SOMO 1 ..1 Fal. 21:1-16
Nabothi Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu katika Yezreeli, karibu na nyumba ya kifalme ya Ahabu mfalme wa Samaria. Ahabu akasema na Nabothi, akamwambia, Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, maana ni karibu na nyumba yangu; nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu lililo zuri zaidi; au ukipenda, nitakupa fedha sawasawa na thamani yake. Nabothi akamwambia Ahabu, Bwana apishe mbali nikupe urithi wa baba zangu.
Wale wazee wa mji wake, na walio wenye nguvu waliokaa mjini mwake, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza, kama ailivyoandikwa katika nyaraka alizowapelekea. Wakapiga mbiu ya watu kufunga, wakamweka Nabothi juu mbele ya watu. Na hao watu wawili, watu wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana Mungu na mfalme. Ndipo wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa.
Wakampelekea Yezebeli habari, wakasema, Nabothi amepigwa kwa mawe, amekufa. Ikawa Yezebeli aliposikia ya kwamba Nabothi amepigwa kwa mawe na kufa, Yezebeli akamwambia Ahabu, Inuka, ulitamalaki shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, alilokataa kukupa kwa fedha, maana Nabothi hako hai, lakini amekufa. Ikawa Ahabu aliposikia ya kwamba Nabothi amekufa, akaondoka, alitelemkie shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, ili alitamalaki.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 5:2-3, 5-7 (K) 2
(K) Uisikie sauti ya kilio changu, ee Bwana.
Uisikie sauti ya kilio changu,
Ee Mfalme wangu na Mungu wangu,
Kwa maana Wewe ndiwe nikuombaye.
Bwana, asubuhi utaisikia sauti yangu,
Asubuhi nitakupangia dua yangu na kutazamia. (K)
Wajivunao hawatasimama mbele za macho yako;
Unawachukia wote watendao ubatili.
Utawaharibu wasemao uongo;
Bwana humzira mwuaji na mwenye hila. (K)
Bali mimi, kwa wingi wa fadhili zako,
Na kusujudu kwa kicho,
Nikielekea hekalu lako takatifu. (K)
SHANGILIO
Kol. 3:16, 17
Aleluya, aleluya,
Neno la Kristu likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote;
Mkimshukuru Mungu Baba kwa Yeye.
Aleluya.
INJILI
Mt. 5:38 – 42
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mmesikia kwamba imenenwa Jicho kwa jicho, na jino kwa jino; lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili. Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili. Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Leo tafakari yetu inaanzia katika zaburi ya wimbo wa katikati na hapa tunakutana na zaburi ya Daudi. Daudi akilia akimuomba Mungu asikilize ukelele wa sauti yake. Hii ni sala aliyoisali kwa nguvu sana alivyokuwa kazungukwa na hatari kubwa iliyotaka kuteketeza maisha yake. Miongoni mwa hatari kali zilizomzunguka Daudi, ni ile ya Sauli kuingia ndani ya pango alilokuwa kajificha na hivyo ama kweli Daudi alitetemeka sana kuona hili. Alivyokuwa kule ndani, hakika alisali sana kuomba Mungu ampe usalama dhidi ya adui huyu aliyekuwa na nguvu za kipesa, kijeshi na kifalme.
Lakini basi leo kwenye masomo yetu, anayelia ni Maskini mmoja aitwaye Nabothi. Yeye alikataa kuuza shamba la wazazi wake, shamba lililokuwa urithi kwake na lilikuwa na vitu kama makaburi ya wazazi wake. Na hivyo aliona ni aibu kwa kizazi chake chote kama angaliliuza shamba ili ati kwa sababu tajiri mmoja alitaka kutengeneza shamba la mizabibu. Tajiri huyu angaliweza kwenda kutengeneza shamba hili mahali pengine. Lakini basi yeye anakataa na hapohapo basi habari zinamfikia mke wa mfalme anayeamuru huyu Nabothi auawe na shamba kuchukuliwa. Nabothi alipokuwa anauawa, alitoa kilio kikali sana kwa Mungu kumwomba amsadie. Kilio hiki kweli kilijibiwa na Mungu kwani huyu Ahabu na yule mke wake walioamuru kifo cha huyu mtu, waliishia kupewa adhabu kali kabisa; jambo hili liliwafanya nao wapewe hukumu zilizogharimu maisha yao.
Ndugu zangu, kwa nyakati zetu tumeshuhudia wengi wakidhulumu sana. Kuna viongozi wanaopewa fedha za maendeleo ya nchi wanaishia kuzitapanya. Wengine wanapewa pesa za maendeleo ya shule au hospitali au kwenye kununua dawa za hospitali na wao wanazila. Wengine wanahamisha hata madawa ya hospitali kwenye pharmacy zao. Na tunawaona wanaofanya hivi kuwa ni wajanja wazuri sana.
Ndugu zangu, tuwe makini: tukumbuke kwamba kilio cha hawa wote wanaokosa huduma wakitulilia na hicho kilio kikitua mbele za Mungu, hakika tutaishia pabaya sana. Wengi tunalaaniwa kutokana na mambo kama haya. Dhuluma ni hatari. Kama baba kadhulumiwa na labda kafukuzwa kazini-na yeye akamlilia Mungu, na watoto wake na mke wake wakajiunga naye kumlilia Mungu, unafikiri kwamba aliyedhulumu atakuwa salama kweli? Jamani, tuache tabia hizi. Hizi ni laana. Wengi wetu tusiwe hivi.
Katika injili tunakutana na Yesu akitufundisha kwamba tusionyeshe jino kwa jino. Mtu akikupiga kofi shavu hili geuza na jingine. Yesu anapofundisha hivi sio kwamba anataka wanyonge waonewe Zaidi. Tujue kwamba hapa ndio atakavyoweza kushughulika vizuri na wale wanaonea wengine kama akina Ahabu na Mke wake. Tujue kwamba mtetezi wa wadogo ni Mungu. Hakika yeye atawatetea tu. Hivyo, tusiwadhulumu. Tumsifu Yesu Kristo.
:copyright:Pd Prosper Kessy OFMCap.