RAIS John Magufuli Machi 13, 2020 amewaomba Watanzania kuzingatia tahadhari dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona kwa kuwa hakuna dawa ya kutibu ugonjwa huo bali kinachotibiwa ni dalili tu.

 

Ameyasema hayo akizindua karakana ya matengenezo ya magari na mafunzo ya ufundi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), iliyopo Lugalo Jijini Dar es Salaam

Alichokisema Magufuli:
“Ugonjwa huu unaharibu uchumi, tusidharau tahadhari, niwaombe ndugu zangu tuzingatie tahadhari, kila mtu katika eneo lake achukue tahadhari ya Corona, tukidharau tutakwisha, mpaka leo hakuna dawa, wanatibu dalili tu.
“Napenda nirudie ndugu zangu Watanzania, ni vizuri sana tukaendelea kuchukua tahadhari kwa nguvu zote, ugonjwa huu unaua na unaua kwa haraka, tusipuuze hata kidogo ugonjwa huu, kama una safari isiyo ya lazima sana usisafiri.

“Vyombo vya ulinzi na usalama simamieni mipaka yetu ili kila anayeingia awe amepimwa na ugonjwa huu wa Corona ili tusijekaribisha janga ambalo madhara yake ni makubwa katika taifa letu.”