni alama ya uhai. Kama hauko hai huwezi kutenda kosa. Mwanamichezo wa Marekani John Wooden anasema, ‘’Kama hufanyi makosa, hufanyi chochote katika maisha’’. Huwezi kuishi kwa muda mrefu bila kutenda kosa. Mwanadamu ni tajiri wa makosa. Tunajikuta kila mara katika makosa na dhambi. Tunamkosea Mungu na wenzetu. Tena, kuna wakati tunamkosea Mungu na wenzetu kwa bahati mbaya au kwa kukusudia. Katika sura hii nitakufundisha umhimu wa kukiri kosa pale unapokuwa umetenda kosa. Nitakufundisha pia namna ya kulitazama kosa kama fursa ya kujifunza jambo jipya. Katika roho ya ukimya na tafakuri mwanana, ninakualika usafiri pamoja nami katika makala hii inayolenga kuyaangazia maisha yetu.
Kosa kubwa ni kudhamiria kutenda kosa. Kosa la kimakusudi ni kosa kubwa. Ni kosa ambalo linakugharimu. Usikusudie kutenda kosa kwa lengo la kumkomoa mtu ama kumshushia heshima yake na utu wake, kinyume chake utakuwa wewe ndiye mhanga wa kosa ulilokusudia mwenyewe kulitenda.
Jifunze jambo jipya kila unapokuwa umetenda kosa. Katika safari ya mafanikio, kosa ni fursa ya kujifunza mbinu mpya ya kufanikiwa. Huwezi kufanikiwa kwa kuyaficha makosa yako. Huwezi kuwa mtu mwema kwa kuyaficha makosa yako. Neno la Mungu linasema, ‘’Afichaye makosa yake hatafanikiwa; lakini anayeyaungama na kuyaacha atapata rehema’’ [Mith 28:13].
Kila kosa lina jambo la kujifunza ndani yake. Unapotenda kosa, jiulize kwa nini umetenda kosa. Je, umetenda kosa kwa kudhamiria au ni kwa bahati mbaya? Je, umejifunza nini kutokana na kosa ulilolitenda? Je, utarudia kulitenda kosa hilohilo? Kiri kosa lako halafu omba msamaha kwa kosa ulilolitenda. Upotendewa kosa, jiulize kwa nini umetendewa kosa. Huwezi kutendewa kosa pasipo sababu. Sababu ya kutendewa kosa inaweza kuwa ya kukusudi na inaweza pia isiwe ya kukusudia. Jiulize; Je, hili kosa nililotendewa nimetendewa kwa bahati mbaya au ni kwa makusudi maalumu? Je, aliyenitendea kosa alikuwa katika hali gani na katika mazingira gani? Je, kuna faida yoyote ambayo nitaipata endapo nitamchukia huyu aliyenitendea hili kosa? Msamehe kwa moyo wa dhati aliyekukosea. Kosa ni ujumbe kuwa unafanya au umefanyiwa kitu fulani.
Mtoa hotuba wa Marekani, Roger Von Oech alipata kuandika hivi, ‘’Ukifanya kosa, litumie kama njia ya kuvukia kwenda kwenye wazo jipya ambalo usingeligundua kama pasingekuwepo na kosa’’. Yawezekana historia ya maisha yako inakukatisha tamaa. Usikate tamaa. Nisikilize kwa umakini hapa. Tunaweza kujifunza mbinu bora za kutoshindwa tena kutokana na makosa yetu ya awali na kufanya vizuri pale tuliposhindwa. Jambo hilo linawezekana.
Hatuwezi kufanya vizuri pale tuliposhindwa awali ikiwa tunapendelea kuhalalisha makosa yetu. Tunapokiri makosa yetu na kuomba msamaha, tunajenga mazingira ya amani ndani ya mawazo yetu. Hebu akili zetu zipewe nafasi na kazi ya kutafakari mema, ndipo mioyo yetu itajazwa amani. Sifa kubwa ya maskini wa kiroho na kiuchumi ni lawama. Unapotenda kosa, usitangulize lawama. Weka lawama pembeni. Kiri kwanza kosa lako. Kosa halitatuliwi kwa kulalamika. Kosa halitatuliwi kwa kujilaumu au kwa kuwalaumu wengine.
Maisha ni mfano. Maisha ya watu wengine ni mfano kwako. Maisha yako ni mfano kwa watu wengine. Mwandishi Gilbert West anasema, ‘’Mfano ni kitabu ambacho watu wote wanaweza kusoma’’. Jifunze kutokana na makosa ya watu wengine. Mtu mwenye busara makosa ya wengine, kwake ni shule. Anajifunza somo fulani. Kosa kubwa ni kuyafurahia makosa ya wengine. Makosa ya wengine yasigeuke kuwa furaha kwako bali yageuke kuwa funzo kwako.
Jifunze kuwa mkweli na kuupenda ukweli katika maisha yako. Mwalimu Nyerere alisema, ‘’Ukweli ni ukweli hata kama hakuna mtu anayesema ukweli. Uongo ni uongo hata kama watu wote watasema uongo’’. Uongo unaponya kwa muda mfupi lakini unaumiza kwa muda mrefu. Unapotenda kosa la aina yoyote, kubali ukweli uweke bayana uhalisia la kosa ulilolitenda. Kubali ukweli uwe mwalimu wa maisha yako. Kubali ukweli ukupe amani ya moyoni. Mwandishi wa vitabu wa Uingereza George Orwell alipata kuandika; ‘’Katika dunia yetu hii iliyojaa ulaghai, utapeli na udanganyifu tendo la kusema ukweli linachukuliwa kama la kimapinduzi, lakini ukweli ndio unaotakiwa’’.
Uongo unapotea, lakini ukweli unaishi milele. Mwanaharakati Clarence W. Hail alipata kusema, “Unaweza kuuweka ukweli kaburini lakini ukweli hauwezi kukaa kaburini”. Wayahudi walipomuua Yesu Kristo walimweka kaburini. Walifikiri wameuzika ukweli. Walifikiri wamemaliza kazi, lakini ukweli ni kwamba Yesu Kristo hakukaa kaburini. Alifufuka. Ukweli wa Yesu Kristo kufufuka ulishinda. Unapotenda kosa, usiliweke kaburini. Ukilificha kosa lako kaburini, ukweli utalifichua. Methali ya Kifaransa inasema, “Watu binafsi watakufa lakini ukweli ni wa milele”. Ismail Haniyeh alipata kusema, ‘’Baadhi ya watu hudhani kuwa ukweli unaweza kufichwa kwa kuuzuia kidogo au kuupamba lakini kadiri muda unavyozidi kwenda kilicho cha kweli hudhihirishwaa na uongo kutoweka’’. Kukiri kosa ni kujiponya kiroho na kimwili.