Maadamu kijana yuko mitandaoni na mitaani akiwa amepungukiwa mori na shauku ya kuja kanisani, sipendi kumrudisha kwa nguvu ili wote tuwe kundini. Mimi namtafuta kama rafiki. Tena, sipendi arudi kwa shari isije ikawa kama Waswahili wasemavyo, ‘majuto ni mjukuu.’ Hata hivyo, kijana akijisahau sana mahali alipo anaweza akarudi kundini akiwa amejeruhika kwa sababu atakuja kwa mshtuko. Naam, ni ukweli mtupu. Maisha na marekebisho ya kiroho mara nyingine huja kwa mshtuko fulani unaoangaza kujirudi. Risasi haiwezi kutoka kama chombo cha kufyatulia hakijaguswa. Ndicho kisa cha hadithi ya mtu aliyepoteza njia wakati wa mchana akaiona tena usiku kwa mwanga hafifu wa nyota.

Katika maisha tunaweza kupoteza njia wakati wa mchana tunapokuwa tunatembea kwenye barabara za mafanikio na maisha mema yenye raha na buraha. Tunaweza kuja kugundua njia yetu sahihi wakati wa usiku tutakapokuwa tunatembea kwenye shari ya mwanga hafifu wa nyota.

Kijana asiporudi kundini mwa Bwana mapema wakati huu wa mchana inawezekana kurudi baadaye usiku kwa njia ya shari na ikiwezekana baada ya kugongwa na taabu nyingi. Katika malezi ‘samaki mkunje akingali mbichi.’ Tatizo la kumkunja samaki akiwa amekauka ni kumfanya avunjike. Si rahisi kubadilika baadaye kama tabia itakuwa imepinda!

Nimejifunza kitu maishani. Wakati mwingine shari fulani husaidia kurudisha watu kwenye mstari kama wameenda tenge na hivyo kurekebisha maisha yao. Hii naiita ni shari mbaya ambayo huwa tunaileta sisi wenyewe kwa kuiga mambo mabaya na yasiyofaa. Kijana aondokane na shari hii ili mabaya mengi yasije yakampata akajikaanga kwa mafuta yake mwenyewe. Lakini, ipo shari nyingine ambayo hatuwezi kuikwepa ambayo ikifika ingawa inaumiza, husaidia kukwepa majanga fulani makubwa mbele ya maisha. Ninampa moyo kijana ili shari hii ikitokea maishani apambane nayo tu maana hamna namna! Kuna hadithi kutoka familia moja huko China:

Hapo zamani za kale familia moja huko nchini China ilikuwa na maisha yenye dhiki sana. Baba, mama na kijana walimiliki punda mmoja tu. Siku moja walipoamka asubuhi hawakumkuta punda mahali alipokuwa anakaa. Majirani wakasema kwa mshangao: ‘Loo, hii ni bahati mbaya sana!’ Baba wa familia akajibu kwa hekima akasema: ‘Kama ni bahati mbaya au ni nzuri, nani anajua?’ Baada ya siku kumi, walipoamka asubuhi walikuta yule punda amerudi akiwa na punda milia tisa. Majirani wakasema: ‘Loo, ni bahati njema sana!’ Baba wa familia akasema: ‘Kama ni bahati njema au ni mbaya, nani anajua? Siku moja kijana wakati anawalisha punda wake, punda mmoja alimpiga teke akaanguka na kuvunjika miguu yote. Majirani wakasema: ‘Loo, ni bahati mbaya kweli! Baba wa familia akajibu akasema: ‘Kama ni bahati mbaya au ni nzuri, nani anajua?

Siku moja wezi kutoka sehemu za mbali walifika kwenye kijiji ambacho familia ilikuwa ikiishi. Mali na vitu vingi pamoja na mifugo yote ilichukuliwa. Tangazo likasikika kijijini likiwataka vijana wote waende mstari wa mbele ili kurudisha mali zote za kijiji. Mapigano yalikuwa makali sana kiasi kwamba vijana wengi waliuawa na wengine kuumizwa sana. Kwa vile kijana alikuwa amevunjika miguu yote, hakuweza kwenda vitani. Je, Kijana alipovunjika miguu ilikuwa bahati njema au mbaya?

Tunajifunza kitu cha kusisimua kutokana na mwanzo wa wongofu wa Mtakatifu Augustino wa Hippo (354-430). Mwanzo wa safari yake kuwa mkristo ulikuwa hivi: akiwa kwenye bustani yake alisikia sauti ya mtoto ikimwambia kwa Kilatini ‘tolle, lege’ tafsiri yake kwa Kiswahili ni ‘chukua, usome.’ Wakati huo Augustino alikuwa anasoma nyaraka za Mtume Paulo. Mara akakiachia kitabu kianguke na kijifungue chenyewe. Alishangaa kusoma aya ya 13 ya sura ya 13 ya Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi ambapo Paulo anawashauri wasomaji wake waachane na tamaa za mwili na kutembea kwenye njia ya Kristo. Kuanzia hapo aliamua kuwa Mkristo na akabatizwa.

Kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu (Rum 13:13).

Nakualika kijana ambaye huna nafasi kwenda kanisani sasa umsikilze mtume Paulo anaposema,

Usiku umeendelea sana, mchana umekaribia; basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru (Rum 13:12).

Ndugu msomaji wa Makala hii, tokea wiki iliyopita nimekuwa nikimshauri kijana arudi kanisani aache kuelemewa na masumbufu ya maisha na kumwalika amtambue Mungu ili afanikiwe maishani mwake. Je, huyu kijana ni nani hasa? Pata jibu wiki ijayo!

Pd. Dkt. Stephen NYAKUMOSA Kadilo

Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi ya Afya na Tiba Shirikishi cha Mt. Francisko (SFUCHAS)-Ifakara.