Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Watanzania kutotishwa na janga la ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19) na badala yake waendelee kuchapa kazi na kujenga uchumi huku wakizingatia tahadhari zote za kujikinga kuambukizwa ugonjwa huo kama zilivyotolewa na wataalamu.

 

Mhe. Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 22 Machi, 2020 alipohudhuria Ibada ya Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, iliyoongozwa na Paroko wa Parokia hiyo Padre Onesmo Wisi.

 

Katika salamu zake katika Ibada hiyo, Mhe. Rais Magufuli amesema kuwepo kwa ugonjwa wa Corona isiwe sababu ya kutishana kiasi cha kumsahau Mwenyezi Mungu, hivyo ametoa wito kwa Wakristo na Waumini wa madhehebu mengine kumrudia Mwenyezi Mungu ili aepusha janga hili, badala ya kumwacha shetani atawale.

 

Mhe. Rais Magufuli amekemea tabia za baadhi ya watu wanaofanya mzaha juu ya ugonjwa huu ama kuwatia hofu wananchi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, na badala yake ametaka Watanzania waendelee kuchapa kazi huku wakizingatia tahadhari.

 

“Watu tusitishane, tunatishana mno. Niwaombe ndugu Wakristo na Watanzania kwa ujumla wa Madhehebu yote, huu ndio wakati mzuri sana wa kumtegemea Mungu kuliko wakati wote, tuendelee kuchapa kazi, tuendelee kuujenga uchumi wetu, hatuwezi kusalimu amri kwa ugonjwa huu wa Corona na kushindwa kumtegemea Mungu na tukashindwa kuendeleza uchumi wetu” amesema Mhe. Rais Magufuli.

 

Amewashukuru viongozi wa Dini kwa kuungana na Serikali katika kuwahamasisha wananchi kuchukua tahadhari na ametoa wito kwa viongozi hao kuendelea kuliombea Taifa ili Mwenyezi Mungu aepushe balaa hili la Corona.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
22 Machi, 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa amejumuika pamoja na waumini wengine wa Kanisa la Mtakatifu Paulo wa Msalaba Jimbo kuu la Dodoma katika Ibada ya jumapili iliyoongozwa na Paroko wa kanisa hilo Padre Onesmo Wissi, ambapo Mhe. Rais amewataka Watanzania kutotishwa na ugonjwa Corona na badala yake wamtangulize Mungu mbele kwa Maombi huku wakizingatia tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huo. Machi 22, 2020.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Sakramenti Takatifu, alipoungana na waumini wengine wa Kanisa la Mtakatifu Paulo wa Msalaba Jimbo kuu la Dodoma katika Ibada ya jumapili iliyoongozwa na Paroko wa kanisa hilo Padre Onesmo Wissi, ambapo Mhe. Rais amewataka Watanzania kutotishwa na ugonjwa Corona na badala yake wamtangulize Mungu mbele kwa Maombi huku wakizingatia tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huo. Machi 22, 2020
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Padre Onesmo Wiss wa Kanisa la Mtakatifu Paulo wa Msalaba Jimbo kuu la Dodoma bila kushikana mikono wakati wa ibada ya jumapili iliyoongozwa na Paroko huyo, ambapo Mhe. Rais amewataka Watanzania kutotishwa na ugonjwa Corona na badala yake wamtangulize Mungu mbele kwa Maombi huku wakizingatia tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huo. Machi 22, 2020