Benki Kuu ya Tanzania leo Machi 19, 2020 imewatoa hofu wananchi kuhusiana na maambukizi ya virusi vya corona kupitia noti za pesa, ikisema kuwa noti hizo zimetengenezwa kwa namna ambayo zinaweza kuzuia vimelea kusalia kwenye noti.

 

Taarifa hiyo ya Benki Kuu ya Tanzania, imekuja kipindi ambapo kumekuwa na sintofahamu kuhusu maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona viitwavyo COVID-19 kupitia noti hizo ambazo zinapita na kushikwa na mikono ya watu katika manunuzi ya bidhaa na huduma mbalimbali.

 

Kwa mujibu wa mamlaka zinashoshughulika na afya zilitoa maelekezo kwa watu waepuke kusalimiana kwa kushikana mikono au kugusana licha ya kutosema chochote kuhusu noti za pesa ambazo hushikwa kwa mikono ya watu hao wanapofanya manunuzi ya vitu na huduma mbalimbali.

 

Benki Kuu imetoa ufafanuzi kuhusu hilo ikisema kuwa, licha ya usalama uliopo kwenye noti hizo bado inasisitiza wananchi kuzingatia miongozo mbalimbali inayotolewa na mamlaka zenye dhamana ya afya ya jamii.

 

“Hata hivyo kwa kuwa noti hizo zinapita katika mikono mingi, tunawashauri wananchi kuzingatia miongozo mbalimbali inayotolewa na mamlaka zenye dhamana ya afya ya jamii, ikiwa ni pamoja na kunawa mikono mara kwa mara, kutumia maji yanayotiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono (Sanitizers), kufanya hivyo kutasaidia kuua vimelea kwenye mikono.” Ilisema taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania.

 

Hata hivyo Benki Kuu imewashauri wananchi kufanya miamala kwa kutumia njia mbadala za malipo kama vile simu za mkononi, intaneti na kadi bila kulazimika kufika kwenye kaunta za benki au ATM kuchukua noti.

Benki Kuu imewataka wananchi kupuuza taarifa zinazosambazwa mitaani, ambazo hazina vyanzo vya uhakika zinazohusisha noti za benki hiyo na usambaaji wa virusi vya ugonjwa wa corona.

 

Ugonjwa wa corona ambao ni tishio duniani ulitangazwa kuingia hapa nchini Machi 16, 2020 kwa mgonjwa wa kwanza kupatikana jijini Arusha na wagonjwa wengine raia wa kigeni wawili, mmoja Zanzibar na mwingine jijini Dar es Salaam.

 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliutangazia umma kuwa hadi sasa Tanzanian ina jumla ya wagonjwa watatu wenye virusi vya ugonjwa wa corona (COVID-19).