Malezi ya kijana ni uangalizi wa karibu wa kijana kiakili, kiafya, kiroho, kitabia na hata kijamii. Nyuma kidogo kijana alilelewa na jamii nzima ila siku hizi kuna changamoto kidogo. Wanaohusika katika malezi ni wazazi nyumbani, walimu shuleni na vyuoni na viongozi wa kiroho.

Hawa wote ni walezi wa asili katika maisha ya kijana. Baadhi yao kulegea katika malezi kunakoonekana hivi leo kunasababisha ufa mkubwa kimaadili kiasi kwamba kijana hajitambui anakoelekea. Kwa mtindo huu, hasara ya taifa na jamii nzima kwa ujumla ni kuzalisha vijana wanaojilizaliza na kulalamika na wala si uzalendo na uwajibikaji. Pia kuna nyanja nyingine ambazo hutoa malezi kwa namna ya pekee sana. Hawa ni wasanii au wanasanaa na viongozi wa serikali

 

Wasanii wanatoa malezi kwa ujumbe unaotokana na mada zao za nyimbo, hadithi, tamthiliya na kadhalika; lakini pia viongozi wa serikali wanatoa malezi kwa sera wanazotunga ili kuruhusu au kukataza mambo fulani yafundishwe au yasifundishwe kwenye jamii ambamo raia wao wanaishi. Kuruhusu mambo yasiyo na maadili yafundishwe hadharani ni kuruhusu maadili yavurugwe. Hili si jambo jema hata kidogo! Katika maisha ya Kiroho, kama utawala utaruhusu mambo yasiyo na maadili yafundishwe hadharani ni dalili ya juu sana ya upagani kwenye eneo hilo. Hapa ndipo tulipo kwa sasa!

MAANA YA KIJANA:

Kijana ni mtu aliyeko kwenye rika la ujana.

Ujana ni kipindi cha Maisha kati ya utoto na utu-uzima. Umri kamili wa ujana unatofautiana. Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa (UN), kijana ni mtu yeyote aliye na umri kuanzia miaka 15-24, Jumuiya ya Madola (Common Wealth Organization), kijana ni mtu yeyote mwenye umri kuanzia miaka 15-29. Kadiri ya Sera ya taifa ya vijana hapa kwetuTanzania kijana ni mtu mwenye umri kati ya miaka 15-35. 

Kwa maana pana zaidi bila kuzingatia kigezo cha umri, ujana ni kipindi ambacho mtu hajafikia uzee baada ya kupita maisha ya utotoni.

Ujana unaelezwa kama kipindi cha ustawi wa mwili na wa nafsi tangu mwanzo wa ubalehe kwa ukomavu hadi mwanzoni mwa utu uzima. Kwa ufupi, ujana ni kipindi ambacho mwili unaingia katika ustawi mkamilifu, hali kadhalika na nafsi. Ni katika kipindi hiki cha ujana, viungo vyote vya mwili hutenda kazi kwa ukamilifu. Hali kadhalika, ni katika ujana fikra nzuri na mbovu hujitokeza kwa wingi, huku zikisukumwa na mihemko na misukumo ya mwili ya kila namna. Hii ni kutokana na mabadiliko ya homoni hivyo kijana hapa huhitaji miongozo ya kimaisha ili kumwongoza. Bila huu mwongozo ndio mwanzo wa kuharibika kwa kijana kitabia.

Kijana anapokuwa katika hali hii huhitaji kuelimishwa sawasawa ili aelewe mambo mbalimbali yanayomzunguka. Kwanini? Kwa sababu hali ya mabadiliko aliyonayo hajaizoea hivyo anahitaji kuelekezwa kwa kina la sivyo atachanganya mambo.

 

TABIA ZA UJANA:

Wengi wa vijana pote duniani wana tabia zinazolandana kwa namna moja ama nyingine. Haijalishi ni kijana wa Kiafrika, Ulaya, Amerika au Asia. Wengi wao huwa na tabia zifuatazo:

  • Wengi wa vijana hupenda kuwa pamoja ikilinganishwa na marika mengine. Hupenda kukaa katika makundi huku wakifurahi pamoja au kushirikishana mambo. Ni kipindi ambacho vijana huwekana wazi masuala nyeti ya kimaisha bila woga. Hujiamini kwa yale wanayoyafanya, yawe ni mazuri au mabaya.
  • Wengi wa vijana huwa na mitazamo mingi mikubwa kuhusu maisha yao ya baadaye. Hata kama wako kwenye anasa na starehe, bado wanapenda kuwazia sana kuhusu ubora wa maisha yao yajayo. Ni kipindi wivu wa maendeleo upo juu kwa kijana binafsi. Wengi wao hawana moyo wa kujiunga pamoja na kubuni miradi ya maendeleo itakayowainua katika maisha.
  • Wengi wa vijana pote duniani huwa katika harakati ngumu za kupambana na tamaa za mwili (Hayati Benjamin W. Mkapa alipenda kuiita hali hii ni michakato). Alitaja neno hili wakati akitoa hotuba yenye kueleza hali halisi wakati alipokuwa anasoma kwenye Chuo kikuu cha Makerere nchini Uganda akingali bado kijana. Kijana kuwa kwenye hali hii ni makuzi lakini mambo anayoyafanya hayazuii kuzingatia maadili na utu wema. Michakato mingi ya kijana wakati huu huwa ni kutokana na mabadiliko ya kihomoni yanayotokea katika miili yao kwa kipindi hiki, hususani katika masuala ya mapenzi. 

Mpenzi msomaji, naomba kuishia hapa kwa leo ili niandae mwendelezo wa mada ya wiki ijayo!

Pd. Dkt. Stephen NYAKUMOSA Kadilo

Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi ya Afya na Tiba Shirikishi cha Mt. Francisko (SFUCHAS)-Ifakara.