Baba Mtakatifu ametoa zawadi ya mashine ya kupumlia kwa Hospitali ya Campanha de Marabá, iliyoko nchini Brazil. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi kufikia Jumatano, tarehe 15 Julai 2020 majira ya asubuhi, watu 1,931,204 walikuwa wameambukizwa Virusi vya Corona, COVID-19. Watu 74,262 tayari wamekwisha kufariki dunia. Kuna wagonjwa 1,213,512 ambao wamelazwa nchini Brazil.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, watu wa Mungu wanapaswa kuendelea kufuata ushauri wa madaktari na wataalam wa afya pamoja na kutekeleza itifaki dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 ili mafanikio yaliyokwisha kupatikana yaweze kuendelezwa zaidi badala ya kutumbukia tena kwenye taharuki na hofu ya maambukizi mapya ya Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu ametoa zawadi ya mashine ya kupumlia kwa Hospitali ya Campanha de Marabá, iliyoko nchini Brazil. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi kufikia Jumatano, tarehe 15 Julai 2020 majira ya asubuhi, watu 1,931,204 walikuwa wameambukizwa Virusi vya Corona, COVID-19. Watu 74,262 tayari wamekwisha kufariki dunia. Kuna wagonjwa 1,213,512 ambao wamelazwa nchini Brazil. Askofu Vital Corbellini wa Jimbo Katoliki la Marabá, amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa moyo wa huruma na upendo aliouonesha.

Kwa hakika mashine hii itasaidia kuokoa maisha ya watu wengi, lakini zaidi watu mahalia. Hospitali hii imetenga wodi maalum kwa ajili ya kuwahudumia watu mahalia ambao wameambukizwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kwa bahati mbaya sana hawa ni watu ambao haki zao msingi hazipewi kipaumbele cha kwanza. Ni watu ambao wamenyang’anywa sehemu kubwa ya ardhi inayotumiwa na Makampuni makubwa ya Kimataifa kwa ajili ya shughuli za kiuchumi. Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, CNBB kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, Caritas Brazil, limeanzisha kampeni ya mshikamano wa Kanisa nchini Brazil. Kampeni hii inaoongozwa na kauli mbiu “Ni muda wa kusaidiana”. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuchangia kwa hali na mali ili kuwasaidia waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19. Tayari matunda ya kampeni hii yameanza kuonekana.  Baba Mtakatifu Francisko anasema, inawezekana kabisa, watu wa Mungu kutoka katika kipeo hiki cha mahangaiko ya maisha ya kiroho, kanuni maadili na utu wema, wakiwa imara zaidi, mambo yanayotegemea dhamiri nyofu na uwajibikaji wa kila mmoja, kwa kutegemea na kuambata neema ya Mungu.

Ni wajibu wa waamini kutangaza na kushuhudia kwamba, kamwe Mwenyezi Mungu hawezi kuwaacha waja wake, hata katika udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu. Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika Fumbo la Msalaba, hata waamini nao kwa msaada wa Mwenyezi Mungu wanaweza kupambana na matatizo na changamoto pevu, hatimaye wakaweza kuibuka kidedea! Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu ili aweze kujenga umoja na udugu wa kibinadamu, ili kuondokana na dhana ya uchoyo na ubinafsi, mambo yanayoonekana kuwa kama ni dira na mwongozo wa maisha ya walimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa angalisho kwa watu wote wa familia ya Mungu kutojisahau kwani mara tu baada ya kipeo cha janga la Corona, COVID-19 wakajikuta wakitumbukia katika ombwe na hali ya kufikirika. Ni rahisi sana kuwasahau majirani; au watu wengine wanaowahudumia; lakini wakumbuke kwamba, kuna watu wanaowatia shime na ujasiri wa kuweza kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu!

CHANZO: www.vaticannews.va