Mabadiliko hayazuiliki. Kubadilika kwa ajili ya yaliyobora ni ajira ya wakati wote.

-Adlai E. Stevenson II

Mabadiliko ni kanuni ya maisha na uumbaji. Hebu fikiri na uwaze. Ulipokuwa na umri wa miaka mitatu, ulikuwa wewe? Bila shaka ulikuwa ni wewe. Lakini sasa umebadilika, lakini bado ni wewe. Je, ulipokuwa na umri wa wiki moja, ulikuwa  wewe? Ndiyo ulikuwa ni wewe. Lakini sasa umebadilika, lakini bado ni wewe. Je, ulipokuwa tumboni mwa mama yako, ulikuwa ni wewe? Ndiyo ulikuwa ni wewe. Sasa umebadilika, lakini bado ni wewe. Je, miaka 300 iliyopita ulikuwa wapi? Bila shaka mbele za Mungu ulikuwa ni “wazo”. Lakini bado wewe uliyekuwa wazo mbele za Mungu bado ni wewe. Tafakari miaka 200 ijayo hautakuwa hai, lakini bado utakuwa ni wewe. Mwanafalsafa Henri Bergson anasema, ‘’Kuishi ni kubadilika, kubadilika ni kukamilika, kukamilika ni kuendelea kujiumba mwenyewe pasipo mwisho’’. Mabadiliko hayazuiliki. Mabadiliko ni ya lazima. Hakuna yeyote duniani anayeweza kuyakwepa mabadiliko.

 

Kila mtu katika maisha yake anafikiria kuwabadili watu wengine. Ni watu wachache wanafikiria kubadilika wao wenyewe. Mafanikio yaliyo bora kiroho, kimwili, kiuchumi na kifamilia ni kila mtu kukubali kuwa; ‘Mabadiliko mazuri anayotaka kuyaona yakitokea duniani’. Badilika ili uwabadili wengine. Kubali kuwa mabadiliko. Fanyika kuwa mabadiliko. Badilika ili mke|mme wako abadilike kupitia wewe. Badilika ili jirani yako abadilike kupitia wewe. Badilika ili watoto wako wabadilike kupitia wewe. Badilika ili mfanyakazi mwenzako abadilike kupitia wewe. Badilika ili familia yako ibadilike kupitia wewe. Badilika ili mtaa wako ubadilike kupitia wewe. Badilika ili taifa lako libadilike kupitia wewe. Badilika ili dunia ibadilike kupitia wewe. Mabadiliko yanaanza na mimi. Mabadiliko yanaanza na wewe. Kabla hujafikiri kumbadili mtu yeyote, fikiri kwanza kujibadili  wewe mwenyewe. Rinohold Niebuhr alisali sala hii, ‘’Mungu, nipe utulivu wa kukubali mambo ambayo siwezi kubadili; na ujasiri wa kubadili mambo ambayo naweza kubadili; na hekima ya kujua tofouti zake’’.

 

Maisha yetu yamejaa vipindi visivyotarajiwa. Usipokuwa mpokeaji wa mabadiliko katika mtazamo chanya, utakuwa mhanga wa mabadiliko katika mtazamo hasi. Mwandishi, mnenaji na mshauri wa biashara, Brian Tracy anasema, ‘’Azimia kuwa bwana wa mabadiliko kuliko kuwa muathirika wa mabadiliko’’. Kinga pekee dhidi ya athari hasi ya mabadiliko ni kuyatarajia na kujiandaa kuyapokea katika mtazamo chanya. Iko hivi; Ukipambana na mabadiliko, utaishia kuwa muathirika wa mabadiliko. Ukikubaliana na mabadiliko, utakuwa mshindi wa mabadiliko. Njia bora ya kukabiliana na mabadiliko katika maisha yako ni  kuyafanya mabadiliko yawe  rafiki  yako na sio  adui  yako. Hatuwezi kuyazuia mabadiliko. Hatuwezi kuyachelewesha mabadiliko. Hatuwezi kuyaua mabadiliko. Mabadiliko daima ni utangulizi wa yajayo kwa yaliyopo. Mabadiliko ni kesho inayobadilika leo. Kuyakataa mabadiliko ni uamzi wa kuishia jana. Bila kujali chanzo cha mabadiliko iwe binafsi, kijamii, kisiasa, kiuchumi au kiroho hatuwezi kujifanya kuwa mabadiliko hayatokei. Yanapotokea tusiyakatae. Badala yake tutafute namna bora ya kuyaelewa.  Unatakiwa kupata faida kamili kila fursa za mabadiliko zinapojitokeza katika maisha yako.

 

Tembea kwenye kusudi la Mungu. Mungu ana mpango na wewe. Anataka jambo kubwa litokee kupitia wewe. Anataka atukuzwe kupitia wewe. Uwepo wako duniani sio ajali ya kibaiolojia, bila kujali mazingira yaliyozunguka kuzaliwa kwako. Uko hai kwa sababu ya Umwilishwaji wa Ki-Mungu uliopitia kwa wazazi wako. Kutungwa kwako mimba na kuzaliwa kwako ni uthibitisho kwamba, Mungu ana mpango na wewe. Usijutie kuwa miongoni mwa wanafamilia wa kibinadamu wanaoishi katika sayari hii ya dunia. Jambo moja na la mhimu ambalo kila mtu anapaswa kulifahamu ni kwamba, Mungu hawezi kuruhusu chochote kije katika maisha yako ambacho hutaweza kukabiliana nacho. Mtume Paulo ameandika hivi;

 

‘’Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya mwanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; amabaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili’’ [1Wakorintho 10:13]

 

Maisha yako yana alama isiyozuilika. Alama hiyo ni ‘Mabadiliko’. Tazama, ulipokuwa mtoto mchanga ulikuwa huna mawazo kama uliyonayo leo. Mabadiliko yalikulazimisha kukua kutoka kwenye umri wa uchanga. Umekuwa kijana, lakini mabadiliko yanakulazimisha kuwa mzee. Mabadiliko ni kama maji yanayotiririka mtoni. Huwezi kuingia mara mbili katika maji ya  mto yanayotiririka. Mtiririko wa maji uliopita hauwezi kujirudia tena.

 

Ukiyakubali mabadiliko utakuwa mshindi wa mabadiliko, na ukiyakataa mabadiliko utakuwa mhanga wa mabadiliko. Watu ambao wamekuwa wakiyakataa mabadiliko katika maisha yao wamekuwa wakiteseka sana. Tukio la kuyakataa mabadiliko nililiona kwa baba yangu mzazi. Baba hakuukubali uzee wake. Hali hii ilimtesa sana. Niliyaona mahangaiko aliyokuwa akiyapata wakati namuuguza katika hospitali ya ‘Tumbi’. Baba alitamani kuuendelea kuwa kijana wakati wote. Usiku mmoja tukiwa hospitalini aliniamsha na kuniuliza; ‘Kwa nini nimekuwa mzee?’’ swali hili lilinidhihilishia kwamba baba hakuwa ameyakubali mabadiliko yaliyompeleka katika uzee. Haya ndio maisha yanayowapata wengi. Watu wengi leo hawapendi kuitwa ‘Baba au mama’. Wanaona wanadharishwa. Wanapendelea waitwe majina ambayo hayaendani na umri wao. Wana hofu na mabadiliko. Lakini kinachowafanya waitwe ‘Baba au mama’ ni mabadiliko. Lazima ukubali kwamba, ulikuwa mchanga, umekuwa kijana na utakuwa mzee na pengine utakuwa bibi au babu.

 

Tukubali kuyapokea mabadiliko kwa mwitikio chanya {+}. Mwandishi wa vitabu na mwandishi wa michezo ya kuigiza, George Bernard Shaw anasema, ‘’Maendeleo hayawezekani pasipo mabadiliko, na wale wasioweza kubadilisha akili zao hawawezi kubadilisha chochote’’.

 

Na William Bhoke