MWANZO: Zab. 25:15 – 16… Macho yangu humwelekea Bwana daima, naye atanitoa miguu yangu katika wavu. Uniangalie na kunifadhili, maana mimi ni mkiwa na mteswa.

SOMO 1
Kut. 17:3 – 7

Watu wakawa na kiu huko; nao wakamnung’unikia Musa, wakasema, Mbona umetupandisha kutoka Misri, kutuua sisi na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu? Musa akamlilia Bwana, akisema, Niwatendee nini watu hawa? Bado kidogo nao watanipiga kwa mawe.

Bwana akamwambia Musa, Pita mbele ya watu, ukawachukue baadhi ya wazee wa Israeli pamoja nawe; na ile fimbo yako ambayo uliupiga mto kwayo, uitwae mkononi mwako, ukaende. Tazama, nitasimama mbele yako huko, juu ya lile jabali katika Horebu; nawe utalipiga jabali, na maji yatatoka, watu wapate kunywa.
Musa akafanya hivyo mbele ya wazee wa Israeli. Akapaita mahali pale jina lake Masa, na Meriba; kwa sababu ya mateto ya wana wa Israeli, na kwa sababu walimjaribu Bwana, wakisema, Je! Bwana yu kati yetu au sivyo?

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 95:1 – 2, 6 – 9 (K) 8

(K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! Msifanye migumu mioyo yenu.

Njoni, tumwimbie Bwana,
Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
Tuje mbele zake kwa shukrani,
Tumfanyie shangwe kwa zaburi. (K)

Njoni, tuabudu, tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake. (K)

Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu;
Kama vile huko Meriba,
Kama siku ya Masa Jangwani.
Hapo waliponijaribu baba zenu,
Wakanipima, wakayaona matendo yangu. (K)

SOMO 2
Ru. 5:1 – 2, 5 – 8

Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika Imani, na tuwe na Amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya Imani kuifikia neema hii ambayo tunasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu.
Na tumanini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi. Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu. Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema. Bali Mungu aonyeshe pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.

SHANGILIO
Yn. 4:15

Bwana, hakika wewe ndiwe Mwokozi wa ulimwengu, unipe maji yale ya uzima, nisione kiu kamwe.

INJILI
Yn. 4:5 – 42

Yesu alifika kunako mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu, mwanawe. Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu amechoka kwa safari yake, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita. Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe. Kwa maana wanafunzi wake wamekwenda mjini kununua chakula. Basi yule mwanamke Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? (maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria).
Yesu akajibu, akamwambia, Kama ungalijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai.
Yule mwanamke akamwambia, Bana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata wapi hayo maji yaliyo hai? Je! Wewe u mkubwa kuliko baba yetu, Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na wanyama wake?
Yesu akajibu, akamwambia, Kila anyway maji haya ataona kiu tena; walakini yeyote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.
Yule mwanamke akamwambia, Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka.
Yesu akamwambia, Nenda kamwite mumeo, uje naye hapa. Yule mwanamke akajibu, akasema, Sina mume. Yesu akamwambia, Umesema vema, Sina mume; kwa maana umekuwa na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako; hapo umesema kweli. Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii! Baba zetu waliab

udu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia. Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu. Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi. Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli. Yule mwanamke akamwambia, Najua ya kuwa yuaja Masihi, (aitwaye Kristo); naye atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote. Yesu akamwambia, Mimi ninayesema nawe, ndiye.
Mara hiyo wakaja wanafunzi wake, wakastaajabu kwa sababu alikuwa akisema na mwanamke; lakini hakuna aliyesema, Unatafuta nini? Au, Mbona unasema naye? Basi yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake mjini, akamwambia watu, Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda. Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo? Basi wakatoka mjini, wakamwendea.
Huko nyuma wanafunzi wakamsihi wakisema, Rabi, ule. Akawaambia, Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi. Basi wanafunzi wake wakasemezana, Je! Mtu amemletea chakula? Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake. Hamsemi ninyi, Bado miezi mine, ndipo yaja mavuno? Tazama, mimi nawaambieni, Inueni macho yenu myatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno. Naye avunaye hupokea mshahara, na kukusanya matunda kwa uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wapate kufurahi pamoja. Kwa maana hapo neno hilo huwa kweli, Mmoja hupanda akavuna mwingine. Mimi naliwatuma myavune yale msiyoyataabikia; wengine walitaabika, nanyi mmeingia katika taabu yao.
Na katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke, aliyeshuhudia kwamba, Aliniambia mambo yote niliyoyatenda. Basi wale Wasamaria walipomwendea, walimsihi akae kwao; naye akakaa huko siku mbili. watu wengi zaidi wakaamini kwa sababu ya neno lake. Wakamwambia yule mwanamke, Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

“MBEGU ZA UZIMA”
Tafakari ya Kwaresima
Jumapili, Machi 15, 2020.
Juma la 3 la Kwaresima

Kut 17: 3-7;
Zab 95: 1-2, 6-9;
Rum 5: 1-2, 5-8;
Yn 4: 5-42.

UNA KIU?

“Gods must be crazy” Ni jina la filamu na ni juu ya watu walioko katika Jangwa la Kalahari. Filamu hii inaonesha wazoefu wa jangwa. Mmoja wa watu hawa alitembelea mabubujiko ya maji ya Tungela (maporomoko makubwa ya maji Afrika), huko Afrika kusini. Alishangazwa kuona maji makubwa yanashuka kutoka juu. Alisimama pale kwa masaa akishangaa. Hawa watu waliopo Kalahari walizoea kukusanya maji kutoka katika majani (umande) au kupata maji kutoka katika aina ya mmea ambao shina lake huwa na maji, ili kupooza kiu yao. Kama ilivyo katika simulizi hilo, lirtujia ya leo ya Domini ya tatu ya Kwaresima inatuonesha kwamba sisi wote tuna kiu. Watu wana kiu ya fedha, anasa, madaraka, na mali, na hata kama akipata nyingi, bado kiu ni kubwa. Katika hali nyingine kuna “maji ya uzima” upande mwingine ndani ya Yesu Kristo. Tunapojiandaa wenyewe kuingia katika mafumbo ya mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo kipindi hiki cha Kwaresima, tunaitwa leo tutulize kiu yetu ya kiroho na kutuliza kiu ya Yesu anayezitafuta roho zetu na ana zisubiri zirudi kwake. Yesu alipata kiu ya mwanadamu kumrudia Mungu, na hivyo akasema pale msalabani “Nina kiu”.

Katika somo la kwanza tunaona Waisraeli wanao lalamika. Watu hawa hawa waliovushwa salama kutoka katika utumwani huko Misri, na waliokuwa wakitembea kwa uhuru kuelekea Nchi ya ahadi. Kwanza kabisa walilalamika kuhusu chakula, Mungu akawapa mana, mkate kutoka mbinguni. Hata baada ya kuona muujiza huu bado hawaja uamini upendo wa Mungu. Wakaanza kukusanya zaidi ya mahitaji yao, lakini yote iliharibika siku iliofuata. Alafu wakaanza kulalamika kwasababu ya maji. Pamoja na hilo Mungu akafanya muujiza mwingine akawapa maji. Lakini Israeli hakujifunza kumtuminia Mungu. Mwanadamu ni kiumbea ambaye haridhiki. Mahitaji yetu daima tunaona hayatoshi, yanaendelea kuongezeka daima. Ni kama vile kula chumvi, unahisi kiu kila wakati, alafu baadae unakula tena chumvi unahisi kiu tena.

Katika somo la Injili tunamuona huyu Mwanamke msamaria ambaye pia alikuwa akiishi maisha yake yasio pendeza. Alikuwa katika kisima ili kutuliza kiu yake ya kila siku. Alikuwa anajiribu kutuliza kiu ya mwili wake kwa kila aina ya anasa. Lakini kila siku alikuwa akirudi katika kisima kwa ajili ya maji. Yeye kama ilivyo kwa wanadamu wote ni lazima alisimama nakuuliza “hivi kuna aina ya maji ambayo nikinywa sintaona kiu tena?”. Mt. Agustino anatoa jibu anavyosema “mioyo yetu haitatulia …hadi itakapo tulia kwako Bwana Yesu”

Yesu alikuwa njiani kuelekea Yerusalemu kwa kupitia Samaria. Watu wasamaria walionekana kama Wayahudi wasio faa au Wayahudi waliochanganyika. Hawakuwa wakichukuliwa kama sehemu ya jamii ya Wayahudi. Hata tunaona Yesu anakutana na Mwanamke Msamaria. Huyu Mwanamke alikuja katika kisima kuja kuchota maji saa sita mchana. Hii ilikuwa sio kawaida kwasababu, wanawake walikuja kuchota maji wakiwa katika makundi tena ikiwa ni hasubuhi au jioni. Huyu mwanamke inaonekana alipenda kuwakwepa wenzake pengine kwasababu ya tabia ya maisha yake ambayo Yesu alimwambia baadae. Yesu akiwa ni Myahudi anamuomba maji ya kunywa. Alikuwa na mazunguzo naye ambayo yalimlenga kutoka katika mazungumzo ya maji ya kawaida hadi kwenye maji ya uzima, kutoka katika kiu ya kidunia hadi kiu ya kiroho. Anashindwa kumtambua Yesu hapo mwanzo, na Yesu anirarua dhamiri yake kwa kufunua ukweli wa maisha yake. Hili lilikuwa rahisi kwake kupokea neema ya Mungu. Yesu anamsaidia katika hali ya kukuwa na kutambua kumwadudu na hapo anamtambua Yesu kama Masiha. Baada ya kumtabua Yesu, analeta kijiji kizima kwake. Mwanamke ambaye alikuwa amekataliwa na jamii anakuwa chombo cha Mungu cha kuwaleta wanakijiji kwa Yesu. Alikuja kuchukua maji ya kawaida akarudi na maji ya uzima. Yesu hakunywa hata tone moja la maji, lakini kiu yake ilitulizwa kwa kupata roho moja kwa ajili yake.

Yesu alijua yote kuhusu huyu Mwanamke lakini alitaka kumpa maji ya uzima. Alitaka kuzima kiu ambayo yeye alikuwa

nayo rohoni mwake. Alivyokuwa akiongea naye, na kuanza kumsikiliza kiu yake ilianza kuzimwa. Ilianza kuzimwa kwasababu ndicho alichohitaji, tunachohitaji wote, ni upendo huu kamili na kukubaliwa na Yesu, ambao Yesu anautoa mwenyewe. Alitoa kwake, na anataka kuutoa kwetu pia. Cha kushangaza Mama huyu aliondoka na kuacha “mtungi”. Hakuchukua maji aliokuwa amekuja kuchukua. Au alichukuwa? Katika hali hii ya kuacha mtungi ni alama kwamba kiu yake ilikuwa imezimwa kwa kukutana na Yesu. Hakuwa tena na kiu, Yesu alizima kiu yake.

Katika kuishi kwetu kila siku, tunajikuta tukimwacha Mungu na kutafuta mambo yanayo pita. Tunafatilia tukitafuta maana katika hivyo vitu lakini tunakuta hamna, ni utupu ndani yake. Tutafakari juu ya kiu isiopingika tulio nayo ndani mwetu. Tukisha itambua, tuelekeze dhamiri zetu kumwelekea Yesu ili azime kiu yetu kwa maji ya uzima. Tukifanya hivi, tutaacha mitungi mingi ambayo kwakweli haizimi kiu yetu.

Sala: Bwana, wewe ni maji ya uzima ambayo roho yangu inatafuta. Ninakuomba nikutane na wewe katika maisha yangu, katika aibu yangu na maumivu ya moyo. Ninaomba nikutane na upendo wako, upole wako na kukukubali sasa, ninaomba upendo wako uwe chanzo cha maisha yangu ndani yako. Yesu nakuamini wewe. Amina.

Tabia Takatifu ya Kwaresima: KUZIMA KIU-ninakuomba nigawe maji ya kumaliza kiu ya watu, wakiwa ni wahitaji, omba omba, ninaomba iwe kazi yangu. Ninaomba pia nizime kiu yangu ya kiroho kwa kutafakari juu ya neno lako na kwa kupata neema kutoka katika maisha ya sakramenti. Ninaomba niwalete wengine nao waweze kutuliza kiu yao pia. Amina.