Tanzania leo imepokea msaada wa dawa zinazofubaza Virusi vya #Corona kutoka Serikali ya Madagascar. Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataia, Prof Palamagamba Kabudi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) kwa niaba ya Tanzania leo Mei 8, 2020 amepokea msaada wa dawa zinazofubaza Virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19 kutoka Serikali ya Madagascar.

Prof. Kabudi amesalimi Madagascar leo na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar, Tehindrazanarivelo Djacoba As Oliva katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Antananarivo.

Msemaji Mkuu wa Serikali Ya Tanzania Dkt. Abbasi amethibitisha hilo na kusema; ”Tanzania leo imepokea msaada wa dawa zinazofubaza Virusi vya Corona kutoka Serikali ya Madagascar.” iliandikwa kwenye Twitter.

Dawa hizo zinawasili Tanzania wakati ambapo nchini Madagascar kwenyewe idadi ya wagonjwa wa corona inaripotiwa kuongezeka. Kufikia taifa lio lina jumla ya watu 195 walioambukizwa corona licha ya kutangaza kuwa na dawa ya mitishamba iliyo na uwezo wa kutibu ugonjwa huo.

Mnamo Mei 3, Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli alisema kuwa atatuma ndege Madagascar kwenda kufuata dawa ya hiyo mitishamba. Wakati huo Rais Magufuli alisema kuwa amewasiliana na Madagascar baada ya kupokea barua rasmi kutoka nchi hiyo iliyoeleza kuwa wamegundua dawa ya corona.

Shirika la Afya Duniani limesema ni muhimu dawa zinazosemekana kuwa na uwezo wa kutibu kufanyiwa majaribio kwanza na kuonya kuwa huenda watu wakaona wamepata tiba na kujihisi kuwa salama ikiwa watakuwa na imani na dawa ambazo hazijafanyiwa majaribio.