SOMO 1 Isa. 1:10, 16-20 Lisikieni neno la Bwana, enyi waamuzi wa Sodoma; tegeni masikio msikie sheria ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora.
Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; achene kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane.
Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.
Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha Bwana kimenena haya.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 50:8-9, 16-17, 21, 23 (K) 23
(K) Autengenezaye mwenendo wake, Nitamwonyesha wokovu wangu.
Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako,
Na kafara zako ziko mbele yangu daima.
Sitatwaa ng’ombe katika nyumba yako,
Wala beberu katika mazizi yako. (K)
Una nini wewe kuitangaza sheria yangu,
Na kuliweka agano langu kinywani mwako?
Maana wewe umechukia maonyo,
Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako. (K)
Ndivyo ulivyofanya, nami nikanyamaza,
Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe,
Atoaye dhabihu za kushukuru, ndiye anayenitukuza.
Naye autengenezaye mwenyendo wake,
Nitamwonyesha wokovu wa Mungu. (K)
SHANGILIO
Mt. 4:17
Tubuni asema Bwana, kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.
INJILI
Mt. 23:1-12
Yesu aliwaambia makutano na wanafunzi wake, akasema, Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa; basi, yoyote watakayowaambia, myashike, na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi. Wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao. Tena matendo yao yote huyatenda ili kutazamwa na watu; kwa kuwa hupapanua hirizi zao, huongeza matamvua yao; hupenda viti vya mbele katika karamu, na kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu, Rabi.
Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni. Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu. Na yeyote atakayejikweza atadhiliwa; na yeyote atakayejidhili atakwezwa.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
*ASALI MUBASHARA-Jumanne 10/03/2020*
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari ya neno la Bwana tunaanza kwa kuiangalia zaburi ya wimbo wa katikati ambapo Mwenyezi Mungu anasisitiza kwamba yeyote autengenezaye mwenendo wake atampatia rehema zake. Hii ni zaburi inayotualika tumrudie
Bwana kwani kwa kumrudia hata kama dhambi zetu ni nyekundu kama bendera, pale tutakaomrudia hakika hatatuacha kwani yeye hafurahii kifo cha mtu muovu. Ujumbe wa namna hii ndio nabii Isaya anaowasisitizia wana wa Israeli waufuate. Katika somo la kwanza, anawalinganisha na wana wa Sodoma kwani wamezidi kwa uovu; walikwenda kujiunga na mataifa jirani na huko walijifunza uovu tu, walijifunza uasherati, wakafuata tamaduni mbovu za hawa mataifa.
Hiki kiliwafanya wafukuze Baraka za Mungu zilizokuwa zinatakiwa ziwafuatie; waliishia kulaaniwa na kuishi katika maisha magumu, ukame ukaharibu mazao yao, wakapatwa na njaa kali na mambo yakawa mabaya sana. Sasa nabii Isaya anawaalika wamrudie Mungu tu licha ya kwamba walikwisha muudhi hivyo naye atawaokoa.
Somo hili linatufaa hata sasa kwa kipindi hiki cha kwaresma. Kuna nyakati ambazo tumeikaribisha dhambi, tukaifurahia na kuishi nayo ndugu zangu. Kitendo hiki kimetufanya tukose rehema za Mungu, labda sasa tunalalamika, watu tunaishi pembeni kabisa mwa rehema za Mungu, tumejifungia rehema na neema za Mungu, tunaomba hatupati, tumeingia katika ukame wa kiroho, tunateseka, tunagombana na wenzetu kila siku, maisha hatuna raha-huu ni wakati wa kumuomba Mungu na kumrudia. Hiki kipindi sio cha kukosa neema, tusikubali tuendelee au kuishi nacho hivyo. Hiki hutufanya tusijisikie vibaya sana.
Katika injili yetu, tutasikia Yesu akiwaamuru wanafunzi wake kusikia mafundisho ya Mafarisayo kwani mafundisho yao ni mazuri lakini matendo yao ni mabaya. Hivyo, kama watafaulu kufuata mafundisho yao hakika wataokoka lakini endapo watafuata matendo yao hakika watapotea kama wafarisayo wenyewe wanavyopotea. Wafarisayo waliishia kuwa na mwenendo mbaya wa maisha kwa sababu ya sifa walizozipokea. Mwanzoni kwenye karne ya tatu BC kilianza kama kikundi kizuri-cha kumtukuza Mungu, kikafanya matendo mengi ya huruma, watu wakawapenda na kuwafurahia na kuwapa sifa nyingi. Wakaaminiwa na watu na watu kuwapatia madaraka makubwa. Sasa wakajisahau, wakaanza kutumia nafasi zao kupata heshima, tofauti na lengo lao la mwanzoni. Hivyo, sifa ziliwavimbisha vichwa kiasi cha kusahau lengo lao la kuwasaidia watu na kuishia kuwa watesi wa watu, wanyonyaji wakubwa. Nasi tunaalikwa kuwa makini na sifa tuzipatazo. Sifa itakupatia madaraka, na watu watakuamini lakini bila kuwa makini hiyo sifa yaweza kuwa chanzo cha wewe kuanguka. Kipindi hiki tujiangalie ni sifa zipi ambazo zilishawahi kutufanya tuanguke, mwanzoni ulikuwa safi lakini sifa Fulani inakuangusha. Tuwe makini na sifa tuwezazo kupewa. Tusikubali zituangushe, kila sifa unayopokea iangalie hasara itakayokuletea kiroho. Wengine walisifiwa tu na wanawake wakaishia kuwapa hata magari na mali zao, nakuacha familia ikiyumba.
:copyright:Pd. Prosper Kessy OFMCap.
*NB: SHAJARA ZA 2020 ZA ASALI MUBASHARA -Zenye tafakari ya kina zipo zakutosha wasiliana nami 0755444471 au 0714002466. Jipatie shajara hii ikufundishe namna ya kuchambua masomo na jinsi ya kujisogeza karibu na Mungu kwa njia ya Neno lake, “Kutokufahamu maandiko nikutokumfahamu Kristo”-Mt.Jerome.*