SOMO 1 ..Yoe. 2:12-18 Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea; rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya. N’nani ajuaye kwamba hatarudi na kugeuka, na kutuachia Baraka nyuma yake, naam, sadaka ya unga, na sadaka ya kinywaji, kwa Bwana, Mungu wenu?

Pigeni tarumbeta katika Sayuni, takaseni saumu, kusanyeni kusanyiko kuu; kusanyeni watu, litakaseni kusanyiko, kusanyeni wazee, kusanyeni watoto, na hao wanyonyao maziwa; bwana arusi na toke chumbani mwake, na bibi arusi katika hema yake.
Hao makuhani, wahudumu wa Bwana, na walie kati ya patakatifu na madhabahu, na waseme, Uwaachilie watu wako, Ee Bwana, wala usiutoe urithi wako upate aibu, hata mataifa watawale juu yao; kwani waseme kati ya watu, Yuko wapi Mungu wao?
Hapo ndipo Bwana alipoona wivu kwa ajili ya nchi yake, akawahurumia watu wake.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 51:1-4, 10-12, 15 (K) 1

(K) Uturehemu, Ee Bwana, kwa kuwa tumetenda dhambi.

Ee Mungu, nirehemu,
Sawasawa na fadhili zako.
Kiasi cha wingi wa rehema zako,
Uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa na uovu wangu,
Unitakase dhambi zangu. (K)

Maana nimejua mimi makosa yangu,
Na dhambi yangu I mbele yangu daima.
Nimekutenda dhambi Wewe peke yako,
Na kufanya maovu mbele za macho yako. (K)

Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu
Usinitenge na uso wako,
Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. (K)

Unirudishie furaha ya wokovu wako;
Unitegemeze kwa roho ya wepesi.
Ee Bwana, uifumbue midomo yangu,
Na kinywa change kitazinena sifa zako. (K)

SOMO 2
2 Kor. 5:20 – 6:2

Ndugu zangu, basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu. Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye.
Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure. Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nilikusaidia; tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

SHANGILIO
Zab. 95:8

Msifanye migumu mioyo yenu; msikie sauti ya Bwana.

INJILI
Mt. 6:1-6, 16-18

Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampatai thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu. Amini, nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume; sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.
Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amini, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.
Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa nafunga, Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

*ASALI MUBASHARA- JUMATANO YA MAJIVU 26/02/2020*

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo tunaanza kipindi muhimu katika mwaka wa kanisa-kipindi cha kwaresma na kinaanza kwa Jumatano ya majivu tunayoianza leo. Hiki ni kipindi ambacho kanisa hutafakari mateso ya Kristo kwa undani zaidi na sadaka yake msalabani. Ndani ya mateso yake Kristo tunakutana na upendo ambao ndio sababu zilizomfanya yeye ateseke kwa lengo la kufuta hatia zetu. Kwa sababu Kristo aliteseka kwa ajili ya dhambi zetu, kipindi hiki kwa namna ya pekee huwa ni kipindi kinachotuhitaji sisi kutafakari juu ya mwenendo wetu wa maisha na kuona kwamba je?

Tunaishi kile Kristo alichotujia? Je kweli dunia imeacha dhambi? Tukifikiria haya ndugu zangu tunagundua kwamba bado dunia haijaacha dhambi na bado tunazidi kutenda dhambi na mbaya zaidi hatuzitumii zile njia alizotuachia Kristo kutupatanisha na Baba na kufuta dhambi zetu.
Hivyo, kipindi hiki kinapoanza kinakuwa ni kipindi cha toba na kuomba msamaha na kubadilika kwa mimi binafsi kutoka katika kuendelea kutenda dhambi na kushindwa hata kuomba msamaha kwa Mungu kwa dhambi ninazotenda na kushindwa kutumia hata zile njia zilizowekwa na Kristo mwenyewe kutuondolea dhambi. Hivyo tunaomba msamaha kwa Mungu kipindi hiki. Halafu tunamuomba Mungu msamaha kwa ajili ya makosa ya wenzetu wanaomkosea kwani katika dunia, kuna dhambi nyingi zinatendeka na watu hawataki kuomba msamaha.

Ukipatwa kuelezwa juu ya maovu yanayotendeka duniani hapa waweza hata kuzimia. Ukisikia juu ya biashara za watu wanazoanzisha utashangaa. Unakuta mtu yuko tayari kufungua kahospital chake katika nchi Fulani Fulani na kuanzisha biashara ya wizi wa viungo vya binadamu kama figo kwa ajili ya kuuziwa wale wa kupandikiza viungo “organ transplant”, baadhi ya madaktari wa nchi Fulani Fulani wanaiba viungo ndani ya miili ya wagonjwa wanavyofanyiwa operation na kwenda kuziuza kwa matajiri wenye figo mbovu. Hii ni baadhi ya uovu tu unaotendeka duniani. Watu tunakuwa waovu kuliko hata shetani. Lazima tuiombee dunia. Dhambi kama hizi zitafanya Mungu aiadhibu dunia na mmoja akiadhibiwa lazima ikuadhiri na wewe pia kwani duniani tunaishi kwa undugu. Kaka yangu akiadhibiwa, na mimi nitaumia tu.

Hivyo, kipindi hiki ni cha kuomba msamaha kwa jili ya makosa yetu na ya dunia nzima. Kama unajiona huna dhambi, basi omba kwa ajili ya wenzako.

Na katika kipindi hiki, tunaalikwa kufunga na kutenda matendo ya huruma. Haya ni matendo ya sadaka yenye umuhimu mkubwa. Matendo ya huruma na kufunga yanatuandalia njia. Yatatupatia furaha kubwa, yatatufanya tusamehewe dhambi zetu na kuwaletea wengine unafuu katika maisha yao.

Hicho ndicho kipindi chetu cha kwaresma ndugu zangu na leo kama Jumatano ya majivu, tunaanza kipindi hiki na neno la Mungu siku ya leo linatualika vyema katika kutafakari siku hii.

Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha nabii Yoeli. Huyu nabii aliishi kwenye miaka ya 400BC na katika wakati wake kulitokea nzige waliosababisha njaa kali sana na watu na mifugo kufa na uchungu mkubwa ukaenea kati ya watu. Yeye alitumwa na Mungu kuwatangazia watu kwamba nzige wale ni adhabu toka kwa Mungu kutokana na dhambi zao na hivyo alitangaza mfungo na kuwaambia kwamba huo ndio ungewaokoa katika mapigo ya nzige hao. Na ukweli ni kwamba watu walipotubu, wale nzige waliondoka na njaa kuisha na watu kuacha kufa tena. Hizi ni habari njema kwetu sisi ndugu zangu. Hakuna popote pale ambapo mwanadamu au mkristo amesisitiza kufunga na kusali halafu Bwana akamuacha. Nakwambia, kachunguze-kufunga na kusali ni nyenzo muhimu.

Hata Yesu mwenyewe alisema kwamba kwa baadhi ya mapepo, hasa yale yenye nguvu Zaidi, yanatoka tu kwa njia ya sala na kufunga. Kufunga hukufanya ushiriki pamoja na Yesu katika mateso yake, huufanya mwili na moyo usafiri na Yesu na kuufanya utulie na uwe katika mstari. Na hapa mwanadamu hupata kuungana na Bwana kwa namna ya ajabu na hivyo kuurudisha urafiki tena. Ndio maana hata ukisikia mtu anakuambia kwamba atakwenda kufunga na kusali kwa ajili yako na ukute kweli umemdhulumu, mwogope sana. Ogopa, kama unajua maana y

a haya matendo mawili, nakwambia utaogopa ajabu. Hivyo, ndugu zangu kufunga na kusali ni kwa muhimu sana kwetu.

Katika injili ndugu zangu tunakutana na Yesu akitoa hotuba yake ya mlimani akizungumzia namna ya kusali na kufunga na kufanya matendo ya huruma. Injili hii ni ya muhimu kwetu sana. Hii ni kwa sababu kila kwaresma tunajua kwamba kweli kufunga na kusali na kutoa matendo mema humfurahisha Bwana na kuturudishia urafiki naye. Lakini tatizo ni namna tunavyoyatendaga haya matendo. Unakuta tunayatumia bila Imani au kwa lengo la kujionyesha na ndio maana huwa hayatuleteagi faida. Hivyo, ili yatuletee faida, lazima kufuata kile injili inachosema.

Hivyo, kufunga utafunga, utasali na kutoa sadaka lakini tatizo litabakia kwenye namna unavyofanya. Kwa lengo ghani? Umedhamiria? Haya ndio yatakayotuletea mabadiliko kwenye kwaresma yetu. Hiyvo ndugu zangu tusisitizie juu namna ya kufanya haya matendo tunayofanyaga. Wengi hatupati neema kwa sababu tunakosa namna nzuri ya kuyafanya kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu.

:copyright:Pd. Prosper Kessy OFMCap.

*NB: SHAJARA ZA 2020 ZA ASALI MUBASHARA -Zenye tafakari ya kina zipo zakutosha wasiliana nami 0755444471 au 0714002466. Jipatie shajara hii ikufundishe namna ya kuchambua masomo na jinsi ya kujisogeza karibu na Mungu kwa njia ya Neno lake, “Kutokufahamu maandiko nikutokumfahamu Kristo”-Mt.Jerome.*