Sikukuu ya Wafanyakazi 2020 ni changamoto ya kusimama na kuanza tena upya, ili kufufua shughuli za kiuchumi, uzalishaji na ugavi. Wafanyakazi katika sekta ya umma na binafsi wanahamasishwa kujifunga kibwebwe ili kuchangia katika mchakato wa ufufuaji wa uchumi katika ngazi mbali mbali. Wafanyakazi wajitahidi kuchangia: juhudi, maarifa pamoja na kuzingatia nidhamu na uwajibikaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani kwa Mwaka 2020, maarufu kama Mei Mosi, inaadhimishwa wakati Jumuiya ya Kimataifa inakabiliana na changamoto kubwa kutokana na athari za Janga la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID. Binadamu amejifunza na kuona udhaifu wake kutokana na maafa makubwa yanayoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia, kwa watu kuambukizwa, kufariki dunia na wenye bahari zao kama mtende kupona na kurejea tena katika maisha ya kawaida. Katika Janga hili wafanyakazi katika sekta ya afya wamekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kuokoa maisha ya watu. Dhana ya kazi ulimwenguni imebadilika na kupata mwelekeo mpya na haitakuwa rahisi tena kurejea katika mazoea ya miaka iliyopita.

 

Askofu mkuu Antonio Caiazzo wa Jimbo kuu la Matera nchini Italia katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani kwa Mwaka 2020 inayoongozwa na kauli mbiu “Kazi katika uchumi ambayo ni fungamani” anasema kwamba, Virusi vya Corona, COVID-19 ni Janga la Kimataifa linalowaathiri watu wote katika ajira na uzalishaji wa mali na huduma kwa watu wa Mungu. Kwa upande wa Italia, hali imekuwa ni ngumu kutokana na ukweli kwamba, kumekuwepo na uhaba mkubwa wa fursa za ajira nchini Italia, kiasi cha kuwasukuma vijana wa kizazi kipya nchini Italia, kutoka ili kwenda kutafuta malisho ya kijani kibichi sehemu nyingine za dunia. Vijana wengi wamekata tamaa kuhusu leo na kesho yao mintarafu maisha ya ndoa na familia na matokeo yake, kuna idadi ndogo sana ya watoto wanaozaliwa nchini Italia.

 

Ugonjwa wa Corona, COVID-19 umesababisha vifo vya watu wengi nchini Italia na kwamba, kuna idadi ya kubwa ya wananchi ambao wameambukizwa na bado wanaendelea na tiba! Kumbe, Sikukuu ya Wafanyakazi kwa Mwaka 2020 ni changamoto ya kusimama na kuanza tena upya, ili kuhakikisha kwamba, shughuli za kiuchumi, uzalishaji na ugavi zinarejea tena katika hali yake ya kawaida. Wafanyakazi katika sekta ya umma na binafsi wanahamasishwa kujifunga kibwebwe ili kuweza kuchangia katika mchakato wa ufufuaji wa uchumi katika ngazi mbali mbali, kuanzia uchumi wa familia hadi uchumi wa Kimataifa. Kwa hakika mambo yamebadilika sana na wala hakuna sababu ya kukata wala kujikatia tamaa, bali Serikali ijitahidi kuwawezesha wananchi wake kiuchumi, ili waweze kuanza tena upya kuchakarika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kila mtu kwa nafasi yake, ajitahidi kuchangia, juhudi, maarifa pamoja na kuzingatia nidhamu na uwajibikaji kazini.

 

Askofu mkuu Antonio Caiazzo anasema, Janga la Virusi vya Corona, COVID-19 lisiwe ni sababu ya watu kupoteza fursa za kazi na ajira. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ni kwa njia ya kazi inayofanywa kwa uhuru, kwa ubunifu, kwa kushirikiana, kusaidiana na kushikamana na wengine, ndivyo wanadamu hudhihirisha na kuendeleza heshima ya maisha yao. Kuna haja kwa Serikali na Kanisa kuendelea kushirikiana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, daima utunzaji wa mazingira nyumba ya wote ukipewa kipaumbele cha pekee. Waraka wa Kutume wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, “Laudato si” ni muhatasari wa Mafundisho Jamii ya Kanisa kuhusu kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amedhaminisha kuitunza na kuiendeleza na kwamba, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kusimama kidete kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote. Kanisa katika yote haya linakazia kuhusu utu na heshima ya binadamu, mafao ya wengi yanayoongozwa na kanuni maadili; mshikamano unaojengeka katika kanuni auni; haki na amani; mambo ambayo yanaweza kuchunguzwa kwa kuangalia changamoto za Makanisa mahalia!