Pd. Dkt. Stephen NYAKUMOSA Kadilo

Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi ya Afya na Tiba Shirikishi cha Mt. Francisko (SFUCHAS)-Ifakara.

Lengo kuu la kuumbwa na kuwekwa kwetu duniani ni kumjua, kumpenda na kumtumikia Mungu ili tupate kufika kwake mbinguni. Kuishi maisha yetu ili kufikia adhma hii muhimu inatutaka maisha yetu yawe bora kwa kuzingatia misheni/wito na maono juu ya Mungu maishani mwetu. Maandiko Matakatifu yanatueleza bayana kwamba:

Heri wenye moyo safi, maana hao watamwona Mungu (Mt 5:8).

Kuwa na moyo safi ni jambo la kwanza katika maisha lakini kumwona Mungu ni jambo la pili na la muhimu kabisa. Kitu kinachovutia ni kwamba kuna uhusiano mkubwa kati ya mambo haya mawili. Kuwa na moyo safi kama wito huhusiana kwa karibu sana na hitaji la kumwona Mungu. Usafi wa Moyo huandaa maono ya aina mbili: kwanza ni maono ya kimaarifa na pili ni maono ya kiroho. Maono ya kimaarifa hukamilishwa kwa kushikilia au kutunza nguvu za kibiolojia hadi pale majaliwa ya Mungu yatakapomwandaa yule atakayeyapokea. Ndivyo anavyotuasa Askofu Mkuu Fulton Sheen.

Nguvu ya kimapenzi inapotumika katika kuzuia tamaa za mwili, nguvu hii huwa haipotei bali hubadilika na kuwa kitu kingine. Kwa mfano, nguvu ile ile ambayo mfanyabiashara hutumia ili kupata pesa nyingi, inaweza pia kumfanya awe mtakatifu. Nguvu inayotumiwa na watu kwenye uhalifu inaweza kutumika kujenga jamii na kuleta maendeleo makubwa.

Nguvu ya kibiolojia ambayo tunaitukuka sana na kuienzi, inapoenda kwenye akili hutengeneza tabia. Ushuhuda kinzanifu juu ya jambo hili ni kuwa kijana ambaye ametumbukia kwenye tamaa za kingono lazima awe na ufaulu wa chini kwenye masomo na umbumbumbu mwingi katika utekelezaji wa majukumu yake yanayohitaji umakini mkubwa. Kwa maneno mengine, baada ya kutumia hazina yote ya nguvu za mwili kimapenzi, hakuna tena kinachoonesha maisha mapya kiakili.

Pamoja na hayo yote kuna uhusiano mwingine kati ya usafi (weupe wa moyo) na imani. Kama nguvu kubwa ya maisha ya kijana inapendelea sana starehe kama muziki, mpira, tamaa za mwili na tamaa ya vitu halafu ikakosa muda wa kwenda kanisani wala kuwa na moyo wa sala Je, ni nini kimesababisha? Uhusiano wa Imani na usafi au weupe wa moyo utaweza kujibu swali hili kinagaubaga. Kupungukiwa imani kwa vijana katika ulimwengu wa sasa na katika nyakati zetu hizi sio kwamba hawajapewa sababu na umuhimu wa imani bali sababu ya imani yao inatokana na kukosa mwongozo halisi wa kimaadili ndani yao. Mdhambi anaweza kuona mambo yote vema isipokuwa Mungu tu; na ndiyo maana mwishoni mwa kila jambo mdhambi huwa haoni chochote kabisa. Bwana wetu Yesu Kristo alisema:

Nawaambia: Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang’anywa hata alicho nacho (Lk 19:26).

Kuzaliwa upya kwa ujana utatokana na ujana wenyewe kuamua kujiunda upya na kuanza maisha mapya. Wanasheria wanapokuwa wamekubuhu kuwa wala rushwa kupindukia hawahitaji daktari mwenye shahada ya uzamivu aje kuwapa vipindi vya masomo darasani bali mwanasheria aliye mwema na mwenye kuzingatia maadili ya taaluma ya sheria ndiye anaweza kuwarekebisha wenzake waondokane na mfumo huo mbaya. Viongozi wa serikali, walezi mbalimbali na viongozi wa dini wanalo jukumu la kutoa mwongozo ili kuandaa vijana wema. Jukumu la vijana kuwa wema ni la vijana wenyewe wakiongozwa na maamuzi yenye utashi kamili wa kubadilika. Mwandishi Eugene E. Kawau kwenye kitabu chake chenye anuani Maisha ya ujana: Kihisia, Kiakili na Kiimani anamnukuu Franklin D. Roosevelt aliyekuwa Rais wa 32 wa nchi ya Marekani akisema:

Hatuwezi kufikiria kila wakati kuwatengenezea vijana wetu maisha ya baadaye, lakini tunaweza kuutengeneza ujana wetu kwa ajili ya maisha ya baadaye.

Nayo Barua Kutoka Jangwani aliyoandika Carlo Carretto ilikuwa kitabu kinachomwelezea mtu aliyeenda jangwani kujifunza namna ya kusali. Sehemu moja ya kitabu hiki Carretto anasema mara kwa mara alipotea njia akiwa jangwani wakati wa mchana kwa sababu ‘jua lilikuwa juu sana angani.’ Lakini wakati wa usiku aliiona njia tena akiwa ‘anaongozwa na nyota.’

Nini maana ya habari hii? Itafafanuliwa wiki ijayo!