Kanisa Katoliki nchini Italia linasikitika kutangaza vifo vya watu 9,134 kati yao kuna Mapadre zaidi ya 60 na Askofu mmoja waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Watu 66,414, walikuwa wameambukizwa na wengine 10,950 wamepona kutokana na ugonjwa wa Corona hadi kufikia tarehe 28 Machi 2020, majira ya 12:00 jioni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kama binadamu Mapadre wanatambua udhaifu na uwepo wa dhambi katika maisha na utume wao; changamoto ya kutubu na kuongoka, ili kuanza hija ya utakatifu inayokita mizizi yake katika mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu. Mapadre wanapaswa kuwa ni wachungaji wema, kwa mfano wa utakatifu wa maisha yao, wawasaidie waamini walei kuiona njia ya hija ya utakatifu wa maisha, kwa kukazia umoja, maisha ya kisakramenti, kazi na utume wa mashirika na vyama mbali mbali vya kitume parokiani, bila kusahau, nidhamu na wajibu wa kila mwamini. Uaminifu wa Mapadre na walei uwawezeshe kuuona utakatifu, kwa njia ya maisha ya kisakramenti, liturujia na sala, kila upande ukijitahidi kutekeleza wajibu wake. Katika Maadhimisho ya Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney, Baba Mtakatifu Francisko aliwaandikia Mapadre wote duniani, barua ya upendo na mshikamano wa kibaba, akiguswa na furaha ya huduma inayotolewa na Mapadre sehemu mbali mbali za dunia, kila kukicha!

Hawa ni mapadre ambao wengine wamechoka na kudhohofu kwa afya mbaya na changamoto za maisha; kuna baadhi yao wametumbukia katika mateso na mahangaiko makubwa ya ndani kutokana na huduma yao kwa familia ya Mungu. Licha ya mambo yote hayo, Baba Mtakatifu anasema, Mapadre wanaendelea kuandika kurasa za maisha na utume wa Kipadre sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu katika barua hii anapenda kuwashukuru na kuwatia moyo Mapadre, wote wakitambua kwamba, wao kwa hakika ni marafiki wa Kristo Yesu katika maisha na utume wao. Baba Mtakatifu anasema, kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale, ameyaona mateso na mahangaiko ya watu wake, anasema haachi kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Mapadre, akiwakumbuka katika sala zake; anataka kuwafariji wote katika nyoyo zao, ili hatimaye, waweze kuimba ukuu na utukufu wa Mungu katika maisha yao.

Katika moyo huu wa shukrani huzuni na majonzi makubwa, Kanisa nchini Italia linasikitika kutangaza vifo vya watu 8, 163 kati yao kuna Mapadre zaidi ya 60 na Askofu mmoja ambao wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Watu 62,013, walikuwa wameambukizwa na wengine 1,0361 wamepona kutokana na ugonjwa wa Corona hadi kufikia tarehe 26 Machi 2020, majira ya saa 12:00 za Jioni kwa saa za Ulaya. Katika orodha hii kuna idadi ya watawa tisa ambao wengi wao wamefariki dunia baada ya sadaka na majitoleo yao kwa wagonjwa na wazee. Kanisa linamlilia kwa namna ya pekee kabisa Askofu Angelo Moreschi wa Vikarieti ya Gambella, iliyoko nchini Ethiopia. Askofu Angelo Moreschi amefariki dunia tarehe 25 Machi 2020 akiwa na umri wa miaka 67.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia linaungana na watu wote wa Mungu kumwombea Marehemu Askofu Angelo Moreshi, anayesadikiwa kuwa ni Askofu wa kwanza kufariki kwa ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Ni Askofu aliyejisadaka kwa ajili ya utume miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Askofu Angelo Moreschi alizaliwa tarehe 13 Juni 1952 huko Nave, Brescia. Baada ya malezi na majiundo yake ya kitawa kwenye Shirika la Wasalesian wa Don Bosco, tarehe 15 Agosti 1980 akaweka nadhiri za daima. Kumbe, amemtumikia Mungu kama Msalesiani kwa muda wa miaka 46. Tarehe 2 Oktoba 1982 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kama Padre ametekeleza wajibu wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa miaka 38. Tarehe 5 Desemba 2009, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akatemteua kuwa Askofu wa Vikarieti ya Gambella, nchini Ethiopia na kuwekwa wakfu tarehe 31 Januari 2010. Amefariki duniani tarehe 25 Machi 2020 akiwa amelitumia Kanisa kama Askofu kwa muda wa miaka 10

Baba Mtakatifu anasema haachi kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wito wa Upadre kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambao si kwa mastahili yao wenyewe, bali wameitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kipindi cha shida na magumu ya maisha, iwe ni fursa ya kurejea tena katika zile nyakati angavu za sadaka na huduma kwa watu wa Mungu, ili kugundua tena neema za Mungu katika maisha na utume wao, ili kuwasha tena furaha inayokita mizizi yake katika unyenyekevu, ili kamwe majonzi na uchungu wa moyo, yasizime ile furaha na uungwana! Huu ni wakati wa kusimama tena na kusema, Mimi hapa Bwana, nipe nguvu ya kusimama tena ili nitoe huduma kwa watakatifu majirani; tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Mapadre wazee wagundue tena ndani mwao, ile furaha waliyokuwa wanapata walipozitembelea familia za Kikristo; walipokuwa wanakwenda kutoa Sakramenti za Kanisa kwa wazee na wagonjwa.

Mapadre watambue kwamba, wamepakwa mafuta ya wokovu, ili kuwahudumia jirani zao na kamwe wasikate tamaa, ndiyo maana anasema, kamwe haachi kumtolea Mwenyezi Mungu shukrani kwa ajili yao. Mapadre watambue udhaifu wao wa kibinadamu, karama na neema walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu, ili kuweza kuamua na kutenda kwa ukarimu. Mapadre waendelee kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, kwa sababu huruma ya Mungu yadumu milele. Moyo wa shukrani ni silaha madhubuti inayowawezesha kutafakari ukarimu wa Mungu katika maisha yao, mshikamano, msamaha, subira, uvumilivu na upendo, kiasi hata cha kuthubutu kusema kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro, “Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi”, lakini Kristo Yesu akamwambia “Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu” kwa sababu huruma yake yadumu milele!

Source: https://www.vaticannews