Neno la Bwana likamjia Eliya Mtishbi, kusema, Ondoka, ushuke, ukutane na Ahabu mfalme wa Israeli, akaaye katika Samaria; yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ndiko alikoshukuia ili alitamalaki. Ukamwambie, ukisema, Bwan aasema hivi, Je! Umeua, ukatamalaki? Nawe utamwambia, kusema, Bwana asema hivi, mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba na damu yako, naam, damu yako.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 51:1-4, 9, 15 (K) 1
(K) Ee Mungu uturehemu uyafute makosa yetu.
Ee Mungu unirehemu, sawasawa na fadhili zako.
Kiasi cha wingi wa rehema zako,
Uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa na uovu wangu,
Unitakase dhambi zangu. (K)
Maana nimejua mimi makosa yangu,
Na dhambi yangu i mbele yangu daima.
Nimekutenda dhambi Wewe peke yako. (K)
Usitiri uso wako usitazame dhambi zangu,
Uzifute hatia zangu zote.
Ee Bwana, uifumbue midomo yangu,
Na kinywa hcangu kitazinena sifa zako. (K)
SHANGILIO
Yak. 1:21
Aleluya, aleluya.
Pokeeni kwa upole neno la mungu lililopandwa ndani, liwezalo kuiokoa roho zenu.
Aleluya.
INJILI
Mt. 5:43 – 48
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, pendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi; ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyk, mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru; je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Karibuni ndugu zangu kwenye tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Leo tafakari hii inaanza kwa kuitazama zaburi ya wimbo wetu wa katikati. Hapa tunaikuta zaburi ya maombolezo ya mtu akiomba msamaha. Aliyeomba huu msamaha alikuwa ni Daudi. Yeye baada ya kufanya dhambi kubwa: baada ya kuzini na mke wa askari wake na kutaka kuifunika dhambi hii ili iwe siri, aliamua kumwua yule askari wake ili kuzuia asipate heshima mbaya mbele ya taifa lote la Israeli. Kweli hili lilikuwa kosa kubwa sana na ubinafsi mkubwa sana-kutaka kuficha heshima yako kwa kutumia uhai wa mwingine-Mungu alikasirishwa sana na kosa hili kwani Daudi alionesha ubinafsi na unyama wa hali ya juu. Hivyo, alidhamiria kumwangamiza Daudi. Lakini cha ajabu ni kwamba Daudi alimlilia Mungu usiku na mchana akimuomba msamaha na Mungu akabadili mawazo yake.
Sasa leo kwenye masomo yetu aliyetenda makosa makubwa hivi kama Daudi na baadaye kumlilia Mungu na kupata msamaha ni mfalme Ahabu. Yeye alishiriki katika kumwua yule maskini Nabothi na kuchukua shamba lake. Ahabu hakumzuia mke wake Jezebeli kutokumdhuru Nabothi. Yeye aliruhusu mke wake kumdhuru Naboth na hakumpatia Nabothi ulinzi. Hivyo, nabii Elia alitumwa kumtangazia adhabu huyu Ahabu na mke wake. Lakini cha ajabu kweli Mungu anahuruma. Kitendo cha Ahabu kumlilia Mungu kilimfanya Mungu kubadili mawazo na licha ya dhambi zake zote. Mungu alikuwa tayari kumsamehe Ahabu. Lakini Jezebeli hakujiangusha miguuni mwa Mungu na hivyo Mungu hakuonesha msamaha kwake.
Hapa ndugu zangu twajifunza juu ya huruma ya Mungu kwa mtu mnyenyekevu. Hakuna ajiangushaye miguuni mwa Mungu akiomba msamaha na halafu kuachwa hivihivi. Yaani ukimlilia Mungu kwa unyenyekevu, anabadili hata adhabu kubwa kabisa alizokuwa kadhamiria. Basi sisi ndugu zangu tumlilie Bwana. Kweli tunamatatizo mengi. Tumlilie Bwana, tusiyaache yatutese tu. Tuyapeleke kwa Bwana. Yaani Mungu hamwachi mnyenyekevu aumbuke.
Lakini aliye na majivuno mbele ya Mungu kwa hakika huumbuka kila siku; Mungu hapendi majivuno. Hakuna aliye na majivuno aliyewahi kupita mbele ya Mungu. Mke wa Ahabu-Yezebeli na majivuno yake alikataa kumwomba Mungu msamaha na kwa kweli aliangamizwa kwa mauti ya fedheha sana licha ya kwamba hapo mwanzo alijivuna sana. Nasi tuepuke chembe yoyote ya majivuno.
Halafu ndugu zangu tutambue kwamba ni wajibu wetu kuwalinda hasa wale walio wadogo na maskini wasio na wa kuwasaidia na kuwatetea. Lazima tuwalinde na tusikubali wakandamizwe na wale wanao onekana kwamba wananguvu.
Pia somo hili linatoa somo kwa akina mama na akina dada wanaotumia nafasi za waume zao au wazazi wao vibaya. Yezebel alitumia nafasi ya mume wake kama mfalme kuangamiza wengine. Sisi kama akina mama tusije kukumbwa na kiwewe na kutumia utajiri au cheo cha waume zetu kwenye kukandamiza watu. Hili tuepuke sana.
Katika injili, Yesu leo anatushauri pia kuwapenda maadui wetu-anazungumza kwamba yabidi tujishushe, tuwe na upendo hata kwa wale ambao machoni petu ni adui. Hapa twaweza kusema kwamba anawaasa hata wale wanaotendewa ubaya kwamba nao pia waepukane na majivuno. Wawe tayari kuwapenda maadui wao ambao hapo mwanzo waliwatesa. Hili ni muhimu kwa sababu dunia hii ni kupanda na kushuka. Hata yule aliyekuwa na pesa za kutosha na kuwatesa watu anaweza kugeuka na kuwa maskini mara moja na kumkuta ndiye maskini na wale walioteswa ndio wapo juu. Sasa, hairuhusiwi ati hawa walioteswa waanze nao kutesa wenzao. Sio hivyo, msamaha unahitajika-usiwarudishie ovu wale waliokutesa zamani. Lazima tubakie wanyenyekevu daima. Tumsifu Yesu Kristo.
:copyright:Pd. Prosper Kessy OFMCap.
Albert Byellengoadmin
https://youtu.be/ca75mUw90LY