Wanaume wengi wanakufa kwa magonjwa ya moyo kwa sababu toka wakiwa wadogo walikatazwa kuwa binadamu. Walilazimishwa na waligombezwa na walionywa kuwa hawaruhusiwi kuonyesha hisia zao.

Matokeo yake wanaishi kama “magogo” miaka yote toka wakiwa wadogo mpaka wazee wakiwa na machungu moyoni ambayo wameambiwa wakae nayo. Mwanaume halii.

 

Hata ukifiwa na baba yako au mama yako na wewe ni mwanaume bado watu hawataki ulie. Wanasema mwanaume halii. Hata ukiumwa kansa na unasikia maumivu makali bado wanasema mwanaume halii.

 

Na kwa sababu jamii haitaki mwanaume alie basi wanaume wanalia mioyoni mwao. Wengine wanajifungia chumbani wanalia kwa kujificha. Wamejaa vidonda, wamejaa makovu mioyoni mwao.

 

Lakini nani alisema mwanaume ni jiwe au ni roboti hana hisia? Hivyo ndivyo walivyoumbwa au ni mtazamo tu wa jamii? Nani alisema kulia ni ishara ya udhaifu? Nakumbuka wakati wa msiba wa Edward Moringe Sokoine, Rais Julius K. Nyerere alilia.

 

Nani anaweza kusema Rais Nyerere alikuwa dhaifu? Alipotoka jela, Mike Iron Tyson alilia. Nani anaweza kusema yeye ni mwamba kuliko Tyson?

 

Kutoa machozi na kulia ni sehemu ya kutibu moyo wako, ni sehemu ya kujenga nafsi yako, ni sehemu ya kutoa yaliyo moyoni mwako na ni sehemu ya kuwa mtu. Haijalishi ni mwanaume, mwanamke au mtoto kulia na kutoa machozi ni sehemu ya kuuchanulisha moyo wako unaotaka kusinyaa. Kulia kwa uchungu au furaha ni sawa kabisa.

 

Rafiki yangu Aubry Padmore ambaye anaishi Atlanta Georgia anasema “sioni aibu kulia hadharani. Nilipopoteza mwanangu wa kike nililia”.

Aubry mmoja wa “speakers” wakubwa kule Atlanta anasema hutakiwa kufikiria watu watasema nini. Mwenye kauli ya mwisho ni Mungu”. [God has the last say]. Kwanini unaona aibu kulia?

 

Haijalishi wewe ni mwanaume au mwanamke, haijalishi ni shida gani, hata kama umeachwa na mchumba wako “kulia ni sawa tu” It’s okay to cry.

 

Hata kama umepigwa makwenzi na mke wako kulia ni bora kuliko kumpiga ngumi moja ukamuua. Utafia jela!utaacha watoto wanahangaika.

 

Wanaume wengi wanalia kwa namna nyingine. Badala ya kulia wanaenda kunywa pombe baa, au kufanya uhuni au kunywa vidonge vya usingizi. Kaa chini ulie “my friend”. [sit down and cry]. Maisha ndio hayahaya.

 

Rafiki yangu mmoja alinifurahisha sana. Akasema nimetoka kulia. Nikamwambia kwa nini?Akasema nimepigwa makofi na wife.

 

Nikamwambia “you are my hero” Akasema usimwambie mtu. Nikamwambia sitakutaja jina. Huu ujumbe lazima ufike. Ungekuwa jela sasa hivi.

 

Unapoumizwa moyo wako lia tu! Kubwa zaidi mlilie Mungu wako. Mwaka jana nilialikwa kuzungumza kwenye kongamano la wanaume. Nikashangaa wamekuja wanaume wachache sana. Wengi wanaona aibu kuja kusema yanayowasibu. Lakini wale wachache waliokuwepo waliongea mambo mpaka nikashangaa.

 

Wengine wanapresha kwa sababu wana tezi dume na hawawezi kusema wanalia kimyakimya. Matokeo yake hawapati msaada.

 

Wengine wanapigwa makofi na wake zao wanalia moyoni na hawawezi kusema. Wengine wamegundua watoto si wao baada ya kuwa kwenye ndoa miaka 30. Lakini wameshaambiwa usilie kaa kimya wewe ni mwanaume.

 

Matokeo yake wanapata presha wanakufa. Nani anaongea na wanaume?

Nani anawaambia “it’s okay to cry?

Nani anawaambia unaweza ukasema ya moyoni mwako?

Kwanini unaruhusu baba yako afe kabla ya umri wake. Kwa nini usimuache alie?

Mbona akifa na wewe unalia?

Wewe unafurahi idadi ya “single mothers” inapoongezeka? Wasaidie wanaume waishi!

NA William Bhoke