Kitabia, hakuna jambo linalokinai kiasi cha kuamua kuliacha bila kuwa na jambo jingine ambalo linachukua nafasi ya lile lililoachwa. Kwa lugha nyingine, bandika bandua ndiyo mtindo wa kila siku kitabia. Kama huu ndio ukweli wa mambo, basi kijana ambaye hayuko kanisani leo ana kitu anachokifanya badala yake. Kwanza tuangaze kwa ufasaha zaidi juu ya matumizi ya mitandao ya kijamii ambako naamini kijana kaweka nguvu yake kubwa kwa muda mwingi zaidi kuliko mambo ya kiimani halafu baadaye tutauangalia utepetevu wa imani yake tukikazia macho mwongozo wa kidini kutoka nyumbani, shuleni na jamii kwa ujumla.
Kutawaliwa na mitandao ya kijamii (Addiction to social media):
Baadhi ya vijana wameshatawaliwa na matumizi ya mitandao ya kijamii kiasi kwamba hawawezi kutulia na kufanya jambo bila kuangalia jambo jipya (updates) kwenye mitandao husika. Kitabibu inafahamika kuwa mitandao ya kijamii ina uwezo wa kuamsha homoni za dopamine na oxytocin ambazo hutoa hitaji la raha. Katika hali hii kijana anahaha kuwa na raha kwa kuona anachotaka kuona bila kupoteza muda. Hali hii si kitu kingine bali ni ulevi wa namna yake. Zifuatazo ni dalili za kuathiriwa na mitandao ya kijamii:
- Kushindwa kuendelea na Maisha bila kuwa na simu
- Kuongeza muda wa kutumia simu kila kukicha.
- Kutumia simu kama njia ya kuondokana na msongo wa mawazo au upweke.
- Kukosa utulivu na kuwa na hasira unapokosa simu yako, inapokuwa bila chaji au kukosa salio.
- Unapoona huna mahusiano ya dhati kwa watu; hasa mnapokuwa pamoja halafu wewe unajishughulisha zaidi na simu.
- Unapoona unatumia simu mara nyingi lakini faida unayoipata hujui, yaani unajiona wewe na simu ni kama mmeoana bila sababu.
Kabla ya kuzama sana kuangalia athari za mitandao kwenye maisha ya kijana, hebu tuiangalie kwa ufupi na kwa jumla historia ya mitandao hii ilivyoanza kisha tuamue kama tuko sahihi kuiatamia zaidi bila kumjali aliyetujalia kuyagundua haya yanayotusumbua.
Katika mambo yote tukumbuke kuwa uvumbuzi wa mambo yote katika sayansi na teknolojia, Mungu asiwekwe kando hata mara moja kwani mambo haya tunayafanya katika asilimia ndogo sana kati ya mambo mengi ambayo Mungu katufunulia ili tuyagundue. Padre Titus Amigu kwenye Dibaji ya kitabu changu chenye anuani Mateso na Kifo Cha Yesu Kristo: Mtazamo wa Kibiblia, Kihistoria na Kisayansi ameandika hivi:
Lakini, mwanadamu hata awe msomi namna gani, hana cha kujivunia. Mwanadamu hajawaji kuunda chochote kipya isipokuwa kuyachanganua na kuyachangachanga mambo aliyoyaratibu Mungu kwa hekima yake kuu. Kwa taarifa yetu, Biblia inasema na sayansi inakiri kwamba hadi sasa kilichovumbuliwa na mwanadamu ni 4% tu ya mambo aliyoyaweka Mungu ulimwenguni. Imeandikwa, ‘Maajabu mengi makuu kuliko haya yamefichika maana tumeziona tu kazi zake chache. Maana Bwana amefanya vitu vyote, akawapa heshima wale wamchao’ (YbS 43:32-33)
Kama vijana wamepungua kanisani kwa sababu ya kumdharau Mungu kumbe mambo yaliyopo ni asilimia 4% tu, je tutakapogundua mpaka kufikia walau 50% mambo yatakuwaje? Bwana wetu Yesu Kristo alihoji: Walakini atakapokuja mwana wa Adamu, Je, ataiona imani duniani? (Lk 18:8)
Mwandishi Mark Link, SJ anasimulia kwamba, mnamo mwaka 1842, bunge la Marekani lilicheka sana wakati Samuel Morse alipoeleza wazo lake la kutuma ujumbe kupitia kwenye waya. Mnamo mwaka 1878, bunge la Uingereza lilicheka sana wakati Thomas Edison alipoeleza wazo lake la kuunda mwanga kwenye balbu za chupa. Hali kadhalika, mnamo mwaka 1908, mzungumzaji wa kampuni ya J.P. Morgan alicheka wakati Bill Durant aliposema kwamba, ‘muda utafika ambapo magari nusu millioni yatakuwa yanatembea kwenye barabara nchini kote.’
Ni kawaida yetu kuona kwamba kitu ambacho kinazidi uwezo wa fikra ya kibinadamu kukishangaa ama kukichekelea! Hiki ndicho kisa kwamba tarehe 11 Aprili, 1953 siku ya alhamisi usiku, gazeti la The Tacoma News Tribune Washington D.C lilipotangaza kuwa ‘Katika siku za usoni, hakuna atakayekwepa umiliki wa simu ya mkononi.’
Mark R. Sullivan Rais na Mkurugenzi wa kampuni ya Pacific Telephone and telegraph huko California naye alisema hivi:
Namna mwonekano wa simu ijayo utakavyokuwa kwa hakika ni jambo la kufikirika. Huu hapa ni unabii wangu:
Katika hatua za mwisho za maendeleo yake, simu itabebwa na mtu yeyote, labda kama leo tunavyobeba saa. Huenda simu haitahitaji kasha ama kiambatanisho chochote, na ninafikiri kuwa watumiaji watakuwa na uwezo wa kuonana wao kwa wao huku wakitembea. Lakini ni nani anajua kuwa simu itakavyokuwa? Simu itatafsiri ujumbe kutoka lugha moja hadi nyingine.
Misemo wa Kiswahili ni bayana sana juu ya jambo hili: Hayawi hayawi huwa na Lisemwalo lipo na kama halipo laja. Mambo yote yaliyotabiriwa na kusemwa mapema juu yake, sasa tunayo mikononi mwetu na katika mazingira yetu. Sasa tuna aina mbalimbali za simu, saa za simu na aina nyingi za kompyuta. Je, mambo haya yana changamoto zozote?
Ni kweli ulimwengu umekuwa Kijiji kimoja lakini ni Kijiji chenye tofauti nyingi sana. Ralph Turner kwenye kitabu chake I am just a Sukuma ndiyo kusema ‘Mimi ni msukuma’, ingawa yeye alikuwa mzungu anauliza: Je, katika ulimwengu huu wa utandawazi; sisi tuna mchango wowote au sisi tunakokotwa tu?
Padre Charles W. Bundu ambaye kwa sasa ni Chaplain kwenye Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino kilichoko Mwanza -Tanzania, alipokuwa anahutubia Mapadre kwenye Kongamano la mwaka wa Mapadre huko Dodoma Agosti 2010 alionya kwamba, ‘Tusipoangalia utandawazi utaturudisha kwenye utumwa’ aliendelea kusema, ‘Prof. Ally Mazrui alisema hivi kwa Waamerika weusi:
Sahau unakotoka, kumbuka unavyoonekana
Sahau asili yako, kumbuka rangi ya ngozi yako
Sahau kwamba u Mwafrika, kumbuka kuwa u mweusi.