Vijana wengi hawazingatii Maisha ya kiroho/kidini. Wengi wao humezwa katika starehe, huona ulimwengu ni kama sehemu ya kufurahia maisha tu na sio kupambana na changamoto zake. Hapa ndipo idadi ya vijana wanaohudhuria kanisani inakuwa ni ndogo na watu wazima na wazee ndio wamejaa kanisani.
Ni nadra sana kumkuta kijana anasali au akishiriki masuala mengineyo ya kiroho.
Shida hii iko nchi za ugaibuni ingawa hata hapa kwetu hali hii imeshaingia tena inashamiri kwa kasi kubwa kama upo wa kimbunga.  Dalili mojawapo ya uhakika wa jambo hili ni idadi kubwa ya vijana kwenye viwanja vya mpira ukilinganisha na idadi yao ndogo makanisani!
Idadi kubwa ya vijana kwenye klabu za muziki kuliko kanisani! Idadi kubwa ya vijana wakiwa uwanjani wakifanya mazoezi ya mpira wakati misa na ibada za kwanza zinapoanza asubuhi!
Asilimia kubwa ya vijana hupuuzia masuala ya ibada au hata wakienda, nafsi zao zimegawanyika; kidogo sala, kidogo mahusiano, kidogo maisha, kidogo starehe, kidogo kuchezea simu, mara kutafuna jojo na kadhalika. Mtu akiambiwa zima simu yako ufungue roho yako mwitikio wake ni hasi na fitinishi – Hii ni dalili mbaya ingawa hapa ndipo tulipo kwa sasa.
Vijana wengi pote duniani, ndio wahanga wakubwa wa matumizi ya vilevi kama sigara, pombe, madawa ya kulevya na vinginevyo kama tiba ya msongo wa mawazo (stress).
Kisaikolojia msongo wa mawazo unaathiri utendaji wa kawaida wa kijana katika kujitawala. Dalili zake ni Pamoja na kulegea au kukosa nguvu (Kimwili); kujisikia vibaya, kuwa na wasiwasi (Kihisia); kujihisi kutotaka kufanya chochote, kuboreka (Kitabia) na kukosa utulivu kifikra, kushindwa kujitambua (Kiakili).
Msongo wa mawazo usipodhibitiwa vizuri, husababisha kujichukia mwenyewe, kujitenga na wengine, kujiona hufai kitu na hivyo kuwa na sonona (depression). Wengine hujichukia kiasi cha kutaka kujidhuru. Msongo wa mawazo kwa vijana walio wengi unatokana na haya yafuatayo:
Changamoto za kimahusiano na kimawasiliano katika simu; na walezi, walimu, marafiki, mpenzi n.k
Changamoto za kimasomo; kazi za darasani, ufaulu hafifu n.kÂ
Kujikataa (kujilinganisha) kiumbo, kifikra na kihisia.
Changamoto za misukumo ya makundi (peer pressures).
Kutengwa na marafiki, wazazi kutengana, kuhamisha makazi ama shule.
Vifo vya watu wa karibu, uwepo wa wagonjwa katika familia na kuanza majukumu ya kimalezi mapema.
Tamaa ya mali za haraka, kutokuwa na ajira maalumu, majukumu mengi na mabadiliko ya mwili.
Vijana katika kipindi hiki ndipo wanahitaji maongozi na malezi bora kutoka kwa wazazi, walimu na viongozi wa dini. Ndicho kipindi wanapohitaji kupewa Habari muhimu za kimaisha.
Kuna ukinzanifu wa mambo muhimu ya maisha kutoka kwa wazazi, walimu na viongozi wa kanisa dhidi ya mambo muhimu ya maisha kutoka kwa misukumo ya kimakundi (peer pressures) kutoka kwa vijana wenzao na kutoka mitandaoni. Kipi kinatakiwa kufuatwa ili kijana apate malezi bora?
Ufugaji wa kuku unaweza kutupatia ufumbuzi wa namna ya kufanya jukumu hili. Kuku wa kisasa wana ufugaji ambao unahitaji uangalizi wa kina sana ili kuwatunza kuku hawa.
Kuku wa kienyeji wana mazoea ya kujitafutia chakula chao ingawa wasukuma wanamsemo yaani ‘Kuku mwenye vifaranga hamezi funza.’Â
Uangalizi wa kuku wa kienyeji ni mdogo sana ukilinganisha na kuku wa kisasa. Kijana anapojihoji na akajitafutia majibu ya kila swali analoji,matokeo yake makubwa ni kupotea kimaadili maana majibu yake mengi yanaongozwa na mihemko ya hali yake kimakuzi. Kumbe, kijana anapaswa kujitambua na kuwa msikivu kwa wakubwa ili apewe mwongozo.
Kuna mambo ambayo lazima yaongozwe na kuelekezwa na wakubwa ndipo vijana nao wayafanye. Maandiko Matakatifu yanatuelekeza kwamba: Siku ya ufufuko wa Bwana, Maria Magdalena alienda kaburini kungali giza bado akakuta jiwe la kaburi la Bwana limevingirishwa mbali na mwili wa Bwana haukuwemo kaburini.
Akishika njia kwenda kuwapasha wanafunzi wa Yesu juu ya habari hiyo, Petro na Yohane walikimbia kwenda kaburini.Yohane kwa vile alikuwa kijana, aliwahi kufika akabaki nje hakuingia kaburini kwani alimsubiri Mzee Petro ili aingie kwanza. Petro aliingia kaburini kwanza halafu Yohane naaye ndipo aliingia baadaye akaona na kuamini (Rejea Yoh 20:1-10).
Pd. Dkt. Stephen NYAKUMOSA Kadilo
Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi ya Afya na Tiba Shirikishi cha Mt. Francisko (SFUCHAS)-Ifakara.