UPONYAJI WA MAJERAHA KATIKA MAISHA

“Nina uwezo mkubwa mno wa kuyafanya maisha yawe ya uchungu au ya furaha. Nina uwezo wa kuwa chombo cha maumivu makali au chombo cha kuvutia, naweza kunyanyasa au kutia hamasa, kuumiza au kuponya. Kama tukiwatendea watu  kadri walivyo, tunawafanya wanakuwa wabaya zaidi. Kama tukiwatendea watu kama wanavyopaswa wawe tunawasaidia kuwa namna wanavyoweza kuwa”.

– Wolfgang Von Goethe

Kila mmoja wetu ameitwa kuwa mponyaji wa majeraha ya wengine licha ya kwamba  yeye mwenyewe anayo  majeraha yake. Binadamu wote tunayo majeraha ya kihisia, kiakili, kiroho, kimwili, kiuchumi na kifamilia. Inwezekana una majeraha ya kusalitiwa na mwenzi wako wako wa maisha. Inawezekana una majeraha ya kufiwa na mwenzi wako wa maisha. Inawezekana una majeraha ya kuishiwa na mtaji wa kibiashara. Inawezekana una majeraha ya kiuchumi. Mjeraha ni mengi. Nafasi hainiruhusu kuyataja yote. Itoshe kusema kamba makala hii ina nia ya kuyaponya majeraha yako ya kihisia, kiuchumi, kifamilia, kiafya na kiroho. Kila mwisho wa kitu au hali fulani huleta mwanzo mpya! Ninakualika usafiri pamoja nami katika makala hii inayolenga kukutia moyo, kukufundisha, kukufariji na kukuimarisha.

Unapoamua  kufanya mambo makubwa katika maisha yako, ni lazima uwe tayari kukabiliana na watu ambao wamejipanga kuyashambulia malengo yako[Vission Attackers]. Hawa ni watu ambao wameamua, wamedhamiria na wako tayari kukukwamisha na kukushambulia kwa namna yoyote ile. Na lengo lao ni moja tu: ‘Usifanikiwe’. Kuna aina mbili za watu wa aina hii. Wa kwanza, ni wakimya [Silent Attackers]. Hawa wanakushambulia kimya kimya. Hawataki ufahamu kwamba wao ni maadui zako. Hawa wanakuonesha uso uliojaa tabasamu, lakini moyoni wanakusimanga. Aina ya pili ni; Wawazi. Hawa wanajipambanua wazi kwamba ni maadui zako. Wanakushambua waziwazi. Kanuni ya mafanikio inasema; ‘’Ni lazima ukutane na watu wa aina hii’’. Watu wa aina hii hawakwepeki. Ni mhimu sana kumwomba Mungu  kila wakati  ili  akufunulie nia ya ndani ya mioyo ya watu wanaokuzunguka.

Dunia imejaa watu wasiowatakia wenzao mema. Wapo watu ambao wakiona unafanikiwa wanaumia sana. Wapo watu ambao wanatamani kukuona ukihangaika usiku na mchana. Wapo watu ambao wakiona mnaelewana vizuri na mke/mume wako wanaumia sana. Furaha yao ni kwamba, watamani kuona hamwelewani ndani ya ndoa yenu. Wapo watu ambao wakiona mnaelewana na wafanyakazi wenzako wanaumia sana. Wapo watu ambao wanapenda wakuone ukiindelea kuishi kwenye nyumba za kupanga. Hawapendi kuona ukipata pesa wala kupata mafanikio ya aina yoyote. Naomba kukufundisha jambo la busara hapa. Watu wa wa aina hii wapo. Tunaishi nao. Wengine ni ndugu zetu wa damu. Wengine ni majirani zetu. Wengine ni wafanyakazi wenzetu. Wengine ni marafiki zetu. Wengine tunasali nao Kanisa moja. Nisikilize hapa: Usiwachukie watu wa aina hii. Ukiwachukia utakuwa unawapa upenyo wa kukudhoofisha kiutafutaji, kiupendo, kihisia na kiuchumi. Wapende watu hawa. Waombee kwa Mungu watu hawa. Siku zote wema unaushinda ubaya. Acha wakuoneshe ubaya, lakini wewe waonyeshe wema. Usitumie nguvu nyingi kuwawaza na kuwachukia. Tumia nguvu nyingi kuwasogeza mbele ya kiti cha rehema cha Mungu.  Watapigana nawe kwa namna nyingi lakini watashindwa. Wewe ni mshindi.

Watu wengi tumejeruhiwa katika maisha yetu. Tunayo majeraha mengi. Naomba kukunong’oneza jambo hili: ‘Mwenyezi Mungu anakupenda sana‘. Ni kweli, Kuna watu katika maisha yao wamejeruhiwa sana Kiroho, kimwili, Kiakili, Kiuchumi, Kimahusiano na Kiungozi. Wamejeruhiwa sana. Wamejeruhiwa na kujeruhika. Pole sana kwa kujeruhiwa. Usihuzunike sana. Usiogope. Usisononeke. Kama umejeruhiwa na mke/mme wako, kumbuka, ‘Mungu hajakuacha’. Kama umejeruhiwa na mtoto wako, kumbuka, ‘Mungu hajakuacha’. Kama umejeruhiwa na rafiki yako, kumbuka, ‘Mungu hajakuacha’. Kama umejeruhiwa na jirani yako, kumbuka, ‘Mungu hajakuacha’. Kama umejeruhiwa na serikali yako, kumbuka, ‘Mungu hajakuacha’. Kama umejeruhiwa na kiongozi wako wa kiroho, kumbuka, ‘Mungu hajakuacha’. Kama umejeruhiwa na mwajiri wako, kumbuka, ‘Mungu hajakuacha’. Narudia kusisitiza kwa msisitizo uliojaa ukweli na hekima kwamba: ‘Mungu hajakukataa. Mungu hajakuacha. Mungu anakupenda sana’.

Katika familia yangu tuliwahi kupata jeraha. Tarehe 14 September 1999, lilitokea tukio la kuhuzunisha sana kwenye familia yangu. Dada yangu kipenzi, Cecilia aliuwawa kikatili na mume wake. Dada aliuwawa akiwa anamnyonyesha mtoto wake wa kike aliyekuwa na umri wa miezi mitano. Tukio hili tulilipokea kwa mwono wa dharau. Tuliamini kwamba, mume wa dada yetu amemuua dada yetu kwa kutudharau. Vijana tuliapa kulipiza kisasi. Tulitaka na sisi kuua. Katika hali ya usiri sana, Mama yetu mzazi alifahamu nia yetu. Akatuita wote kwa pamoja na kutuambia; ‘’Wanangu nia mlio nayo ni mbaya. Acheni. Ninyi ni Wakristo! Kristo aliwapenda maadui zake. Mpendeni aliyemuua dada yenu. Kumpenda adui ni wito wa Kikristo. Naombeni mnisikilize’’. Busara hii iliyokuwa imejaa upendo na hekima ilitawanya mawazo yetu. Mpaka leo tunasalimiana na kutembeleana vyema na aliyemuua dada yetu. Tunampenda. Palipo na upendo kuna maisha. Tupendane. Methali ya watu Ufilipino  inasema, ‘’Upendo ni chumvi ya maisha’’.

Ukweli ni kwamba, unapokuwa umemchukia mtu yeyoyote yule aliyekuumiza, unakuwa bado uko kifungoni. Ili utoke kifungoni ni lazima umfungue yule aliyekupeleka kifungoni. Maumivu na uchungu hutufanya kuwa wafungwa wa mazingira ya zamani na hutukumbusha daima kile kilichotokea zamani. Mwaka 2018, nilitoa chapisho langu la kitabu kinachoitwa, ‘USIKATE TAMAA KATIKA MAISHA’’. Hiki ni kitabu ambacho kimegusa maisha ya wasomaji wengi. Wengi waliokisoma kitabu hiki wamekiri kubarikiwa na wengi kubadilisha mienendo yao ya kimaisha. Nilipata mshituko pale ambapo msomaji wangu mmoja aliponitumia ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu yangu ya kiganjani. Ujumbe wake ulikuwa unasomeka hivi:

‘’Mr, William, nilipokuwa na umri miaka tisa [9] nilibakwa na rafiki yangu aliyekuwa na miaka kumi na nne [14]. Sijawahi kumwambia mtu yeyote kilichotokea, lakini nimeitunza chuki hii moyoni. Imepita miaka 19 lakini moyo wangu bado una maumivu na hasira dhidi ya wanaume. Kila ninapokutana na mume  wangu kimwili  ninajisikia kubakwa. Ninashiriki tendo la ndoa kwa shinikizo la mume wangu’’.

 Moyo wangu uliumia nilipogundua maumivu aliyokuwa ameyabeba mwanadada huyu kwa miaka 19. Hasira inatunza chuki moyoni. Katika mazungumzo yangu binafsi na mwanadada huyu nilimuuliza: ‘’Ungependa Yesu akufanyie nini?’’ Alilia kwa nguvu sana.  Niligundua kwamba ana maumivu ya nafsi na moyo. Moyo wake ulikuwa umejeruhiwa sana. Mioyo ya watu wengi  imevunjika vunjika. Mioyo ya watu wengi inavuja damu. Watu wengi wameumizwa.  Watu wengi wana majeraha na wanashindwa namna ya kuyaoondoa majeraha yao. Watu wengi wametunza majeraha kwenye mioyo yao.

Ninaomba kukuuliza swali: ‘Je, Moyoni mwako umebeba nini?’ Kama  umembeba mtu, mtue. Mtue mume wako aliyekuumiza. Mtue mke wako aliyekuumiza. Mtue mtoto wako aliyekuumiza. Mtue jirani yako aliyekuumiza. Mtue mzazi wako aliyekuumiza kwa kukubaka, kukunyanyasa, kukutukana, kukukataa n.k. Mtue rafiki yako aliyekuumiza. Mtue mfanyakazi mwenzako aliyekuumiza. Mtue mteja wako aliyekudhulumu fedha na rasirimali nyinginezo. Kama una kinyongo, kidondoshe. Kama umeitunza hasira, iondoe. Itafute amani. Utafute upendo. Kristo anasubiri kukuponya. Anasubiri kuyaponya majeraha yako. Anasubiri uwe tayari kuyaachilia yote uliyoyatunza moyoni mwako. Amua kuwa huru kuanzia leo. Toka huko gerezani ulipofungwa.  Balidilisha historia ya maisha yako kuanzia leo.

Nakusihi: ‘Usitunze chuki moyoni kwa muda mrefu’. Ajabu ni kwamba ukiwa na uvundo mwingi wa chuki moyoni mwako unaweza ukaanza kuwaza mawazo ya kujinyonga, kulipiza kisasi, kunywa pombe kupita kiasi ama kunywa sumu. Unapokuwa umeshindwa kusamehe usitegemee kupata amani ndani ya roho yako.

 Hatuwezi kuishi pasipo kutoa msamaha au kuupokea msamaha. Kumbuka! Msamaha unajenga mahusiano yalivunjika. Una kila sababu ya kutoa msamaha. Una kila sababu ya kuwa na amani. Una kila sababu ya kuwa na uhusiano mzuri na familia yako. Una kila sababu ya kuwa mshauri mzuri, hivyo basi kuwa mwepesi wa kutoa msamaha kwa wanaokukosea. Anza leo kuomba msamaha kwa Mungu. Anza leo kuomba msamaha kwa uliowakosea. Anza leo kuwasamehe waliokukosea. Leo hii utakuwa mwana wa Mungu na mbinguni ndiko kutakuwa nyumbani kwako milele yote.

Nakusihi wewe ambaye umeumizwa na mzazi wako: ‘Msamehe’. Umeumizwa na mtoto wako wa kuzaa: ‘Msamehe’. Umeumizwa na mme wako: ‘Msamehe’. Umeumizwa na mke wako: ‘Msamehe’. Umeumizwa na kaka yako, au dada yako: ‘Msamehe’. Umeumizwa na jirani yako: ‘Msamehe’. Umeumizwa na rafiki yako: ‘Msamehe’. Umeumizwa na mwajiri wako: ‘Msamehe’. Kusamehe ni bure. Yawezekana kwa wakati huu mambo yako hayaendi sawa. Una mawazo. Hupati usingizi. Unawaza lakini hupati majibu ya mawazo yako. Unahisi umetengwa. Unahisi umekataliwa na familia au jamii. Unakuwa mtu wa kunung’unika kwa kila jambo.

Mwandishi Dresch Messenger anasema haya, “Maadui wako ni rasilimali yako ya thamani kama haulipizi kisasi kwa sababu wanakufanya uwe macho na kuchapa kazi vinginevyo ungebweteka”. Na mwandishi mwingine aitwaye Sidney Sheldon anasema, “Kufanikiwa unahitaji marafiki na kufanikiwa sana unahitaji maadui”.  Mwandishi wa habari, David Brinkley naye anafafanua kwamba, ‘’Mtu aliyefanikiwa sana ni yule ambaye anaweza kuweka msingi imara kwa tofali zile ambazo wengine humrushia kumpiga nazo’’. Maisha yanaweza kukurushia tofali nyingi. Zidake na zitengenezee msingi ambao utakuwezesha kusonga mbele. Maadui zako pia ni warushaji wa mawe. Daka mawe yao na jenga ngazi. Usiruhusu mambo hasi yanayotokea katika maisha yako yakufanye na wewe uwe ‘hasi’. Yageuze kuwa kitu chanya na yatumie kama msingi wa hatua inayofuata. Yatumie maneno wanayokusema watu kama mawe ya kuvukia ng’ambo ya pili ya mafanikio yako.

Tusiwachukie wanaotuchukia tuwapende ili waone wema na upendo wa Mungu kupitia kwetu. Adui ni wa kumuombea mazuri ili yale mazuri anayopata na kukutana nayo yambadilishe kuwa mtu mzuri. Hilo linawezekana. Ukimchukia anayekuchukua unakosea. Athisthenes Mwanafalsafa wa kigiriki alipata kusema, ‘’Wasikilize maadui wako, kwa sababu ni wa kwanza kugundua makosa yako’’. Yesu alikuwa sahihi kabisa aliposema, ‘’Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi’’ [Mat 5:44]. Ipo Methali ya kabila la wafipa wapatikanao nchini Tanzania inayosema hivi, ‘’Mvua ya Mungu huwanyeshea hata washirikina’’. Martin Luther King, Mwanaharakati mweusi alipata kusema yafuatayo, ‘’Giza haliwezi kutokomezwa na giza, bali hutokomezwa na mwanga tu. Vivyo hivyo chuki haiwezi kutokomezwa na chuki, bali ni upendo tu unaoweza kufanya hivyo’’.

Jifunze jambo kutoka kwenye maisha ya hawa majirani wawili. Huko Amerika ya Kusini kuna Mama wa kizungu na Mama wa Kiafrika waliwahi kuishi eneo moja la makazi kama majirani.  Mama wa Kizungu alikuwa na tabia ya kutupa kinyesi kwenye eneo la Mama wa Kiafrika. Yule Mama wa Kiafrika hakulipigia kelele jambo hilo. Siku moja Mama wa Kizungu aliugua sana. Mama wa Kiafrika alienda kumtembelea hospitalini.  Alimpelekea maua mazuri sana kama zawadi. Mama wa Kizungu alipoyapokea yale maua kama zawadi nzuri kutoka kwa jirani yake akauliza; ‘Umeyanunua wapi maua mazuri haya?’, Mama wa Kiafrika akamjibu; ‘Niliyaotesha kwenye kinyesi ulichokuwa unanitumia’. Mama wa kizungu akanyamaza kwa dakika chache. Baada ya dakika chache za ukimya akafumbua kinywa chake na  kusema, ‘Naomba unisamehe’.  Malipo ni hapa hapa duniani. Tenda wema uende zako. Wema ni akiba.

Namna bora ambayo Mwenyezi Mungu anapendelea tuishi na maadui wetu ni hii: Adui yako anapokata tamaa – Mtie moyo. Adui yako anapokuwa dhaifu – Msaidie. Adui yako anapokuwa mjinga – Mfundishe. Adui yako anapokuwa na majivuno – ishi maisha ya unyenyekevu ili ajifunze unyenyekevu kutoka kwako. Adui yako anapokuoneshea dharau – Mwoneshee heshima. Adui yako anapovaa sura ya chuki – Vaa sura ya upendo. Adui yako anapovaa sura ya huzuni – Vaa sura ya matumaini. Padre Faustine Kamugisha katika kitabu chake cha “Mafanikio Yoyote Yana Sababu’ anasema, “Maadui wanaweza kukusaidia bila kujua”. Kwa namna fulani adui yako anaweza akawa mtaji wa mafanikio yako. Goliati aligeuka kuwa mtaji kwa Mfalme Daudi. Bila adui Goliati, Daudi asingechukua kiti cha Kifalme. Mungu alimbariki Daudi kupitia kumshinda Goliati. Kwa namna fulani adui Goliati alisaidia kampeni za Daudi kukitwa kiti cha kifalme.

Imeandaliwa na

~William Bhoke

0 Comments

leave a comment