Kama ni ukweli kwamba Kanisa linafanya Ekaristi, ni jinsi hiyo hiyo ilivyo kweli kwamba Ekaristi inafanya Kanisa, na kulifanya Sakramenti ya Kristu, fumbo na kigezo cha umoja ambao Mungu anataka na watu wote. “Katika fumbo kuu takatifu la Ekaristi yanapatikana mafao yote ya kiroho ya kanisa” CPO 5).

 

Jumuiya ya Kitawa au Kikristu inayotaka kukua katika imani na kuwa ya kimisionari ni lazima iweke Ekaristi kama nguzo ya maisha na kazi zake, ili iendane na Ekaristi na kuchota kutoka kwayo mafunzo na namna ya kuishi.

 

Ekaristi inageuza jumuiya ya Kitawa au ya Kikristu kuwa Kusanyiko

  • Linalosikiliza Neno la Mungu na linaloweza
  • Kuzungumza na Bwana wake,
  • Jumuiya inayoelewana ambayo imo kwa ajili ya utumishi wa wengine,
  • Jumuiya ya kienjili na kimisionari.

 

  1. Ekaristi Inaunda Jumuiya ya Kitawa au ya Kikristu Kuwa Kusanyiko

 

Kusanyiko ni alama ya kwanza inayoonekana katika sherehe na adhimisho lolote: kusanyiko halianzishwi na binadamu, bali ni matokeo ya dhamira na uhuru wa Bwana anayewaita waumini kujumuika pamoja naye.

  • Ni mwito kwa watoto wa Baba wa pekee, na Ndugu zake Kristu, katika umoja wa Roho Mtakatifu ill kuushinda mgawanyiko wowote.

 

  • Ni katika kusanyiko la Ekaristi ambapo Kanisa au watawa wanakuwa “Watu waliokusanyika katika umoja na Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.”

 

Katika kusanyiko hili, kila Mkristo au Mtawa ana kipaji, karama, kazi na huduma ya kufanya ili kukamilishana; muumini aweza kuwa fumbo la hierakia linaloongoza ibada ya Ekaristi au moja ya karama tofauti, au moja ya miito na njia mbalimbali za maisha.

 

Katika kuadhimisha Ekaristi, kila  mkristu au M[wa]tawa [w]anaalikwa

  • Kuvibadilisha na kuvitumia vipawa vyake, pia
  • Kuvikubali vipawa vya wengine na kila mmoja
  • Aweke wazi vipawa vya jumuiya ya wakristu.

 

Ni katika kusanyiko hili ambapo Watawa wanaalikwa kudhihirisha alama ya ukatoliki na umoja wake unaoenea duniani kote, likiepuka hatari na dalili zozote za kibinafsi na tabia za kibaguzi.

 

Tukiwa tumekaribishwa na kupatanishwa hivyo na nguvu ya Rehema na Huruma ya Mungu, ni lazima tujibidishe kuwa vielelezo na njia ya kukubalika na kupatanishwa kwa wote.

 

  1. Ekaristia Huikamilisha Jumuiya ya Kitawa na ya Kikristu Inaposikiliza Neno la Mungu

 

Mungu, katika Pendo lake kuu, daima huzungumza na kila mmoja kama rafiki (rej. DV 2): Huelekeza Neno lake – Neno liwaangazalo na kuwaokoa watu wake walioitwa katika kusanyiko. Mungu kwa mara nyingine hutujia kupitia mahubiri ya Neno lake, hapa na sasa, kutufunulia mpango wake wa wokovu ili nasi tuushiriki. Kristu mwenyewe ndiye huzungumza nasi na hutuhubiria Injili yake kama chemchemi ya matumaini na uongofu.

 

Wakati wa kusanyiko ni wakati mwanana kwa ukuaji wa jumuiya ya Kitawa na Kikristu; kwa kufanywa upya katika imani pamoja na kuneemeshwa na neno, jumuiya inakua na kuimarika katika kutambua kuwa imealikwa kuitangaza Injili ya wokovu kwa wote.

 

Utangazaji wa Neno la Mungu wakati wa mwaka wa Liturjia huwasaidia wanajumuia daima kuwa katika hali ya ufuasi wa Kristu katika hali zao mbalimbali za maisha. Yesu huzungumza na wanajumuiya kupitia Neno lake la uzima na kweli. Hivyo umuhimu wa homilia (mahubiri), yaani umegaji wa mkate wa Neno la Mungu kwa kuzingatia kwa uaminifu ujumbe wa Bibilia na hali ya kila mmoja. Hii kwa upande mwingine inakazia umuhimu wa kujiweka katika hali nzuri ya kusikiliza na kutengeneza mazingira mwafaka kwa ajili ya ukuaji wa hatua kwa hatua katika imani.

 

Kwa kusikiliza Neno la Mungu, kila Mtawa na Mkristu na jamii nzima ya Kikristu, anaweza kupata mwanga wa kugundua dalili za matendo ya Mungu na wokovu wake katika namna na hali tofauti; wakati huo na kwa pamoja mtawa au mkristu huyo anapata werevu na nguvu za kupigana na namna zote za mabaya na dhambi zinazoupinga mpango wa upendo wa Mungu.

 

  1. Ekaristia Huwafundisha Wanajumuiya Jinsi ya Kujadiliana na Namna ya Kuitikia Majadiliano

 

Jumuiya ya Kitawa au ya Kikristu inayoadhimisha ibada ya Ekaristi daima huchagizwa na Mwenyezi Mungu, kwa njia ya Neno na pendo lake, kwa imani iliyofanywa upya kuitikia kwa kuanzisha mazungumzo ya kindugu na Mungu wakipokea nia na matakwa yake pamoja na kujibidisha katika kuzitunza Ahadi za Ubatizo na Nadhiri zao.

 

Kusikiliza Neno la Mungu kwa imani kunageuka na kuwa utii wa imani yaani ile NDIYO, Amina ya uaminifu thabiti juu ya kile Mungu anachotuambia kuhusu fumbo lake la wokovu. Kwa mantiki hiyo basi maisha ya Kitawa au ya Kikristu yanakuwa

  • Mwito na mwitiko wa kweli na wa kila siku,
  • Jadiliano la kindugu linalofungua undugu kwa wote na kwa sala za maombezi.

 

Kitendo cha kukiri ubatizo kwa imani katika Ekaristia na pia sala za waumini wote, vyote kwa pamoja vinaashiria undani wa umaana wa mazungumzo kati ya Mungu na sisi na kati yetu na Mungu.

 

Mazungumzo hayo hayaishi kwenye ibada tu, bali yanahusisha mfumo mzima wa maisha ya mkristu mbatizwa na jumuiya nzima ya wakristu. Mazungumzo haya yanatulazimu daima

  • Kudhihirisha ukomavu na ubora wa imani yetu,
  • Kudhihirisha ubora wa huduma zetu na pia ushuhuda wa imani ambayo jumuiya inaonyesha, na mwisho
  • Kudhihirisha dhamira na uwezo wa kukidhi haja za wengine, hasa maskini, kwa moyo mkunjufu wenye mapenzi yasiyoelezeka kwa maneno.

 

Mjadala wetu na Mungu katika Ekaristia daima, mtihani wake ni katika mahusiano yetu ya kimaisha na familia zetu pamoja na jirani zetu, katika jumuiya zetu na Kanisa lote katika ngazi za ulimwengu.

 

Jumuiya ya Kitawa au ya Kikristo inayoadhimisha ibada ya Ekaristia daima iko katika mazungumzo na Mungu ambaye Mungu mwenyewe ndiye aliyeanzisha mazungumzo haya tangu zama za historia ya wokovu na anaendelea vivyo hivyo hata leo na sisi. Kwa hivyo Watawa ni vyema wakijifunza mwenendo na tabia za mazungumzo ya Mungu na kuzimiliki kwa kuzitumia kati yao, hasa tabia kama vile ukarimu, uwazi wake kwa wote, hisani na upendo wake kwa kila binadamu katika hali yoyote ile.

 

  1. Ekaristi Huunda Jumuiya ya Majitoleo (Ya Toba) Yenye Mshikamano

 

Adhimisho la Ekaristi linalofanywa na jumuiya ya Watawa linadhihirishwa katika kujitoa sadaka ya nafsi, sadaka ya msalaba wa Kristu. Upeo wa adhimisho uko katika kilele wakati wa adhimisho la Ekaristi. Kwa kufanya kumbukumbu na rudio la karamu ya Bwana, Pasaka inaendelezwa : Kristu anajitoa mwenyewe kwa upendo.

 

Kwa njia ya ishara za Ekaristi ambazo zinajitokeza katika kujitoa huko, Kristu mwenyewe anajitoa kama sadaka ya Pasaka kwa ajili ya wokovu wetu.

  • Ekaristi ni mwili na damu yake aliyomwaga kwa ajili ya wokovu wa watu wote.
  • Ni sadaka ya Yesu msalabani inayotufungulia ufahamu wa mpango wa wokovu wa Mungu, fumbo la Kristu kujifanya mtu likamilikalo msalabani na pendo la Mungu lililo kubwa mno na lisiloelezeka.

 

Msalaba ni kielelezo cha jinsi gani “Umwilisho” ni Mungu anavyoshiriki ubinadamu wetu, ingawa tunatengwa naye kwa mapungufu na madhara (mabaya) ya dhambi.

  • Ni ushahidi tosha wa mshikamano wake nasi katika aibu yetu, duku duku zetu na mahangaiko na hata katika kifo.
  • Msalaba ni ufunuo mkuu wa mshikamano wa Mungu na watu wake;
    • Ufunuo wa ushindi wa pendo lake dhidi ya dhambi,
      • Pendo ambalo limekuwa njia ya wokovu.

 

Mtawa au Mkristo aliyejitoa na kutolewa pamoja na Kristu kunamaanisha kushiriki kikamilifu katika kifo na ufufuko, katika pendo lake kwa Baba na watu kwa ajili ya wokovu wao.

 

Jumuiya ya Kikristu au ya Watawa, katika kusanyiko lake la kiekaristia kumzunguka Kristu wa Paska, inaalikwa daima kuikaribisha na kuipokea zawadi ya upendo ambayo ni sadaka, ili kuwa thabiti kumfuata katika njia ya mshikamano na upendo kwa wote, hasa wale wasiojiweza na masikini.

 

  1. Ekaristi Huifanya Jumuiya ya kikristu au ya Kitawa kuwa Jumuiya na Huduma

 

Ekaristi, sadaka ya agano jipya, ni zawadi ya umoja wa kina kati yetu na Mungu na miongoni mwetu wenyewe. Kushiriki kwetu katika Ekaristi kunatufanya kuwa na uhusiano wa karibu na Kristu, ambaye ni sura halisi ya Mungu Baba na anatoa mwaliko wa ukarimu katika kushiriki kwenye umoja wake na Baba na Roho Mtakatifu (rej. Yob 5:56-57).

 

Ushirika huu wa Ekaristi ni ushuhuda imara wa Amri Mpya ya Mapendo na ya kumfuasa Kristu.

  • Ushirika na Kristu huanzisha na kustawisha ushirika na wenzetu;
  • Ni chanzo, na uendelezaji wa undugu wa Kristu,
  • Kugeuza Kanisa kuwa familia na kuunga mkono juhudi za umoja wa makanisa – Uekumeni.

 

Ekaristi ni chemchemi na mtihani (wa kila siku) kwa umoja wetu,

  • hisani na huduma zetu kwa wengine.

Ekaristi kwa mujibu wa waenjilisti Luka na Yohane, inaambatanishwa na Amri ya Mapendo na moyo wa kusaidiana unaotakiwa kuwa miongoni mwa wafuasi wa Yesu (rej. Lk 22: 24-27; Yob 13).

 

Mkate tuumegao wakati wa Ekaristi ni lazima utusukume kugawana pia mkate katika maisha, yaani,

  • Kugawana mkate wa mapendo, jinsi tulivyo na tulivyo navyo;
  • Ni lazima utufanye kuwa wenzi wa meza moja katika Kanisa na kwa kila mmoja wetu.
  • Vile vile ni lazima mkate huu utufundishe jinsi ya kulitumikia Kanisa na wenzetu wote.

 

  1. Ekaristi Hufundisha Jumuiya ya Kikristu au ya Kitawa Moyo wa Kimisionari na Utangazaji wa Injili

 

Adhimisho la Ekaristi Takatifu humalizika kwa mwaliko wa kwenda na amani,

  • Kutangaza na kushuhudia kwa ulimwengu wote kifo na ufufuko wa Kristu.
  • Tunu tuliyopata katika Ekaristi hatupaswi kuikalia tu sisi wenyewe; ni vyema na haki tukawaeleza na wengine kuhusu jambo hili.
  • Kila adhimisho la Ekaristi ni mwaliko mpya wa jukumu la umisionari tulilopewa na Kristu mfufuka, na pia ni chimbuko, nguvu na egemeo lake.

 

Jumuiya ya Ekaristi ni lazima iwe na umisionari, na huu umisionari ni lazima uwe moja ya sifa za jumuiya ya Ekaristi. Kwa mantiki hii, kama jumuiya zetu zinaonyesha kudorora mara nyingine katika kazi za kitume au zinaonyesha uenezaji dhaifu wa Injili, je hatutakuwa sahihi kusema kuwa hii inatokana na ukweli kwamba jumuiya zimeshindwa kuiruhusu sakramenti ya Ekaristi itoe nguvu zake katika kuhubiri?

 

Kila jumuiya ya Kitawa au ya Kikristu inaalikwa kuchunguza upya njia, lugha na mbinu zake zote na mambo yote yanayohitaji marekebisho ili kazi zao za unezaji Injili zizae matunda katika maeneo husika na duniani kote kwa ujumla: “Kristu alikufa, Kristu amefufuka, Kristu atakuja tena.”

 

Hitimisho

 

Jumuiya ya kikristu au ya Kitawa inapaswa kuwa Jumuiya ya kiekaristi ikiwa inafuata mambo muhimu kama ifuatavyo

  • Kwanza kabisa, kwa kuienzi kumbu kumbu ya furaha kubwa ya
    • kushuka toka mbinguni na
    • Kujifanya mtu kwa Mwana wa Mungu [UMWILISHO],
    • Kujifanya kwake mkate wa uzima kwa dunia na
    • Kuendelea kuwepo kwake daima kati yetu katika fumbo la Ekaristi.

 

  • Kwa kuamua kuiishi Utawa katika hali mithili ya jubilei za Agano la Kale na Agano Jipya, yaani,
    • Katika moyo wa uongofu na kutukuza,
    • Katika udugu na moyo wa kusameheana.
    • Ekaristi ni lazima iwe chazo cha aina ya maisha yanayokamilika katika uhusiano wa kikristu kama ” wana wa na uhusiano wa kidugu kwa watu wote.

 

Jumuiya ya Kikristu au ya Kitawa inakuwa imefikiwa kwa kiwango cha juu kama

  • Fumbo la Kristu litakuwa limetangazwa,
  • Fumbo la Kristo limesherekewa, na watu wameliishi na kulishuhudia katika Sakramenti ya Ekaristi, kama
  • Fumbo la Ekaristi ni chanzo na kilele cha maisha ya Kitawa na Kanisa.

 

Jumuiya nzima  ya  kikristu au ya kitawa, ingawa ni ndogo, maskini na iliyotawanyika, katika meza ya Ekaristi linaye Kristu Bwana wetu anayeliunganisha Kanisa kama moja, katoliki na la kitume (rej. LG 26).

 

  • Wakati wote Kanisa linaalikwa kuwa na umoja, kama vile liturgia ya Mozarabiki inavyoelezea jambo hili kwa uzuri: “ili kwa njia ya mwili na damu ya Bwana jamii yote yaKanisa iunganishwe kuwa kitu kimoja” (rej. LG 26).

 

Jumuiya ya Kikristu au ya Kitawa katika Ibada ya Ekaristi

  • Hukusanyika mbele ya Baba Mungu kama familia yake na jamii yake ya makuhani; Tunatambua kuwa sisi ni uko mteule, watu wa milki ya Mungu.

 

  • Husikiliza Neno la Bwana ili lipate changamoto la kuwa daima “kusanyiko,” jumuiya inayo – kusanywa na kufinyangwa na Neno;

 

  • Hufanya upya Kiapo cha Imani tuliyoipokea katika Ubatizo na Nadhiri za Kitawa, kujikita katika wajibu wa kuwaombea watu wote, ili liweze kuwa Kanisa lenye uaminifu kwa imani liliyopokea, na daima linawaombea watu wote wokovu;

 

  • Huungana na Kristu katika kumsifu Baba na Roho Mtakatifu, na
    • kujitoa kwake kwa kumtolea sadaka takatifu;
    • Inakuwa lyenyewe ni kafara na sadaka kupitia kile kinachomtolea Baba, sadaka inayokubalika kwa Baba kila siku.
  • Huwa Mwili na Roho moja katika kusanyiko la Ekaristi na moja kwa moja kumfikia kila mtu ulimwenguni kote na kushuhudia kwa maneno na matendo ya “Kiekaristia” uwepo wa Bwana ulimwenguni na fumbo lililoadhimisha.

 

Uwepo wa daima wa Bwana katika Ekaristi, uwepo unaotunzwa ndani ya Tabernakulo au unaowekwa wazi kwa ajili ya waumini kuabudu, kwa vile “unatokana na sadaka ya kujitoa na mwelekeo wake ni muungano wa kisakramenti na kiroho” (rej. Eucharisticum Mysterium 50), ni lazima uwe lengo la ibada ya watawa, ili uwavute na kuwaingiza zaidi na zaidi ndani ya fumbo la Pasaka.

 

Wakati Watawa au jumuiya za kikristu zinajiweka kifudifudi mbele ya Sakramenti ya Ekaristi, zinabainisha sura halisi ya Kanisa – Bibi Arusi katika hali ya sala, kuabudu na tafakari juu ya Bwana Arusi katika fumbo lipitalo ufahamu wote. Uwepo wa Kristu katika Ekaristi:

 

  • Ni mwaliko kuabudu, kwa sababu fumbo hili liko juu ya ufahamu wetu, vile vile kwa sababu utukufu wa upendo wa uwepo huu ulivyo karibu nasi, hututia hamasa ya kushukuru iliyo kuu mno imstahiliyo Mungu peke yake kama Bwana wa uhai na uzuri wote;
  • Hukuza hali ya kutafakari, katika hali ya kujawa na amani, imani na upendo, ambao ni kuwa na Kristu katika hali ya maelewano na urafiki mkuu;
  • Husaidia watawa kusali kwa kionjo ambacho Kristu alikuwa nacho kwa Baba yake, na kinachodhihirishwa kwenye sala ya Ekaristi: kuabudu, kusifu, kubariki, kuomba; na kututia moyo ili tupate kujitoa sisi wenyewe kwa Baba pamoja na Kristu kwa njia ya Roho Mtakatifu na pia kuwaombea wengine wokovu.

 

Kwa njia hii watawa wanakiendeleza katika maisha yao kile ambacho wamekisherehekea na kuadhimisha katika fumbo wakati wa Misa na kwa hivyo wanajifunza kuyaoanisha maisha yao ya kila siku na sakramenti hii.

 

Aidha kama Yesu alivyo Ekaristi kwa Baba na kwa Kanisa, kwa mantiki hiyo Jumuiya ya Kitawa inayoishi kwa kuikiri na kuiadhimisha Ekaristi Takatifu, hubadilisha mfumo wake wa maisha na kuwa chombo cha kiroho kinachokubalika kwa Mungu.

  • Na kila kielelezo cha matendo yake huwa ni Ekaristia mbele za Baba na kwa dunia. Kwa njia hii jumuiya ya watu wa Mungu iliyo safarini inapata katika mkate wa Ekaristi “esca viatorum,” yaani chakula cha safari, manna ya kula njiani ikiwa katika hija, na imepewa uhakikisho wa kulifikia lengo lake.

 

Wakristu au Watawa hukumbuka ukweli huu daima katika sala ya Ekaristi na wanajua fika kuwa si wapweke bali wamezungukwa na jumuiya kubwa ya Wakristu wengine wengi duniani kote, Wakristu ambao wako nao pamoja katika safari kuelekea lengo lao, wakikingwa na nguvu na kuwa katika umoja na Mama Bikira Maria na watakatifu wote, ambao Kanisa daima huwakumbuka kwa heshima katika kila adhimisho la ibada ya Ekaristi.

“Bwana Yesu, wewe ni mkombozi pekee wa dunia. Wewe ni mkate ulioshuka toka mbinguni. Wewe ni mkate wa maisha mapya.”