Unyenyekevu na upole unafumbatwa katika lugha ya akili, moyo na mikono, ambavyo hutimilisha mlinganyo kati ya kilicho ndani ya mtu na kile akitendacho mintarafu matendo ya huruma. Papa analielekeza Kanisa kuwa hospitali katika uwanja wa mapambano. Upole ni chombo cha mwanadamu kinachomwozesha mtu kusafiri na kuzifikia hisia za ndani za mtu na kuweza kujenga umoja.

Na Shemasi Karoli Joseph Amani, Vatican.

Katika ulimwengu huu wa kidigitali wengi wanajiuliza kama kweli ulimwengu huu wa kimtandao hauwafanyi watu kutengeneza mipaka na kujiweka mbali mmoja dhidi ya mwingine. Ikiwa si rahisi kubofya ‘like’ katika ukurasa wa mtu sembuse kumsaidia awapo na shida halisi kimwili au kiroho! Akiliandikia gazeti la L’Osservatore Romano, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano Monsinyo Lucio Adrian Ruiz anatanabaisha fadhila ya unyenyekevu katika Ulimwengu wa kidigitali mintarafu mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko. Monsinyo Lucio anasema, Baba Matakatifu Francisko anaeleza kutoka katika Maandiko Matakatifu kwamba upole unaweza kuonekana katika taswira ya familia mintarafu ‘Baba’ anayemtuma mwanaye kuja kutukomboa, ‘Mama’ mwenye upendo usiopimika kwa mwanawe, ‘Mchungaji’ anayejali kundi lake na vilevile ‘Msamaria mwema’ anayejitolea yote ili kukidhi haja ya mwitaji.

Unyenyekevu na upole unafumbatwa katika ujasiri wa kukumbana na maisha katika ukomavu wa kikristo, kuruhusu kujiweka katika kundi sawa na walio chini ili kuwainua; kupenda thabiti kusiosita kuwakaribia wahitaji, kujinyenyekesha katika kuwainua wengine na kujishujaisha kuwachomoa wengine katika madhila yao. Kupitia mitandao ya kijamii hususan instagram, Facebook na Twitter, Baba Mtakatifu Francisko amefanikiwa kugusa na kukonga nyoyo za wengi kwa maneno, vitendo na ishara zake za unyenyekevu na upole zinazoakisi huruma ya Mungu kwa watu wake. Mpaka mwishoni mwa mwaka 2018 akaunti ya twitter ya Baba Mtakatifu (Pontifex) ilipata wafuatiliaji milioni arobaini na saba (47,000,000) ikimfanya kuwa mtu wa tatu miongoni mwa watu 50 wenye ushawishi mkubwa zaidi ulimwenguni.

Ulimwengu wa leo unayo changamoto kubwa ya kung’amua fadhila mbalimbali za kurithisha kizazi cha sasa na vizazi vijavyo na vilevile namna fanisi ya kuchota mambo mema yapatikanayo katika vumbuzi na gunduzi za kisasa mintarafu maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ni wazi kwamba pande hizi mbili zinahusiana kwa karibu na kushawishiana moja kwa nyingine kwa namna mbalimbali. Mahusiano ya kawaida ya kuwa pamoja kiuhalisia; kuonana, kuzungumza na kusikiana uso kwa uso, yamezoeleka na kuchukulika kwa urahisi na watu wengi tangu kale. Lakini ulimwengu wa leo unamsukuma mwanadamu kuhusiana kupitia ‘uwepo’ katika viwezeshaji yaani vyombo vya kidigitali kama simu za mikononi, sikanu na kadhalika ambako watu huweza kuwa pamoja kubadilishana mawazo, hisia na hata mitazamo yao kupitia ishara, picha, ujumbe wa sauti taswira za kidigitali (gifs, emoji). Namna hii ya uwepo katika uwepo katika mawasiliano haiwezi tena kuhesabiwa kana kwamba imebaki katika mfumo wa kidigitali pekee kwani tayari imeingia katika mwenendo wa maisha halisi ya watu na wala sio tu kwamba imebakia mkondoni peke yake.

Maisha halisi ya mwanadamu hujumuisha pia utendaji mkondoni kwa sababu ya mitandao ya kijamii. Zaidi ya nusu ya wakaaji wote wa ulimwengu huu hivi leo ni watumiaji wa internet na mitandao ya kijamii. Vijana wengi hivi leo wanaishi kama ‘wakazi wa ulimwengu wa kidigitali’ na wanatumia lugha ya kidijitali ndani ya hili ‘Bara la kidigitali’. Katika muktadha maafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko mintarafu Upole katika ulimwengu wa kidijitali yanao umuhimu mkubwa kwani kiini chake ni kukua kwa maendeleo endelevu ya mwanadamu anayegubikwa na changamoto nyingi katika kuiandika historia yake mwenyewe ndani ya ulimwengu huu wa kidijitali. Monsinyo Lucio anabainisha kwamba mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko mintarafu unyenyekevu na upole yanaeleza kuwa sifa madhubuti za upole kwamba ni tunu ambayo lengo lake ni kumsaidia mtu kukabiliana kwa ushupavu na magumu na wala si suala linaloshawishi mtu kukwepa juu juu mateso na masumbufu ya ulimwengu pasi na kumwongoza kukabiliana katika uhalisia wa maisha. Unyenyekevu na upole ni fadhila ambayo ni kigezo muhimu kwa mkristo kuonesha ukomavu wa kikristo katika mwenendo wa ushuhuda wa maisha, licha ya magumu na changamoto za maisha.

Upole ni fadhila ya ushujaa ya kuwatazama masikini na wanyonge na kuwasaidia kujiondoa katoka hali zao duni kuliko kutumia unyonge wao kuwanyonya na kuwakandamiza kwa kujitafutia faida binafsi. Katika ujumbe wake kwa mtandao wa TED (Technology, Entertainment, Design) Baba mtakatifu Francisko alizungumzia mapinduzi ya upole akisema kwamba upole ni ule upendo unaoweza kuonjeka kwa ukaribu na uhalisia wake. Hii ni jitihada ambayo kupitia watu wote Mungu anatoka na kuwaendea wengine ili kuwa pamoja nao kupitia uwepo wa kila mmoja wetu katika kuheshimiana, kusikilizana na kusaidiana katika taabu na raha. Upole ni nguvu inayosukuma katika utendaji. Nguvu hiyo huanzia moyoni lakini haibaki hapo bali huendelea na kusukuma macho yetu kuwaona wenye shida, kuwasikia na kubidiisha mikono yetu kuwasaidia. Upole husukuma kujiweka katika hali yaw engine, hata kama ikiwa ni ya chini. Ni njia ya kujishusha ambayo Mungu mwenyewe katika Kristo Yesu anachukua ubinadamu ili aweze kumwinua mwanadamu kufika kwake. Ndicho alichofanya Msamaria mwema, kusimamisha safari yake na kuingia katika hali ya mtu yule aliyekuwa kufani kwa sababu ya kushambuliwa na wanyang’anyi.

Kristo Yesu Mwenye licha ya kuwa Mungu alijishusha na kuishi katika ubinadamu, maisha yake yote yakijitafsiri katika lugha kuu ya upendo usio na mipaka, akijitoa pasipo kujibakisha (kenosis) ambayo kwayo uhai ni huduma na wala sio kuwakandamiza wengine. Unyenyekevu na upole kadiri ya Baba Mtakatifu Francisko unafumbatwa katika lugha ya akili, moyo na mikono, ambavyo hutimilisha mlinganyo kati ya kilicho ndani ya mtu na kile akitendacho mintarafu matendo ya huruma. Katika hilo, Baba Mtakatifu analielekeza na kulitia shime Kanisa kuwa hospitali katika uwanja wa mapambano. Anasema upole ni chombo cha mwanadamu kinachomwozesha mtu kusafiri na kuzifikia hisia za ndani za mtu na kuweza kujenga mahusiano ya kweli kama watoto wa Mungu. Kama anavyosisitizia katika Waraka wake wa Kitume “Evangelii gaudium”, Baba Mtakatifu ahimiza kuutangaza ujirani wa Mungu kwa mwanadamu unaodhirisha kwamba Mungu ni Upendo. Kumbe kazi ya umisionari kwa wabatizwa wote inapata ufanisi mkubwa kupitia maneno na matendo (gestis vobisque) ambayo ndiyo pedagojia ya uinjilishaji wa kina unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Mtandao wa Internet na wadau wake unaweza kuwa ishara chanya ya nguvu na mchango wa upole katika ufanisi wa mawasiliano. Shuhuda mbalimbali zimetolewa na watu tofauti tofauti wakieleza namna wanavyoguswa na maneno, matendo yaliyojaa roho ya upole kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Mmoja wao ni Mark Zuckerberg muasisi wa mtandao wa facebook ambaye baada yay eye na mkewe kumtembelea Baba Mtakatifu Francisko, aliandika katika ukurasa wake wa facebook ”…nimemwambia Baba Mtakatifu jinsi mimi na Priscila tunavyoguswa na ujumbe wake wa Huruma na unyenyekevu na namna anavyoweza kuvumbua mbinu mpya za kuwasiliana na watu wa imani tofauti tofauti ulimwenguni”.(Chapisho la tarehe 26 Agosti 2016) Maneno na matendo yaliyofumbatwa na upole huwagusa watu wa aina zote bila kujali matabaka yao. Unyenyekevu na upole unayo nguvu kubwa ya kugusa hisia na akili ya mwanadamu. Mitandao ya kijamii ni mfereji unaoweza kusambaza huruma n aupole wa Mungu kupitia maneno, matendo na mtukio mbalimbali yenye kubeba ujumbe wa upole.

Katika hili imedhirika kwamba picha, video ujumbe wa maneno na sauti ya upole ya Baba Mtakatifu kusambazwa kwa kasi na kuwafikia wengi kupitia mitandao ya kijamii. Kupitia maneno na matendo halisi Baba Mtakatifu anajitahidi kuwashawishi watu kutilia maanani na kuweka katika utendaji ujumbe wa injili ya huruma, upole na upendo wa Mungu kwa watu. Upole unaweza kuwa kipengele msingi cha ujumbe wa injili na mrefeji wa mawasiliano hai miongoni mwa watu. Katika ulimwengu wa kidigitali, Baba Mtakatifu anawaalika watu wote, wabatizwa kwa namna ya pekee kuwa; wajenzi wa madaraja ili kuwaunganisha watu na kuwatia matumaini katika utamaduni huu mpya. Anawatakala kuwa ni Manabii ili kuhubiri ukweli, kufichua na kulaani udhalimu; Wamisionari ili kubeba huruma na furaha ya injili na kuwaendea watu popote walipo; Anawaalika kuwa ni wachungaji wema ili kuwatafuta waliopotea, wenye huzuni, waliokata tamaa na kuwarudisha. Anawahimiza kuwa ni wasamaria wema ili kupangusa na kuponya madonda ya walioumizwa na madhalimu. Anasema Baba Mtakatifu, katika zama hizi za kidigitali tunahitaji zaidi mapinduzi ya upole. Hayo yatatuokoa!