Askofu mkuu Ruzoka, alizaliwa mwaka 1948. Tarehe 20 Julai 1975 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 10 Novemba 1989 akateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma na kuwekwa wakfu na Papa Yohane Paulo II. Tarehe 25 Novemba 2006, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora na kusimikwa rasmi tarehe 28 Januari 2007.

Na Shemasi Karoli Joseph Amani, – Tabora, Tanzania.

Maisha ya utawa ni kielelezo cha kuitikia wito mtakatifu wa Mungu wa kuyatolea maisha yote yaani mwili na roho kwa huduma kwa Kanisa na watu wa Mungu. Watawa wanaweka nadhiri za utii, ufukara na usafi wa moyo wakiacha ya ulimwengu na kukita maisha yao katika sala na utume wa huduma mbalimbali kwa watu. Hayo ni matunda ya majiundo, tafakari na maandalizi ya muda wa kutosha kabla ya kuweka nadhiri zao.

 

Katika kusherehekea Sikukuu ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, hapo tarehe 16 Julai 2020, Watawa wa Shirika la Mabinti wa Maria, Jimbo kuu katoliki Tabora, wakiongozwa na Mha. Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka na Mama Mkuu Sr. Maria Theresia Sungi, wamewasindikiza wateule katika kuweka nadhiri zao.

 

Katika Makao Makuu ya Shirika huko Kipalapala Jimboni Tabora, Wateule kumi na moja (11) walijitoa kimasomaso kukabidhi maisha yao kwa Kristo Yesu na huduma ya Kanisa kwa nadhiri zao za kwanza. Nao si wengine bali ni; Sr. Albina Muchu, Sr. Letisia Nyamizi, Sr. Jenifrida Matle, Sr. Agnes Dotto, Sr. Happiness Govera, Sr. Bona Amani, Sr.Evalinana Lohi, Sr. Angelina Khwema, Sr. Lusia Manyari, Sr. Triphina Kalyamtima na Sr. Elizabeth Mkawi.

 

Hawa “walitia mkwaju” kuingia Shirikani kwa mara ya kwanza. Dada zao Wateule sita (6) “walimwaga manyanga” kumwambata na kumkumbatia Kristo Yesu kwa maisha yao yote na wakaweka nadhiri za daima nao ni; Sr. Regina Baha, Sr. Angelina Manday, Sr. Martina Tatu, Sr. Sophia Mgeni, Sr. Julietha Mchilo na Sr. Maria Goreth Kiwale.

 

Katika mahubiri yake, Mha. Askofu mkuu Ruzoka alikazia mambo msingi matatu (3). Kwanza ni juhudi kwa kila mmoja kuwania utakatifu wa maisha. Baba Askofu mkuu alisisitiza kwamba maisha ya mkristo, hususan mtawa yanapaswa kuhuishwa na unyoofu katika kumtafuta Mwenyezi Mungu. Taifa la Mungu linayo haki ya kuonja uwepo wa Mungu katika maisha matakatifu ya wakristo wote na kwa namna ya pekee watawa kwani wao ni kielelezo cha utakatifu kwa jamii yote ya waamini. Pili ni kujijengea fadhila kuu ya mapendo ambayo inaambatana na mafiga mengine mawili, yaani imani na matumaini.

 

Baba Askofu mkuu alikazia kusema “Upendo ndiyo bendera ya mkristo”. Kila mkristo anao wajibu msingi wa kuonesha ushuhuda wa imani yake kwa Kristo Yesu unaothibitika katika matendo halisi yaliyojaa upendo usio na mipaka kwa watu wote. Alisisitiza kusema, maisha ya upendo huleta neema katika utume na huduma yeyote anayoifanya mtawa.

 

Watu huvutwa zaidi kwa Kristo Yesu wanaposhuhudia mtawa akitoa huduma yake kwa furaha na mapendo makubwa haijalishi ugumu wa huduma hiyo, Kanisa la Mungu litastawi kwa sababu ya tabasamu na majitoleo adhama ya mtawa anapokuwa utumeni.

 

Tatu, Baba Askofu mkuu Ruzoka alikazia juu ya utii. Aliwaasa watawa kuhuisha utume wao kwa utii kwa viongozi wao na wale wote wanaofanya nao kazi kwani mapenzi ya Mungu hupitia katika watu, miongoni mwao ni wakuu wa Shirika na katika Kanisa lote. Baba Askofu mkuu Ruzoka aliwaasa watawa kupitia mifano mbalimbali kutoka Neno la Mungu na Maisha ya Kanisa mintarafu watakatifu mbalimbali. Akikazia imani aliasa kumtazama Ibrahimu kama mfano wa imani isiyo na kipimo hata akawa tayari kumtolea mwanae wa pekee Isaka kama sadaka kwa Mungu (Mwanzo 22:1-14).

 

Alimtaja pia Nabii Eliya kama kielelezo cha uthabiti wa msimamo katika imani kwa Mungu wa kweli licha ya upinzani wa mfalme na makuhani wa Baali (1Wafalme 18:25-39). Vilevile, alidadafua namna ambavyo maisha ya uchaji na sadaka yanalipamba Kanisa. Alimtaja Mtakatifu Yohane wa Ishirini na tatu, Papa (XXIII) kuwa ni mfano wa uzingatifu na umakini katika kutimiza majukumu yake, kwani alijitahidi kuishi upendo kwa juhudi yote; hata akathubutu kusema “Pendo langu ni kwa Mungu mwenye huruma; na huyo aliye upendo wangu ndiye aliye vilevile huruma yangu’’.

 

Alimwelezea Mtakatifu Benedikto Abate, Baba wa utawa wa magharibi kuwa ni mfano thabiti wa sala na tafakuri jadidi ya Neno la Mungu, lakini pia kuwa ni taswira ya mchapakazi mbobezi aliyejibidiisha kujilisha yeye na watawa wenzie kwa jasho lao wenyewe kupitia kazi za mikono yao, huku wakiongozwa na kauli mbiu “Ora et Labora” yaani “Sala na Kazi”.

 

Akiongelea kuhusu nadhiri ya Ufukara, Askofu mkuu Ruzoka aliwaasa watawa kuwa waangalifu na kuepuka tamaa ya mali katika utume wao. Alisema tamaa ya mali hufunga mioyo ya wafuasi wa Kristo Yesu nao hawawezi tena kuona lililo muhimu kwa maisha na utume wao. Baba Askofu alisisitiza kuzingatia umaskini wa maisha ya kiroho (Mt. 5:3), wakibidiishwa na mfano wa Mama Bikira Maria Mlinzi na mwombezi wao.

 

Sanjari  na hayo, siku ya Jumatatu tarehe 20 Julai 2020, Baba Askofu Mkuu Paulo R. Ruzoka ametimiza miaka arobaini na mitano (45) ya Upadre. Katika hafla fupi ya kumbukizi hizi uaskofuni Tabora, Baba Askofu mkuu Paulo Ruzoka amewashukuru wote waliomsindikiza na wanaoendelea kufanya hivyo, wakimwombea na kumtia moyo katika utume wake tangu akiwa Jimbo Katoliki la Kigoma na hata sasa jimboni Tabora. Alisema yeye alikuwa Padre mzalendo wa sita kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tangu kuanzishwa Jimbo la Kigoma.

 

Katika kipindi kile sehemu kubwa ya Tanzania ikiwa na mapadre wengi kutoka nje ya Afrika, haikuwa rahisi hata kidogo kwa vijana wazalendo kufuasa wito wa upadre. Lakini kijana Paulo Ruzoka, enzi hizo, hakuteteleka wala kubabaika na lolote, na kwa sala, sadaka, kujitoa na kujitolea; akafanya jamala kuonesha kwa matendo nia yake ya kumtumikia Mungu kama Padre wa Kanisa Katoliki.

 

Akitafakari juu ya safari yake ya wito wa upadre alisema kwamba miaka yake 45 ya upadre imechagizwa na tumaini kwamba mapenzi ya Mungu hayana mipaka, nayo humkaribisha kila huyo kwa namna yake.

 

Taifa la Mungu Jimboni Tabora linampongeza sana Mha. Askofu mkuu Paulo Ruzoka na kumwombea kheri la baraka tele katika kuchunga kondoo wa Bwana kama Kuhani kwa mfano wa Melkisedeki kuhani mkuu. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Paulo Ruzoka, alizaliwa kunako mwaka 1948 huko Nyakayenzi, Kigoma. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 20 Julai 1975 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa kuwekewa mikono na Askofu Alphons Daniel Nsabi wa Jimbo Katoliki la Kigoma, akiwa ni Padre wa sita mzalendo, kupewa Daraja Takatifu ya Upadre, matendo makuu ya Mungu.

 

Tarehe 10 Novemba 1989, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma na kuwekwa wakfu na Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 6 Januari 1990 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Tarehe 25 Novemba 2006, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora na kusimikwa rasmi tarehe 28 Januari 2007.