ASALI MUBASHARA-Jumanne 10/03/2020

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari ya neno la Bwana tunaanza kwa kuiangalia zaburi ya wimbo wa katikati ambapo Mwenyezi Mungu anasisitiza kwamba yeyote autengenezaye mwenendo wake atampatia rehema zake. Hii ni zaburi inayotualika tumrudie
Bwana kwani kwa kumrudia hata kama dhambi zetu ni nyekundu kama bendera, pale tutakaomrudia hakika hatatuacha kwani yeye hafurahii kifo cha mtu muovu. Ujumbe wa namna hii ndio nabii Isaya anaowasisitizia wana wa Israeli waufuate. Katika somo la kwanza, anawalinganisha na wana wa Sodoma kwani wamezidi kwa uovu; walikwenda kujiunga na mataifa jirani na huko walijifunza uovu tu, walijifunza uasherati, wakafuata tamaduni mbovu za hawa mataifa.
Hiki kiliwafanya wafukuze Baraka za Mungu zilizokuwa zinatakiwa ziwafuatie; waliishia kulaaniwa na kuishi katika maisha magumu, ukame ukaharibu mazao yao, wakapatwa na njaa kali na mambo yakawa mabaya sana. Sasa nabii Isaya anawaalika wamrudie Mungu tu licha ya kwamba walikwisha muudhi hivyo naye atawaokoa.

Somo hili linatufaa hata sasa kwa kipindi hiki cha kwaresma. Kuna nyakati ambazo tumeikaribisha dhambi, tukaifurahia na kuishi nayo ndugu zangu. Kitendo hiki kimetufanya tukose rehema za Mungu, labda sasa tunalalamika, watu tunaishi pembeni kabisa mwa rehema za Mungu, tumejifungia rehema na neema za Mungu, tunaomba hatupati, tumeingia katika ukame wa kiroho, tunateseka, tunagombana na wenzetu kila siku, maisha hatuna raha-huu ni wakati wa kumuomba Mungu na kumrudia. Hiki kipindi sio cha kukosa neema, tusikubali tuendelee au kuishi nacho hivyo. Hiki hutufanya tusijisikie vibaya sana.

Katika injili yetu, tutasikia Yesu akiwaamuru wanafunzi wake kusikia mafundisho ya Mafarisayo kwani mafundisho yao ni mazuri lakini matendo yao ni mabaya. Hivyo, kama watafaulu kufuata mafundisho yao hakika wataokoka lakini endapo watafuata matendo yao hakika watapotea kama wafarisayo wenyewe wanavyopotea. Wafarisayo waliishia kuwa na mwenendo mbaya wa maisha kwa sababu ya sifa walizozipokea. Mwanzoni kwenye karne ya tatu BC kilianza kama kikundi kizuri-cha kumtukuza Mungu, kikafanya matendo mengi ya huruma, watu wakawapenda na kuwafurahia na kuwapa sifa nyingi. Wakaaminiwa na watu na watu kuwapatia madaraka makubwa. Sasa wakajisahau, wakaanza kutumia nafasi zao kupata heshima, tofauti na lengo lao la mwanzoni. Hivyo, sifa ziliwavimbisha vichwa kiasi cha kusahau lengo lao la kuwasaidia watu na kuishia kuwa watesi wa watu, wanyonyaji wakubwa. Nasi tunaalikwa kuwa makini na sifa tuzipatazo. Sifa itakupatia madaraka, na watu watakuamini lakini bila kuwa makini hiyo sifa yaweza kuwa chanzo cha wewe kuanguka. Kipindi hiki tujiangalie ni sifa zipi ambazo zilishawahi kutufanya tuanguke, mwanzoni ulikuwa safi lakini sifa Fulani inakuangusha. Tuwe makini na sifa tuwezazo kupewa. Tusikubali zituangushe, kila sifa unayopokea iangalie hasara itakayokuletea kiroho. Wengine walisifiwa tu na wanawake wakaishia kuwapa hata magari na mali zao, nakuacha familia ikiyumba.

©Pd. Prosper Kessy OFMCap.

NB: SHAJARA ZA 2020 ZA ASALI MUBASHARA -Zenye tafakari ya kina zipo zakutosha wasiliana nami 0755444471 au 0714002466. Jipatie shajara hii ikufundishe namna ya kuchambua masomo na jinsi ya kujisogeza karibu na Mungu kwa njia ya Neno lake, “Kutokufahamu maandiko nikutokumfahamu Kristo”-Mt.Jerome.