Askofu mkuu Marek Solczyn’ski Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Jumapili tarehe 13 Septemba 2020 katika Ibada ya Misa Takatifu anatarajiwa kumvika Pallio Takatifu, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam katika Ibada ya Misa Takatifu, itakayoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu, Jimbo kuu la Dar es Salaam kuanzia majira ya saa 4:00 asubuhi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume, tarehe 29 Juni 2020 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, alibariki Pallio Takatifu 54 watakazovishwa: Dekano wa Baraza la Makardinali pamoja na Maaskofu wakuu walioteuliwa katika Kipindi cha Mwaka 2019-2020.

 

Mitume hawa walikuwa ni mashuhuda wa maisha, msamaha na mashahidi wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Baba Mtakatifu Francisko anasema, watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa imani, waliyamimina maisha yao kama sadaka safi isiyokuwa na mawaa mbele ya Mungu na ni ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Mitume hawa ni kielelezo cha umoja unaofumbatwa katika upendo na utofauti; katika mateso, sala na ushuhuda wa imani. Wao kielelezo cha unabii unaosimikwa katika ushuhuda wa Injili inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha, kama kielelezo cha upendo kwa Mungu; unaoleta toba na wongofu katika maisha ya waamini.

 

Pallio takatifu  ni kitambaa cha sufi safi kinachotengenezwa na manyoya ya kondoo wachanga; na kinavaliwa na Baba Mtakatifu pamoja na Maaskofu wakuu wa majimbo makuu ya Kanisa Katoliki wanapokuwa katika majimbo yao. Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Januari anaadhimisha kumbu kumbu ya Mtakatifu Agnes, Bikira na shahidi, aliyeuwawa kunako karne ya tatu; akaonesha upendo wa pekee sana kwa Kristo Yesu mchumba wake wa daima, kiasi cha kuyasadaka maisha yake, ili asiuchafue ubikira wake. Yesu mwenyewe alitambulishwa na Yohane Mbatizaji kama Mwana Kondoo wa Mungu anayebeba na kuondoa dhambi za ulimwengu. Ni Mapokeo ya Kanisa kwamba, Siku kuu ya Mtakatifu Agnes, wanabarikiwa kondoo ambao manyoya yao yatatumika kutengenezea Pallio Takatifu, wanazovishwa Maaskofu wakuu katika maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Petro na Paulo Mitume. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

 

Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, Mchungaji mwema, hata Maaskofu wakuu wanahamasishwa kuwabeba kondoo wao kama kielelezo cha wachungaji wema; daima wakikumbuka kwamba, wameteuliwa si kwa ajili ya mafao yao binafsi, bali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya kondoo wa Kristo. Maaskofu wakuu wapya wanapaswa pia kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Pallio takatifu ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baada ya mabadiliko yaliyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2015, tangu wakati huo, Maaskofu wakuu wapya wanavishwa Pallio Takatifu na Mabalozi wa Vatican majimboni mwao, ili kuwashirikisha watu wa Mungu kutoka katika majimbo yanayounda Jimbo kuu husika tukio hili adhimu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia! Haya ni maboresho makubwa katika ufahamu na utambuzi wa maana halisi ya Pallio takatifu wanazovishwa Maaskofu wakuu.

 

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania, ni kati ya Maaskofu wakuu 13 kutoka Barani Afrika ambao wanavishwa Pallio takatifu kwa kipindi cha Mwaka huu wa 2020. Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Marek Solczyn’ski Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Jumapili tarehe 13 Septemba 2020 katika Ibada ya Misa Takatifu anatarajiwa kumvika Pallio takatifu, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam katika Ibada ya Misa Takatifu, itakayoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu, Jimbo kuu la Dar es Salaam kuanzia majira ya saa 4:00 asubuhi.

 

Waswahili wanasema, “eti Jimbo kuu la Dar es Salaam kumenoga.” Tukio hili la kihistoria linatanguliwa na maadhimisho ya Siku kuu ya Kutukuka kwa Msalaba ambayo kwa kawaida inaadhimishwa tarehe 14 Septemba ya kila mwaka. Kutokana na sababu za kichungaji, ili kuweza kuwashirikisha waamini maadhimisho haya, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu Jumamosi tarehe 12 Septemba 2020 kwenye Kituo cha Hija Pugu. Misa hii itatanguliwa na Ibada ya Kitubio na kufuatiwa na Njia ya Msalaba.

Source: VATICAN